Nahodha, mmiliki boti iliyoua Ziwa Tanganyika mbaroni
Mkurugenzi wa SUMATRA, Ahmad Kilima
Jeshi la Polisi mkoani Kigoma linawashikilia nahodha
wa boti ya MV Yarabi Tunashukuru yenye namba za usajili KST 0029,
Akilimali Seif (34) na mmiliki wake, Musiwa Omary (37), kwa tuhuma ya
kubeba abiria zaidi na mizigo kupita kiasi na kusababisha boti kupasuka
na watu 13 kufariki dunia na 67 kuokolewa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai, alisema tukio hilo
lilitokea Januari 3, mwaka huu saa 4:30 usiku katika eneo la mwambao wa
Ziwa Tanganyika katika Kjiji cha Herembe Kata ya Sigunga Wilaya ya
Uvinza.
Kashai alisema kuwa boti hiyo ilikuwa inatokea Namansi, wilayani Nkasi,
Mkoa wa Rukwa ikielekea Burundi ilikuwa imebeba abiria zaidi ya 85 na
mizigo na kusababisha boti hiyo kupasuka na kuzama katika Ziwa
Tanganyika.
Miili ya watu 13 wamepatikana wakiwa wamekufa wanaume wanne na wanawake tisa huku 67 waliokolewa wakiwa hai.
Kamanda huyo alisema wanaohofiwa kufa maji juhudi za kuwatafuta bado
zinaendelea na kwamba nahodha na mmiliki wa boti hiyo wanatarajiwa
kufikishwa mahakamani upelelezi utakapokuwa umekamilika.
Kamanda Kashai aliwataka wamiliki wa vyombo vya majini kuzingatia sheria
za usalama majini zilizowekwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi
Kavu na Majini (Sumatra).
No comments:
Post a Comment