Maafa ya ARV

ZAIDI YA WATU 400,000 WADAIWA KUPEWA  DAWA BANDIA NCHINI, MAMLAKA YA MADAWA YAAGIZA ZIONDOLEWE HOSPTALINI

 MAELFU ya watu walioathirika kwa ugonjwa wa Ukimwi ambao kwa sasa wanaotumia Dawa za Kurefusha Maisha (ARVs) nchini wapo hatarini kufupisha maisha yao baada ya kubainika kuwa toleo mojawapo la dawa hizo la Machi, 2011 ni bandia.   Uchunguzi wa Mwananchi unaonyesha kuwa dawa hizo zilizosambaa katika Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Mara zilianza kusambazwa tangu Mei mwaka huu na hadi sasa bado zipo sokoni, jambo lililoilazimu Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) kuagiza zirudishwe Bohari Kuu ya Dawa (MSD).  Tayari TFDA imetoa waraka ambao umesambazwa kwenda kwa waganga wakuu wa mikoa yote nchini kuwaagiza kuondoa dawa hizo kwenye mzunguko mara moja.

Mwenyekiti wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania  (Tacaids), Fatuma Mrisho aliliambia gazeti hili jana kuwa Tanzania kuna zaidi ya watu 900,000 waliojiandikisha kutumia dawa za ARV, lakini asilimia 55 ya watu hao ndiyo walioanza kutumia. Asilimia hiyo ni sawa na watu 495,000.  Barua hiyo yenye kumbukumbu namba BD.411/412/01D/58 ya Agosti 23 mwaka 2012, imesema hatua hiyo imefikiwa baada ya kufanyika kwa uchunguzi uliobaini kuwa ni bandia.

 Kwa mujibu wa barua hiyo iliyosainiwa na aliyekuwa Kaimu  Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Dk Sikubwado Ngendabanka dawa hizo hazipaswi kutumika na zinatakiwa kuondolewa sokoni mara moja.

Barua hiyo ya TFDA iliendelea kufafanua kuwa, “TFDA imefanya uchunguzi na kubaini uwepo wa dawa bandia yenye jina la biashara TT-VIR 30 (yenye mchanganyiko wa viambata hai vya Nevirapine 200mg, Lamivudine 150 mg na Stavudine 30 mg) ya vidonge inayotengenezwa na Kiwanda cha dawa cha Tanzania Pharmaceutical Industries LTD (TPI),” ilisema sehemu ya barua hiyo. Hata hivyo, taarifa za ndani ya TFDA za kiuchunguzi zinasema kwamba TPI wameonyesha kutoitambua dawa hiyo hivyo kuzidi kujenga wasiwasi iliingiaje sokoni kupitia MSD.

Iliendelea kueleza kuwa, uchunguzi wa awali ulibaini kuwa vidonge vya dawa yenye toleo namba (batch number oc.01.85) iliyotengenezwa Machi 2011 na muda wa matumizi kutarajiwa kuisha Februari 2013 viko tofauti.  “Baadhi vikiwa na kiambata hai cha Efavirez pekee na baadhi vikiwa na mchanganyiko wa viambata hai vya Nevirapine, lamivudine na Stavudine.

Aidha, baadhi ya vidonge vya toleo hili havina ubora unaokubalika ikiwa ni pamoja na kubadilika rangi na kuota fangasi,” ilisema barua hiyo.  Ilisema kuwa, Mamlaka hiyo inaendelea kufanya uchunguzi zaidi kwa nia ya kubaini mtengenezaji na msambazaji halisi wa dawa hiyo ambayo kwa sasa imepatikana katika baadhi ya hospitali za Serikali katika Mikoa ya Tanga, Mara na Dar es Salaam,” ilisema.

“Kutokana na hali hiyo, TFDA inawaomba muwaeleze Waganga Wakuu wa Wilaya, kusimamisha matumizi ya toleo tajwa katika hospitali, vituo  vya afya na zahanati na kurudisha dawa hizo kwa msambazaji (MSD), kwa hatua zaidi za kisheria,” ilisema na kuongeza.  “Endapo itabainika kuwapo kwa matoleo mengine yenye ubora wenye mashaka, taarifa zitolewe mara moja ili nayo yaweze kuondolewa kwenye mfumo wa usambazaji wa Serikali na sokoni pia.”

Akizungumzia barua hiyo jana, Mkurugenzi wa TFDA, Dk Hiiti Sillo alisema pamoja na maelekezo hayo, uchunguzi bado unaendelea ili kujua ni nani aliyetengeneza dawa hizo.  “Kama kawaida yetu sisi tukipata habari mara moja huwa tunachukua hatua ili kudhibiti madhara zaidi, kwa hiyo kweli hiyo barua ni yetu na kwa sasa wataalamu wetu wanaendelea na uchunguzi zaidi,” alisema Dk Sillo.

Alisema kuwa, suala hilo ni nyeti na linagusa maisha ya watu wengi hivyo uchunguzi lazima ufanyike kwa kina.  Dk Sillo alilieleza gazeti hili kuwa, baadhi ya mambo yanayochunguzwa ni endapo kweli dawa hiyo ni bandia na kama tarehe ya kutengeneza na kumalizika kwa matumizi yake ni sahihi.

“Tukibaini kuwa ni bandia kabisa hatua za kisheria zitachukuliwa, ila kwa sasa tunasubiri uchunguzi huo ukamilike kwa sababu pengine yawezekana tu kuwa zipo chini ya kiwango,” alisema Dk Sillo:  “Ukitaka kujua zaidi juu ya dawa hizo, hatua iliyofikia katika kuziondoa sokoni na uchunguzi wake juu ya kuwa bandia ama laa, nitafute kesho, sasa hivi niko barabarani.”

Kwa upande wa MSD, ambao ndiyo wanaodaiwa kuwa wasambazaji wa dawa hizo, walisema kuwa kupata taarifa kamili ya kiasi cha dawa kilichosambazwa na kile ambacho kimerudishwa baada ya taarifa ya TFDA, watatoa taarifa rasmi leo.  “Siwezi kusema chochote leo, nitumie barua pepe kesho kwenye saa tano nitakuwa nimekujibu,” alisema Msemaji wa     MSD, Ety Kuseluka.

Uchunguzi wa ndani ya TFDA ambao hauko katika barua iliyotumwa kwa waganga wa mikoa yote nchini unasema kwamba aina hii ya dawa feki imeanza kusambazwa Mei mwaka huu na idadi kubwa ya watu tayari wametumia na huenda wamepata madhara.

“Kwa jumla, dawa hizo zimesambazwa maeneo mengi na tayari zimesambazwa kwa wagonjwa wengi. Jambo la kusikitisha ni kuwa baadhi ya kopo hizo zina dawa aina ya Efavirenz ambazo hupaswa kutumiwa mara moja tena nyakati za usiku tu . Hivyo wagonjwa waliotumia dawa hizo wamekuwa wakitumia dawa moja (monotherapy) kwa muda mrefu na hivyo kuna uwezekano mkubwa wa virusi kujenga usugu,” ilisema taarifa hiyo ya uchunguzi. Usikose gazeti la Mwananchi kesho kupata taarifa za kina zaidi kuhusiana na dawa hizi zinazodaiwa za bandia.

No comments:

Post a Comment