Waziri wa mambo ya Ndani,Dk Emmanuel Nchimbi.
ASKARI wa Shirika la Upelelezi la Marekani
(FBI), wamewasili Zanzibar kufanya uchunguzi wa kuwabaini waliomuua kwa
kumpiga risasi, Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki.
Kamishna wa Polisi wa Zanzibar, Mussa Ali
Mussa alisema kwa simu jana kuwa wapelelezi wa kigeni wamewasili
Zanzibar na tayari na wameanza kazi hiyo.
Wapelelezi hao wameingia
kazini kushirikiana na wenzao wa Tanzania kuwasaka wauaji wa padri huyo
aliyepigwa risasi Februari 17, mwaka huu.
Padri Mushi aliuawa asubuhi alipokuwa akienda
kuongoza ibada katika Kanisa la Mtakatifu Teresia, Beit el Raas, nje
kidogo ya Mji wa Zanzibar na kuzikwa Kitope, Kaskazini Unguja Februari
20, mwaka huu.
“Wapelelezi kutoka nje wamefika na wapo kazini,” Kamishna Mussa alisema bila ya kutaja wanatoka nchi gani.
Pia Kamishna Mussa hakutaka kueleza ni lini
wapelelezi hao walifika Zanzibar na idadi yao kwa maelezo kwamba hizo ni
siri za Polisi na zikivuja, zitaingilia uchunguzi wanaoufanya.
Hata
hivyo, vyanzo vya ndani ya Serikali, vililithibitishia gazeti hili kuwa
FBI walikuwa wameanza kuwasaka wauaji wa Padri Mushi.
Kutua kwa wapelelezi hao wa Marekani
kunafuatia kauli iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete katika salamu zake
za rambirambi baada ya mauaji ya Padri Mushi kuwa ameliagiza Jeshi la
Polisi kutumia nguvu zake zote pamoja na kushirikiana na vyombo vingine
vya usalama vya ndani na mashirika ya upelelezi ya nchi rafiki katika
kufanya uchunguzi wa mauaji hayo.
Awali, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk
Emmanuel Nchimbi alihusisha tukio hilo na vitendo vya ugaidi wakati
akitoa tamko la Serikali na kueleza kuwa Rais Kikwete ameidhinisha
Serikali kugharamia wapelelezi kutoka nje.
Pia ujio wa FBI unaweza kuhusishwa moja kwa
moja na dhamira iliyoonyeshwa mapema na Serikali ya Marekani iliyokuwa
tayari kusaidia upelelezi wa mauaji hayo na hiyo ilibainishwa katika
salamu za rambirambi za kifo hicho na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso
Lenhardt.
Vyanzo mbalimbali kutoka ndani ya Serikali vimeeleza kuwa
kabla ya kuanza kwa operesheni hiyo, maofisa wa FBI walifanya mazungumzo
na Waziri Nchimbi na viongozi wengine wa Serikali kwa ajili ya
kuangalia ni namna gani watafanya shughuli hiyo.
“Pia hawa jamaa wa FBI walifanya vikao na
maofisa wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), ili kuweka sawa
mazingira ya kufanya upelelezi huu,” kilisema chanzo kingine.
Habari zaidi zinaeleza kuwa uchunguzi wa
wapelelezi hao wa FBI na wale wa Tanzania hautajikita katika kusaka
wauaji wa Padri Mushi pekee, bali watakwenda mbali zaidi na kuchunguza
wale wote wanaojihusisha na wimbi la vurugu za kidini nchini ambalo
linatishia amani.
Hii itakuwa mara ya pili kwa FBI kuja nchini
kufanya operesheni kubwa ya upelelezi. Mwaka 1998 walifika kuchunguza
kulipuliwa kwa Ubalozi wa Marekani na kugundua kuwa Kundi la Al-Qaeda
lilihusika.
Aidha hiyo ni mara ya tatu kwa wapelelezi wa
Tanzania kushirikiana na wageni kuchunguza matukio ya uhalifu baada ya
mwaka 1984, Idara ya Upelelezi ya Uingereza, Scotland Yard ya Uingereza
kuchunguza kuungua kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Habari zaidi zinaeleza kuwa kabla ya ujio wa FBI, Serikali ya
Tanzania ilizungumza na taasisi za upelelezi za nchi tano ili kuongeza
nguvu. Taasisi nyingine zinazodaiwa kuombwa kufanya kazi hiyo ni pamoja
na Scotland Yard na Shirika la Upelelezi la Israel, Mossad.
Akizungumzia upelelezi wa mauaji ya Padri
Mushi, Kamishna Mussa alisema watu kadhaa wametiwa mbaroni kwa mauaji
lakini asingeweza kutaja idadi.
Kuuawa kwa padri huyo ni miongoni mwa matukio
ya kushambuliwa kwa viongozi wa dini huko Zanzibar baada ya kumwagiwa
tindikali Katibu wa Mufti, Fadhil Soraga, kupigwa risasi kwa Padri
Ambrose Mkenda wa Kanisa Katoliki na kuuawa kwa Sheikh Ali Khamis
shambani kwake huko Kidoti, Mkoa wa Kaskazini Unguja
No comments:
Post a Comment