Mwanza. Sakata la vurugu za gesi Mtwara
limeingia sura mpya baada ya waandishi wa habari kuanza kuhojiwa na
polisi wakidaiwa kuhusika na uchochezi uliosababisha vurugu hizo.
Vurugu hizo zilitokea Januari 26, mwaka huu na
kuendelea kwa nyakati tofauti hata kusababisha nyumba za baadhi ya
wabunge, viongozi wa CCM, Mahakama na Halmashauri ya Wilaya ya Masasi
pamoja na magari 18 na pikipiki saba kuteketezwa kwa moto na wananchi
ambao walidaiwa kupinga mpango wa Serikali kusafirisha gesi kutoka
Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mtwara
(MPC), Hassan Simba alithibitisha kuhojiwa kwa waandishi wa habari
kuhusiana na sakata hilo.
Waandishi waliohojiwa hadi jana jioni ni Andrew
Mtuli (Redio Pride FM), anayedaiwa kuendesha kipindi cha Amka na Pride
kinachorushwa na redio hiyo kila alfajiri wakati Emmanuel Msigwa ambaye
ni mtangazaji wa vipindi mbalimbali, Hassad Mdimu mtangazaji wa Kipindi
cha Joto la Wiki ambaye anatuhumiwa kuweka hotuba ya kiongozi mmoja
iliyoitwa ya uchochezi, wote wakiwa ni watangazaji wa kituo hicho cha
redio.
Ilielezwa kuwa mahojiano hayo yanafanywa na
makachero wa polisi kutoka Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam na kwamba
mbali na waandishi wa habari pia imeelezwa watu wa kawaida wamehojiwa
na wengine wanaendelea kuhojiwa kuhusiana na vurugu hizo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Mary Nzuki
hakuweza kupatikana jana katika simu yake kutokana na kudaiwa kuwa
katika pilikapilika za uhamisho kutokana na Inspekta Jejenrali wa Polisi
(IGP) Said Mwema kufanya mabadiliko kwa baadhi ya Makamanda wa Polisi
kwa Mikoa ya Singida na Mtwara.
Wakati huohuo, mwandishi wa habari wa vyombo
mbalimbali Majid Mjengwa ataendelea kuhojiwa na polisi Kituo Kikuu cha
Polisi, Dar es Salaam leo asubuhi.
No comments:
Post a Comment