Hatima ya vigogo waliosimamishwa Tanesco kitendawili



Dar es Salaam. Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) imeendelea kusuasua kutoa majibu sahihi kuhusu hatima ya vigogo watatu, waliosimamishwa kazi mwaka jana kwa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya ofisi.
Tayari bodi hiyo imeunda jopo la watu sita kuwahoji maofisa hao kabla ya kutoa uamuzi, lakini zaidi ya mara tatu Mwenyekiti wake, Jenerali mstaafu Robert Mboma anapotafutwa kuelezea kilichobainika baada ya kuhojiwa kwa vigogo hao, amekuwa akieleza kuwa kazi hiyo itaanza baada ya wiki moja.

Uamuzi wa kuwahoji maofisa hao ulikuja baada ya bodi hiyo kukabidhiwa ripoti na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuonyesha upungufu kadhaa wa utendaji kwa watumishi hao.

Katika maelezo yake ya jana, Mboma alisema: “Tumeshapata jopo la watu sita ambao watakuwa katika makundi mawili yenye watu watatu, tumechelewa kuanza kuwahoji kwa sababu tulikuwa tukichambua mafaili ya watu wanaounda jopo hili.”
“Pia, tulikuwa tukipitia ushauri wa watu mbalimbali, ili kutokuwa na watu ambao wana mgongano wa kimasilahi na maofisa hawa wa Tanesco.”

Tangu Januari mwaka huu, Jenerali Mboma ameshazungumza na gazeti hili zaidi ya mara tatu, kila alipokuwa akiulizwa juu ya suala hilo, alisema kazi ya kuwahoji maofisa hao ingeanza baada ya wiki moja.

Maofisa hao ambao wanasubiri kuhojiwa ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji Huduma za Shirika, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi Ununuzi, Harun Mattambo.

Katika maelezo yake, Jenerali Mboma alisema ripoti ya CAG inaonyesha kuna kasoro hasa ununuzi usiofuata taratibu na ubadilishaji fedha za kigeni (dola).

“Kikubwa alichogundua CAG ni ununuzi usiofuata taratibu na suala la kubadilishwa kwa Dola za Marekani benki, ambazo Shirika halina akaunti,” alisema Mboma na kuongeza:

“Benki ambayo shirika halina akaunti na ambayo wangeweza kubadilishia fedha hizo ni Benki Kuu (BoT) pekee, lakini haikufanyika hivyo jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu.”
Alisema baada ya jopo kumaliza kuwahoji watuhumiwa hao, litawasilisha mapendekezo kwa bodi ambayo itatoa uamuzi wake.

Maofisa hao walisimamishwa kazi Julai 14, mwaka jana, sambamba na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, William Mhando ambaye baadaye alifukuzwa kazi.

No comments:

Post a Comment