CAG ataka kigogo Tanesco, mkewe washitakiwe

 

Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh amemuweka kitanzini aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), William Mhando, baada ya kushauri ashtakiwe pamoja na mkewe, Clara, kutokana ukiukwaji wa sheria katika kutoa zabuni.

Mbali na Mhando, wengine ambao CAG amependekeza wachukuliwe hatua za kisheria ni Mkurugenzi wa Kampuni ya McDonald Live Line Technology, watu wote walioingia katika biashara na Tanesco kinyume cha sheria pamoja na wafanyakazi waliohusika kutoa zabuni hizo.

Mapendekezo hayo ya CAG, Utouh yamo katika ripoti yake ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma ya 2011/12, aliyoiwasilisha bungeni wiki iliyopita ikirejea ukaguzi maalumu uliofanyika katika shirika hilo kutokana na maombi ya bodi ya wakurugenzi ya shirika hilo.

CAG pia ameweka wazi kuwa Tanesco iligubikwa na ukiukwaji uliokithiri wa Sheria ya Ununuzi ya 2004 na kanuni zake za mwaka 2005, uliosababishwa na viongozi wake wa juu.

“Mkurugenzi Mkuu wa Shirika akiwa ndiye mwenye uamuzi wa kuhusu ununuzi, alishindwa kuzuia ukiukwaji huu wa sheria ya ununuzi na mara nyingi aliidhinisha ununuzi wa chanzo kimoja au usiozidi ushindani,” inasema ripoti hiyo na kuongeza:

“Bodi inatakiwa kuripoti kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DPP) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) yale yote yaliyogunduliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kubaini kuwapo kwa rushwa na ubadhirifu.”

Katika ripoti hiyo, CAG amebainisha ukiukwaji mkubwa wa sheria uliofanywa na Mhando, huku akibainisha kuwa mkewe, ambaye ni Mtendaji wa Mkuu wa Kampuni za Santa Clara Supplies Company Limited, alipewa zabuni katika shirika hilo kwa kutumia taarifa za kughushi.

Pia CAG amebainisha kuwa kampuni hiyo haikuwasilisha katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), rejesho la kodi kiasi cha Sh4.854 milioni ilizolipwa na Tanesco.

Santa Clara

CAG amebainisha kuwa kampuni hiyo iliyosajiliwa Aprili 18, 2011, ilipewa Leseni ya Biashara, Mei 2011 na kwamba wakurugenzi na wanahisa wa kampuni ni mke na watoto wawili wa Mhando.

Mke wa Mhando aliwahi kuwa mfanyakazi wa Tanesco, lakini aliacha kazi baada ya mumewe kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu.

CAG amebainisha kampuni hiyo iliingia mkataba na Tanesco na kupewa zabuni Namba PA/001/11/HQ/G/011 ya ugavi wa vifaa vya ofisi, vifaa vya matumizi ya kompyuta na mashine za kudurusu, kwa mwaka 2011 hadi 2012, mkataba ulianza Desemba 20, 2011.

 

Ripoti hiyo imeeleza kuwa mkataba huo ulisainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, ukishuhudiwa na Mwanasheria wa Shirika la hilo na Mkurugenzi wa Santa Clara aliyeshuhudiwa na shuhuda mmoja.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya CAG, moja ya masharti ya zabuni hiyo yalikuwa ni wazabuni kuwasilisha taarifa za hesabu za karibuni zilizokaguliwa. “Kampuni ya Santa Clara iliwasilisha hesabu zilizokaguliwa kwa mwaka 2010 katika kujaribu kutimiza matakwa ya kupewa zabuni, “ inasema ripoti hiyo.

Pia CAG katika ripoti hiyo, amefafanua kuwa hesabu hizo zilisainiwa na Kampuni ya Ukaguzi ya Fix Capital Certified Public Accountants ambayo usajili wake kwenye Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA) ulikuwa umesitishwa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Januari 24, 2012 Santa Clara ilipewa oda namba 2000009446-1 ya kuuza rimu 2,500 za karatasi kwa bei ya Sh7,000 kila moja. “Jumla ya gharama ya oda nzima ilikuwa ni Sh20.65 milioni ikijumuisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT),” inaeleza ripoti hiyo ya CAG.

Hata hivyo, Santa Clara iliwasilisha rimu 500 tu za karatasi zenye thamani ya Sh4.13 milioni na baadaye ikashindwa na hatimaye zabuni hiyo kutekelezwa na kampuni nyingine.

“Kwa maana hiyo Santa Clara haikustahili kupewa zabuni hiyo na hali hiyo ingejulikana mapema wakati wa tathmini ya zabuni, kwani mali zake zilikuwa ni Sh107.7 milioni,” inaeleza ripoti hiyo.

Mkataba wa McDonald

Mkataba mwingine ambao CAG ameubaini kusainiwa na Mhando, kinyume cha sheria ni ule na Kampuni ya McDonald Live Line Technology Limited, wa zabuni ya kukarabati na kutengezeza njia za umeme (live line), mwaka 2008, 2009, 2010 na 2011.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa mmiliki wa McDonald Live Technology Ltd alikuwa mfanyakazi wa Tanesco, lakini aliachishwa kazi Julai19, 1999 kwa sababu za utoro kazini, kutowajibika na upotevu wa pesa, Sh1.280 milioni na kuharibu gari la Tanesco.

Hata hivyo, ripoti hiyo imebainisha kuwa Julai 17, 2008 McDonald aliingia kwenye makubaliano ya ubia na Mhando, ambaye baadaye aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco katika ubia ambao Mhando alikuwa na jukumu la kutafuta miradi na kazi kutoka kwa wateja na McDonald itawajibika na utekelezaji.

CAG anasema kati ya 2009 na 2011, Mhando baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, aliipa kampuni hiyo mikataba mitano ya zabuni za kukarabati na kutengeneza njia mbalimbali za umeme ambayo iliiwezesha McDonald kulipwa zaidi ya Sh1.12 bilioni.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa mikataba hiyo ilitolewa mingine bila kuwasilisha nyaraka kwa ajili ya ukaguzi kama inavyotakiwa, wala kuwa na dhamana ya Benki Kuu.

 

CAG amebainisha kuwa katika mkataba Na.PA/001/09/HW/W014 wa kukarabati njia ya Kiyungi – Arusha 66kV wa Machi 11, 2010, wenye thamani ya zaidi ya Sh1.417 bilioni haukutekelezwa na McDonald.

Utekelezaji wake ulianza Julai 28, 2010 na ilitakiwa kuwa imemalizika Machi 9, 2011, lakini haukukamilika na hata baada ya kuongezewa muda mara mbili na kutokana na hali hiyo, Juni 19, 2012, Tanesco ilivunja mkataba huo wakati McDonald walikwishalipewa malipo ya awali ya Sh475.6 milioni, sawa na asilimia 33 ya mkataba mzima.

CAG katika ripoti yake anabainisha kuwa malipo hayo yalifanywa kinyume cha masharti ya zabuni ambayo inaelekeza kwamba malipo ya awali yalitakiwa kuwa asilimia 15.

Amebainisha kuwa licha ya Tanesco kufanya tathmini na kubaini kuwa McDonald ilitakiwa kuirejeshea Sh 504.7 milioni ikiwa ni faini, fidia na kiasi cha dhamana ya benki kilichokadiriwa, lakini hadi wakati wa ukaguzi huo pesa hizo zilikuwa hazijarudishwa.

No comments:

Post a Comment