Rais Jakaya Kikwete
Jumuiya ya Wazanzibari Waishio Tanganyika imekuja
juu ikipinga vikali mikakati ya kuwabagua inayolenga kuwatisha ili
kuwarudisha nyuma wasiendelee kudai mamlaka kamili ya Zanzibar pamoja na
Muungano wa haki na wenye maslahi kwa pande zote mbili.
Mikakati hiyo inadaiwa kufanywa na watu wa kubuni wanaojiita Umoja wa
Wapemba Waishio Tanzania Bara (Neppelta) kwa kutumia hotuba ya Rais
Jakaya Kikwete, aliyoitoa wakati akizindua Bunge Maalumu la Katiba,
Machi 21, mwaka huu.
Tamko la jumuiya hiyo lilitolewa na Mwenyekiti wake, Abdallah Mohammed Kassim, marufu kama “Dullah”, jijini Dar es Salaam juzi.
Alisema kauli ya watu hao, ambayo ilinukuliwa na baadhi ya vyombo vya
habari hivi karibuni, imeonyesha ubaguzi wa dhahiri dhidi ya
Wazanzibari, ambao kiasili ni wamoja licha ya kutenganishwa na bahari.
Abdallah alisema hawakubaliani na kauli ya watu hao iliyosisitiza kuwa
wao ni “Wapemba” kwa kuwa Zanzibar ni moja na maslahi yake ni ya wote.
“Kitendo cha kusisitiza kuwa Muungano ukivunjika watakaopata hasara ni
Wapemba ni ubaguzi kwani Wapemba ni Wazanzibar hivyo kuwabagua ni
kujenga chuki miongoni mwa raia wa visiwa hivyo viwili ambao ni wananchi
wa nchi moja,” alisema Abdallah.
Alisema Muungano uliopo ni wa nchi mbili, ambazo ni Tanganyika na
Zanzibar na kwamba, Zanzibar ni visiwa vya Unguja na Pemba, hivyo
kuendelea kuwabagua Wapemba kwa maneno na vitendo ni kutowatendea haki.
Abdallah alisema uamuzi wa Wazanzibari kuishi na kufanya kazi Tanganyika
ni haki yao ya msingi, hivyo kuwajengea hofu ni kuwanyima haki hiyo na
kuwafanya waishi kwa mashaka makubwa, kitu ambacho alisema siyo kizuri
kwa raia.
“Jumuiya ya Wazanzibari tunaoishi Tanganyika tunauliza kauli iliyotolewa
na bwana Shehe Haji Faki ambaye alijitambulisha kama Mwenyekiti wa
Wapemba waishio Bara kwa kusema idadi ya Wapemba waishio Bara
imeongezeka hadi kufikia zaidi ya watu 800,000 mwaka 2012 na mtaji wa
trilioni 1.2, takwimu hizi amezipata wapi?” alihoji Abdallah.
Alisema uhusiano na mwingiliano baina ya Wazanzibari na Watanganyika vilikuwapo kabla ya Muungano wa mwaka 1964.
Hivyo, akasema kuishi katika nchi yoyote duniani hakutegemei Muungano,
kwani wapo Watanzania wanaishi nchi mbalimbali duniani bila ubaguzi na
hata Tanzania wapo raia wengi wa kigeni wanaoishi licha ya kuwa nchi
hizo hawajaungana nazo.
“Wazanzibari waliopo Tanganyika na kumiliki ardhi na mali isiwe sababu
ya kuwatisha na kuwajengea hofu ya kudai maslahi ya nchi yao, kwani
utaifa wa mtu hauwezi kutupwa kwa sababu ya kumiliki ardhi, mali, kuoa
au kuolewa,” alisema Abdallah.
Alisema umoja uliopo miongoni mwa Watanzania unakumbusha kuwa
wanaofaidika na Muungano siyo Wazanzibari pekee, kwani faida hizo zipo
kwa raia wa pande zote mbili za Muungano.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment