Rais Jakaya Kikwete
Ripoti ya viashiria vya Ukimwi nchini katika
mwaka 2011/12 imeonyesha kuwa wasichana wenye umri wa kati ya miaka 23
na 24 wameambukizwa virusi vya Ukimwi kwa asilimia 6.6, ikilinganishwa
na wavulana wa umri huo ambao ni asilimia 2.8.
Akisoma ripoti hiyo jana jijini Dar es Salaam,
Mwenyekiti wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania, (Tacaids), Dk Fatuma
Mrisho alisema kiwango cha wasichana wa umri huo wenye virusi ni mara
mbili zaidi ya wavulana.
Akizindua ripoti hiyo, Rais Jakaya Kikwete
alisisitiza Watanzania na sekta zote zinazojihusisha na mapambano dhidi
ya Ukimwi, zitilie mkazo umuhimu wa kukomesha unyanyapaa na kuhamasisha
upimaji wa hiari.
“Watanzania zaidi ya milioni mbili wamefariki
tangu Ukimwi ugundulike miaka 30 iliyopita, tunatakiwa tupambane kwa
dhati kabisa,” alisema Rais Kikwete.
Alipongeza ongezeko la idadi ya watu waliopima kwa hiari na kuwataka wanaume kupima badala ya kuwaachia jukumu hilo wanawake.
Rais pia alizitaka taasisi za Ukimwi,
kudhibiti kasi ya maambukizi katika miji mikubwa na katika barabara kuu
zikiwemo za Chalinze na Njombe.
“Maeneo hayo yanahitaji nguvu zaidi,
hata maeneo yenye kiwango kidogo cha maambukizi nayo yasibweteke
yanahitaji tahadhari,” alisema.
Kuhusu tohara kwa wanaume, Rais Kikwete
alisisitiza zaidi tohara kwa wanaume na kwamba wasiotahiriwa wanaongeza
kasi ya maambukizi kwa asilimia 60 na wanaotahiriwa wanapunguza kwa
asilimia 60 pia.
Kwa upande wake, Dk Kikwete alisema maambukizi
kwa vijana wenye umri mdogo yanatokea wakati vijana hao wana umri wa
kati ya miaka 15 na 19 na matokeo yake kuwa wazi katika umri wa miaka 23
na 24. Alisisitiza kuwa matokeo haya ni kama ya sensa na kwamba si kila
Mtanzania mwenye umri wa miaka 14 hadi 49 amepimwa.
“Kwa jumla asilimia 2.0 ya wasichana na
wavulana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 wana maambukizi ya virusu,”
alisema. Hata hivyo ripoti hiyo ilionyesha kuwa kasi ya maambukizi kwa
Tanzania nzima, imepungua kutoka asilimia 5.8 mwaka 2008 hadi kufikia
asilimia 5.1 mwaka 2011/2012.
Utafiti wa kwanza wa aina hii ulifanywa mwaka 2003 -2004 ambapo maambukizi yalikuwa asilimia 7.06.
Utafiti mwingine ulifanyika mwaka 2009-2010 ambapo maambukizi yalishuka toka asilimia 7 hadi asilimia 5.8
Pia, ripoti hiyo ilionyesha kuwa asilimia tisa
ya wasichana na 10 ya wavulana wenye umri wa miaka 15 na 24 walianza
kujamiiana kwa mara ya kwanza kabla ya kutimiza miaka 15.
Ripoti hiyo
ilionyesha kuwa Mkoa wa Njombe una maambukizi ya juu zaidi ya asilimia
14.8 ya maambukizo kuliko mikoa yote Tanzania.
Maeneo ya visiwani yana asilimia ndogo zaidi ya maambukizi ambapo Unguja ilikuwa na asilimia 1.2 na Pemba asilimia 0.5 tu
“Matokeo
ya ripoti hii yatatupa mwanya zaidi wa kujua nini kifanyike na wapi
nguvu iongezwe katika kupambana na maradhi haya hatari,” alisema
Kikwete.
Takwimu za sasa zinaonyesha kuwa maeneo ya
mijini yana maambukizi mengi zaidi ambapo kwa wanawake ni asilimia 6.2
na wanaume ni asilimia 3.8
Ripoti hiyo ilionyesha kuwa zaidi ya robo ya Watanzania walioko kwenye ndoa wana maambukizi ya Ukimwi.
Ripoti hiyo ya kwanza na ya aina yake ilichambua pia idadi ya
wenza kati ya wanaume na wanawake ambapo kwa Tanzania nzima, asilimia 21
ya wanaume walikuwa na mwenza zaidi ya mmoja wakati ni asilimia nne tu
ya wanawake walikuwa na mwenza zaidi ya mmoja.
“Uwiano wa wanaume
wenye miaka 15 hadi 49 ambao walikuwa wamejamiiana na wenza wawili au
zaidi miezi miwili iliyopita ni zaidi ya mara tano ya uwiano wa
wanawake,” ilisema ripoti hiyo.
Uzinduzi wa ripoti hiyo ulihudhuriwa pia na
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri Wa Fedha Dk William Mgimwa, waziri wa
afya, Dk Hussein Mwinyi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Sedicy Mecky na
wadau mbalimbali wa Ukimwi nchini na nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment