Shule yateketea kwa moto Dar

 

Dar es Salaam. Mabweni ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wazo Hill nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, yameteketea kwa moto na kusababisha hasara ya mamilioni ya shilingi.

Moto huo uliozuka mapema asubuhi, inadaiwa ulisababishwa na hitilafu ya umeme.

Akizungumza jana shuleni hapo, mmiliki wa shule hiyo, Valence Msaki alisema moto huo ulianza saa 11 asubuhi wakati wanafunzi wakiwa kwenye mazoezi ya viungo.

Alisema ulianzia kwenye chumba cha viongozi wa mabweni na licha ya kuwa haukuleta madhara kwa binadamu, lakini umesababisha hasara ya mali mbalimbali za wanafunzi vikiwemo nguo, madaftari, vitanda na magodoro.

Msaki alisema mlinzi aligundua moto huo alipokuwa anakagua mabweni hayo kwani aliona ukitokea kwenye chumba cha viongozi.

Alisema ni asilimia 40 tu ya wanafunzi hao waliokoa baadhi ya vitu vyao na asilimia 60 hawakufanikiwa, hivyo vimeteketea.

“Moto huu ulianzia kwenye chumba wanacholala viongozi wa bweni inawezekana ikawa chanzo ni hitilafu ya umeme kwa kuwa chumba hicho muda wote taa huwa hazizimwi,” alisema Msaki.

Msaki alisema magari ya Kikosi cha Zimamoto yalifika saa 2.30 asubuhi, huku juhudi kubwa za kuuzima moto huo zikifanywa na wananchi, walimu na wanafunzi ambao walitumia maji, mchanga na baadhi ya vifaa vya kuzimia moto vya shule hiyo.

“Sasa hivi tunajipanga ili watoto waweze kulala na kesho tutafanya tathmini ya vitu vilivyoungua ili tujue vitu vingapi vimeungua,” alisema Msaki.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema: “Kizuri ni kwamba hakuna vifo wala mtu aliyejeruhiwa.”

Aliwataka wakuu wa shule mbalimbali katika mkoa huo kufanyia ukaguzi vifaa vya moto na kuziweka shule zao katika hali ya tahadhari ili kusitokee maafa pindi inapotokea ajali za moto.

Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Samueli Nainda alisema kwamba wanaiomba Serikali iwasaidie kutokana na hasara iliyosababishwa na moto huo.

 “Kama hivi vitu vyangu vyote vimeungua kilichobakia ni nguo nilizovaa mwilini sielewi nitafanya nini, huku wazazi wangu wote wameshafariki na wanaonisomesha ni wafadhili ambao wapo Mkoa wa Kigoma,” alisema Nainda

No comments:

Post a Comment