Kilichomwangusha Sumaye Chatajwa


SIASA za makundi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimetajwa kuwa chanzo cha kuangushwa kwa Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye katika nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), kupitia Wilaya ya Hanang’ Mkoa wa Manyara.


 Sumaye ambaye anatajwa kuwa ana nia ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu ujao, alishindwa na Dk Mary Nagu ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji). 


Katika uchaguzi huo, Sumaye alipata kura 481 dhidi ya Nagu, aliyepata kura 648. Mbali na Sumaye, wajumbe wengine waliokuwa wakimuunga mkono akiwamo Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Goma Gwantu, pia walishindwa katika uchaguzi huo. 


Dalili za kushindwa kwa Sumaye, ambaye alikuwa akiungwa mkono na wajumbe wa kamati ya siasa ya CCM wa wilaya hiyo, zilianza kuonekana wiki moja kabla ya uchaguzi huo. Kambi ya Dk Nagu ambayo inatajwa kwamba inaungwa mkono na kambi ya Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, ilionekana kuwa na “ushawishi” mkubwa katika vikao vya kamati ya siasa ya mkoa na kwenye Kamati Kuu ya CCM. Hali hiyo, ilitokana na ukweli kuwa Dk Nagu kama taratibu ambazo zilihitajika, hakupewa baraka na kamati ya siasa ya wilaya hiyo, kugombea kwa kile ambacho kilielezwa kukwepa mpasuko wa CCM Hanang' na pia kumpa heshima Sumaye. 


Hata hivyo, habari zimeeleza kuwa tofauti na msimamo wa Kamati ya Siasa ya wilaya hiyo, Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Manyara, ilionekana kumuunga mkono Dk Nagu hasa kutokana na ukweli kuwa karibu nusu ya wajumbe wa kamati hiyo walikuwa wagombea. 


Kikao cha kamati ya siasa ya mkoa, licha ya kurejesha jina la Dk Nagu pia, kilipendekeza kuondolewa majina ya wagombea kadhaa katika wilaya ya Hanang' likiwamo jina la Mwenyekiti wa wilaya hiyo, Goma Gwaltu ambaye alikuwa kambi ya Sumaye.


 Taarifa za kupendekezwa kuondolewa majina ya wanaomuunga mkono Sumaye, zilitolewa na baadhi ya wajumbe wa Wilaya ya Hanang’, lakini hata hivyo, Katibu wa CCM Mkoa wa Manyara, Ndeng'aso Ndekubali alizikanusha. “Kamati ya siasa ya mkoa ni kikao cha siri na nadhani ni mapema mno kulalamikia suala hilo, ni vyema wakasubiri uamuzi wa juu, ” alisema Ndekubali. Hata baada ya kurejeshwa majina na Nec, ilibainika kuwa wagombea ambao Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo, iliwapa alama za chini, wamerejeshwa katika mchakato wa uchaguzi. 


 Dalili za kuanguka Sumaye, pia zilijionyesha siku ya kupiga kura, ukumbini na nje ya ukumbi kutokana na wajumbe waliokuwa wanamuunga mkono Dk Nagu kuwa na uhakika mkubwa wa ushindi. Wakati wa kujieleza ili aombe kura, Sumaye ambaye alionekana kama tayari amebaini nguvu ya Dk Nagu, alieleza kushangazwa na uamuzi wa Dk Nagu kugombea nafasi hiyo, hali ya kuwa ni waziri. 


Sumaye, pia alikemea kile alichodai kuwa ni rushwa kwenye chaguzi za CCM na kuahidi kama akichaguliwa, angeshirikiana na viongozi wenzake kuhakikisha anawachukulia hatua kali watoa rushwa. Awali Dk Nagu katika maelezo yake, alitumia fursa ya kuomba kura kukanusha kuwa anatumiwa na kundi la Lowassa ili kumkwamisha Sumaye. 


Dk Nagu alifafanua kuwa yeye kama Mbunge wa Hanang’ na Waziri, kamwe hawezi kutumiwa na kundi fulani kwa masilahi ya makundi kwani hata yeye ana sifa za kuchaguliwa. Wakati wa maswali, Dk Nagu hakuulizwa wakati Sumaye aliulizwa maswali matatu ambayo aliyajibu kwa ufasaha, lakini hakuchaguliwa. 


 Mwenyekiti wa CCM aliyeshindwa, Goma Gwaltu, alieleza kupinga mambo kadhaa yaliyokiukwa katika uchaguzi, lakini hata hivyo, alisisitiza kujiandaa kutoa tamko rasmi. “Nitazungumza siku si nyingi kuelezea uchaguzi huu,” alisema Gwaltu. 


Naye Sumaye kwa upande wake, alisema anakusudia kuzungumzia yaliyojiri katika uchaguzi huo hivi karibuni. “Naomba uwe na subira, nitawaita wanahabari na tutazungumza. Leo (jana) nimepigiwa simu na waandishi kama 50, wote nimewaambia kuwa nitazungumza siku chache zijazo,” alisema Sumaye. 


Mbunge wa Viti Maalumu Chadema, Rose Kamili ambaye kwa muda mrefu alikuwa diwani kwa tiketi ya CCM kabla ya kuhamia Chadema, alieleza kuwa Sumaye aliangushwa kwa nguvu ya fedha. Alisema kuwa kitendo cha Sumaye kutajwa kuwa anataka kuwania urais katika uchaguzi ujao ndiyo sababu ya kutoswa katika uchaguzi huo ili kupunguza ushindani. Kwa upande wake Gwaltu alisema kilichomwangusha Sumaye ni makundi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao. 


Alisema kuwa makundi hayo ambayo yameanza kujipanga kwa ajili ya kushinda katika kinyang’anyiro cha kuwania urais, yalifanya kila njia kuhakikisha kuwa Sumaye hapenyi katika hatua hiyo, lengo likiwa ni kufanya upinzani kuwa mdogo 2015. 


Kada mkongwe wa chama hicho ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Basotu, Samwel Kawoga alisema kuwa makundi hayo yalianza kuonekana wazi siku chache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo. Alisema kuwa makundi hayo ni pamoja na yale yanayoongozwa na makada wa chama hicho wanaoutaka urais na mengine ni yale yanayoibuka kila unapofanyika uchaguzi ndani ya chama hicho. 

                                                  Chanzo:http://www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment