Bilionea Bongo asajiri First 11 ya Dunia

Cristiano Ronaldo

MMILIKI wa klabu ya Soka ya Azam, Said Salim Bakhressa ametajwa kuwa miongoni mwa watu 40 wenye utajiri mkubwa barani Afrika.

Bakhressa, ambaye amejikuta zaidi katika biashara ya usindikaji wa vyakula na masuala ya usafiri anakadiriwa kuwa na utajiri wa Dola za Marekani kiasi cha Dola bilioni moja (Sh. 1.6 Trilioni za Tanzania).

Vyanzo vya mapato vya Bakhressa

Utajiri wa Bakhressa unatokana na biashara zinazofanywa na kampuni zake yaliyoko chini ya Bakhressa Group inayofanya biashara mbalimbali katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Biashara hizo ambazo zinasimamiwa na watoto wake ni pamoja na usagishaji nafaka, usindikaji na uuzaji wa bidhaa za ngano, vinywaji baridi, usafiri wa majini na upangishaji majumba.

Kwa mujibu wa jarida maarufu la Forbes la Marekani linaripoti kuwa mwaka jana Bakhressa alitengeneza kiasi cha Dola 800 milioni sawa na Sh 1.2 trilioni.

Bakhressa, ambaye alizaliwa mwaka 1949, alianzia chini kabisa kwa biashara ya migahawa kabla ya kununua mashine za kusaga na kukoboa nafaka.

Utajiri wa Bakhressa ni habari njema kwa soka la Tanzania ambalo kwa miaka mingi limekuwa likitumiwa kama ngazi ya watu kuchuma fedha au kupata nafasi za kisiasa kama ubunge.

Hata hivyo, Bakhressa amekuwa tofauti kwani ameanzisha timu yake tofauti na matajiri wengine.

Amewekeza mabilioni kwenye soka

Tajiri huyo, ambaye alikuwa kiongozi wa Simba kwenye miaka ya 1980, alianzisha timu yake ya Azam mwaka 2004, ambayo ni kati ya vigogo vya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Bakhressa ambaye aliachana na soka baada ya kuudhiwa na migogoro katika klabu aliyoipenda ya Simba, alipata wazo la kuanzisha timu akiamini atatengeneza soko jipya la ajira kutokana na ukweli kuwa vijana ndio wanunuzi wa bidhaa zake kama lamba lamba kiasi cha timu yake kupewa jina la utani la 'Wana lamba lamba'.

Ametumbukiza kiasi cha Sh 1.3 bilioni katika ujenzi wa kituo kisasa cha soka ambacho kina uwanja wenye kiwango cha kimataifa, hosteli, gym, bwawa la kuogelea na basi la kisasa kwa ajili ya timu.

Uwanja wa Azam una nyasi bandia sawa na zile zilizoko katika Uwanja wa San Siro ulioko Milan, Italia na hutumika kwa mechi za Ligi Kuu, Kombe la Kagame na hata mashindano ya Chalenji.

Katika kipindi kifupi alichoanzisha timu hiyo, tayari imetikisa kwani katika siku za karibuni imetwaa Kombe la Mapinduzi, imeshika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2011/12 na ilifurukuta mwaka huu kwenye fainali ya Kombe la Kagame.

Azam kwa mara ya kwanza italipeperusha taifa kwenye mashindano ya Afrika baada ya kukata tiketi ya kushiriki katika Kombe la Shirikisho mwakani.

Ana uwezo wa kuwaleta mastaa wa dunia

Kutokana na utajiri wa Bakhressa wa zaidi ya Sh trilioni moja ina maana ana uwezo wa kuwaleta mastaa bora duniani.

Ifuatayo ni orodha ya mastaa wanaotamba duniani na bei yao inakadiriwa kwa ujumla wao kuwa kiasi cha Sh 1.2 trilioni na ukilinganisha na utajiri wa Bakhressa basi mastaa hao wanaweza kuletwa Azam bila ya wasiwasi wowote.

1.Gigi Buffon

Buffon ambaye ni kipa wa Juventus na Italia anaaminika kuwa kipa bora na ghali zaidi duniani. Alihamishwa kutoka Parma na kujiunga na Juventus kwa ada iliyogharimu Sh 109 bilioni za Tanzania.

2.David Alves

Alves ndiye beki wa kulia wa bei mbaya zaidi duniani. Beki huyo anatamba na Barcelona na Brazil kutokana na umahiri wake wa kupanda mbele na kupandisha mashambulizi ya hatari. Ada yake ni Sh 60 bilioni za Tanzania.

3.Jordi Alba

Ni beki mpya wa kushoto wa Barcelona. Pia anachezea timu ya taifa ya Hispania na uhamisho wake uligharimu Sh 28 bilioni kutoka Valencia ili kujiunga na Barcelona.

4.Nemanja Vidic

Beki huyo wa Manchester United ni kati ya mabeki bora wa kati duniani. Bei ya raia huyo wa Serbia ni Sh 40 bilioni.

5.Thiago Silva

Ni kati ya mabeki wa kati bora duniani. Ni raia wa Brazil anayechezea Paris St. Germain ya Ufaransa. Ukimtaka inabidi kujipapasa kiasi cha Sh 64 bilioni.

6.Xabi Alonso

Anatamba kama kiungo mkabaji. Kila mmoja ameona ufanisi wake katika kikosi cha Real Madrid na timu ya taifa ya Hispania. Ada yake Sh 40 bilioni.

7.Xavi Hernandez

Ndiye kiungo bora duniani. Anasifika kwa pasi zake za uhakika ambazo zimefanya klabu yake ya Barcelona na Hispania kuwa moto wa kuotea mbali duniani. Bei yake ni Sh 32 bilioni.

8.Andreas Iniesta

Kiungo huyo wa Barcelona ndiye mwanasoka bora wa Ulaya. Mkali huyo, ambaye alilelewa katika timu za yosso za Barcelona, bei yake sokoni ni Sh 28 bilioni.

9.Lionel Messi

Messi ndiye mwanasoka mahiri zaidi duniani. Zinahitajika Sh 303 bilioni ili kumsajili Muargentina Messi kutoka Barcelona.

10.Fernando Torres.

Torres ameipa Chelsea taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na mabao yake yakaisaidia Hispania kutwaa taji la Euro 2012 msimu uliopita. Bei yake ni Sh 125 bilioni.

11.Cristiano Ronaldo

Hivi karibuni, alikuwa analalama kuwa hana raha kwenye timu yake ya Real Madrid ya Hispania. Bakhressa anaweza kumchomoa kwa Dola 225 bilioni ili arudishe hamu yake na soka Chamazi.

Kikosi hicho chote kinagharimu Sh 1.2 Trilioni ambacho Bakhressa ana uwezo nazo.

Matajiri wengine wakubwa

Anachuana na tajiri namba moja barani Afrika, Aliko Dongate, ambaye ana utajiri wa Dola 10.1 bilioni.

Dangote, ambaye hivi karibuni alitangaza kuwekeza katika kiwanda cha saruji mkoani Mtwara nchini Tanzania, aliwahi kujaribu kununua klabu ya Arsenal ya England lakini bodi iligomea ombi lake.

Matajiri wengine wanaochuana na Bakhressa ni pamoja na Nick Oppenheimer wa Afrika Kusini (Dola 6.5 bilioni), Nassef Sawaris wa Misri (Dola 4.75 bilioni), Johann Rupert wa Afrika Kusini (Dola 4.7 bilioni), Mike Adenuga wa Nigeria (Dola 4.3 bilioni) na Miloud Chaabi wa Morocco.

Wengine ni Nanguib Sawris wa Misri (Dola 2.9 bilioni), Christoffel Wiese wa Afrika Kusini (Dola 2.6 bilioni) na Patrice Motsepe wa Afrika Kusini (Dola 2.5 bilioni).

Motsepe, ambaye anamiliki mgodi wa madini ya Platinum pia ni mdau wa soka kwani anamiliki Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

No comments:

Post a Comment