Wakimbizi wa Burundi nchini TZ warejeshwa makwao
Ramani ya Burundi
Serikali ya Tanzania imeanza rasmi hatua za kuwarejesha makwao raia wa Burundi waliovuliwa hadhi ya ukimbizi.
Ni katika hatua za kuifunga rasmi kambi ya
Mtabila ambayo ni kambi pekee iliyokuwa ikihifadhi wakimbizi wa Burundi
nchini humo wapatao elfu thelathini na saba.
Sanjari na uamuzi wa kuwarejesha
makwao raia hao, shughuli hii inaambatana na kuwachukulia hatua za
kisheria wale wote ambao hawako tayari kurejea Burundi.
Shughuli ya kuwarejesha makwao kwa hiyari raia
wa Burundi waliokuwa wakimbizi hadi mwezi Agosti mwaka huu kabla ya
kuvuliwa hadhi ya ukimbizi na serikali ya Tanzania,ilimalizika rasmi
Jumatatu ambapo kuanzia leo kinachofuata dhidi ya wakimbizi hao ni
kuandikishwa kwa kufuatwa kwenye maeneo wanakoishi kambini na kisha
kupakiwa kwenye magari na kurejeshwa Burundi.
Akizungumza na mwandishi wa BBC mjini Dar es
Salam Eric David Nampesya, mkuu wa kambi hiyo ambaye ni mwakilishi wa
wizara ya Mambo ya ndani nchini humo, Bwana Frederick Nisajile, alisema
utaratibu huo utakavyokuwa baada ya kukamilika kwa shughuli ya kurejea
kwa hiyari ya 'Kimombo Voluntary repatriarition.'
Bwana Nisajile alisema inatarajiwa kuwa raia wa
Burundi wapatao elfu moja watarejeshwa makwao kila siku katika utaratibu
huu ambao pia utawahusisha maafisa wa idara ya Uhamiaji ili kuwakamata
wale wote watakaokaidi kurejea makwao.
Naye Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa
linalohudumia Wakimbizi UNHCR Bi Chansa Kapaya anasema hakuna uwezekano
kwa Raia hao wa Burundi kutafutiwa nchi ya tatu kwa sababu wao si
wakimbizi tena kwa wakati huu.
Nafasi hiyo haipo tena,nafasi kama hiyo hutolewa
kwa wakimbizi,hawa walipokuwa wakimbizi zamani na kwa sasa
walishavuliwa hadhi ya kuwa wakimbizi,kwa maana hiyo hawawezi kupewa
nafasi ya kutafutiwa hifadhi katika nchi ya tatu,kwa maana hiyo
suluhisho pekee kwao ni kurejea Burundi.
Kuanza kufungwa kwa Kambi hiyo ya Mtabila
kunahitimisha miaka 19 tangu ilipofunguliwa mnamo mwaka 1993,wakati huo
ilipoanza kupokea raia wa Burundi waliokimbia machafuko ya kivita
yaliyofuatia mauaji ya aliyekuwa rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia
nchini Burundi hayati Melchior Ndadaye.
No comments:
Post a Comment