Dar es Salaam. Waziri wa Kazi
na Ajira, Gaudensia Kabaka amesema mwezi ujao wanatarajia kutangaza kima
cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa sekta zote.
Akizungumza jana wakati wa mkutano kuhusu sekta ya
Hifadhi ya Jamii kwa Baraza Kuu la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi
(Tucta), alisema kwa muda mrefu kiwango cha kima cha chini cha mshahara
kwa wafanyakazi wa sekta zote kilikuwa hakijabadilishwa.
“Kwa muda mrefu tulikuwa hatujatangaza kima cha
chini cha mshahara, lakini nafurahi kuwajulisha tu kwamba mwezi ujao
tutatangaza rasmi,”alisema Kabaka.
Pia alitahadharisha kuhusu utitiri wa vyama katika
sehemu moja ya kazi kushauri waajiri wasiruhusu wafanyakazi waanzishe
kwa sababu vitakosa nguvu ya kujadiliana na mwajiri katika kufunga
mikataba ya hiyari .
Waziri huyo alisema sekta ya hifadhi ya jamii ina
idadi ndogo ya wanachama waliojiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii
ukilinganisha na idadi ya nguvu kazi iliyopo ambayo ni milioni 22.
Awali Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta
ya Hifadhi ya Jamii, Irene Isaka alisema hadi sasa michango katika
mifuko hiyo imefikia Sh 1.4 trilioni na kwamba mafao yanayolipwa
yamepanda kutoka Sh500 bilioni hadi kufikia Sh 724 bilioni.
No comments:
Post a Comment