Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia (Chadema),Dk. Willibroad Slaa.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia (Chadema), Dk.
Willibroad Slaa, amewataka Watanzania kutambua kuwa hakuna chama cha
upinzani ambacho kina lengo la kuvunja Muungano bali yanayoelezwa ni
njama ya kudhoofisha msimamo wa kuwapo kwa serikali tatu.
Alitoa kauli hiyo jana katika viwanja vya Tangamano, alipokuwa
akiwahutubia wakazi wa jiji la Tanga, baada ya kuongoza timu ya viongozi
wa juu wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) mjini hapa na kuwataka
wakazi wa jiji hilo kukataa hadaa zinazofanywa kwa lengo la kukanyaga
rasimu ya katiba, ambayo waliitolea maoni yao.
Alisema kilichofanywa na Rais Jakaya Kikwete, wakati akilihutubia Bunge
Maalumu la Katiba kuiponda rasimu ya katiba ni kumdhalilisha aliyekuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, ambaye
ni kiongozi mwenye heshima Tanzania na nje ya nchi na kwamba, Ukawa
itazunguka nchini kote kumtetea.
Dk. Slaa ambaye ni Mwenyekiti wa Ukawa nje ya Bunge hilo, alisema Rais
Kikwete anawahadaa wananchi anaposema wanaotaka serikali tatu wana lengo
la kuvunja Muungano na kusisitiza kuwa hakuna chama chochote cha
upinzania, ambacho kinataka Muungano uvunjike.
“Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na wananchi wote wa Tanzania Bara na hata
visiwani, hakuna anayetaka Muungano uvunjike, bali kinachofanywa na CCM
ni kuwachonganisha kwa wananchi ili waonekane ni maadui wa Muungano,”
alisema Dk. Slaa.
Alisema inasikitisha kuona kuwa kuna baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar
ndani ya Bunge hilo wakidanganywa kuahidiwa kupewa fedha za kuwasomesha
ili waunge mkono msimamo wa kupiga kura ya serikali mbili jambo ambalo
ni kinyume cha malengo ya uwakilishi wao kwa Watanzania.
“Chini ya Umoja wao wa Ukawa wanachofanya ni kutetea maoni ya wananchi
yaliyotolewa kwenye Tume ya Katiba kwa kuwa Tanzania ni nchi ya wote na
hakuna, ambaye akifa atazikwa nje ya nchi hii. Hivyo, ni lazima kutetea
maslahi ya wananchi,” alisema Dk. Slaa.
KAIMU KATIBU MKUU WA CUF ANENA
Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Shaweji Mketo, alisema
Tume ya Maridhiano ya Zanzibar inayoundwa na viongozi kutoka CCM na CUF
ikiongozwa na Nassoro Moyo, imetoa tamko la kumtaka Rais asidhani
Watanzania ni watu wa kuhadaiwa, bali watatetea serikali tatu kwa kuwa
ina lengo la kuimarisha Muungano uliopo.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment