Sekondari ya William Lukuvi wanafunzi walala darasani

Mmoja wa wanafunzi akiwa juu ya godoro hivi karibuni. Picha na Said Ng’amilo 


Wiki iliyopita nilikwenda Morogoro ambako pamoja na mambo mengine nilikuwa na kipindi kwenye televisheni moja mkoani humo, kilicholenga kutoa ushauri kwa jamii kuhusu namna ya kupambana na changamoto za maisha. Baadaye nilikutana na watu waliokuja kwenye hoteli niliyokuwepo kwa lengo la kubadilishana mawazo zaidi kuhusiana na yale ambayo niliyaeleza kwenye televisheni. Mmoja wa watu alikuwa ni Erick Mtengele, kijana wa Kimasai ambaye amekuwa akihangaika huku na kule kutafuta namna ya kuwasaidia wafugaji nchini.

 “Mimi ni kati ya Wamasai wachache nchini walio na elimu ya chuo kikuu, nimehitimu elimu ya maendeleo ya jamii katika Chuo Kikuu cha Tumaini mwaka 2010, kwa bahati mbaya hadi leo sina ajira,” anasema Mtengele ambaye ni mzaliwa wa Kijiji cha Luganga, Kata ya Ilala Mpya, mkoani Iringa.

Tulizungumza mengi, yakiwemo matatizo ya sekta ya elimu nchini na harakati zake za kuwasaidia wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya William Lukuvi wapate angalau bweni, akisema kuwa ameandika barua maeneo kadhaa kuomba shule hiyo ijengewe bweni bila mafanikio.

“Shule haina mabweni, wanafunzi wanalala kwenye madarasa,” anasema Mtengele.

Baada ya mazungumzo hayo nililazimika kufuatilia ili kujua ukweli, nilibaini kuwa ni ukweli thabiti kwamba wapo wanafunzi wanalala kwenye madarasa katika shule hiyo, sababu kubwa ni kwamba shule haina uwezo wa kifedha wa kujenga mabweni.

“Huogopi kufuatilia shule hii?” anaonya mwandishi mmoja wa habari anayefanyia kazi mkoani Iringa kwa maelezo kuwa kufuatilia shule hiyo kunaweza kuzusha kutokuelewana na baadhi ya watu ambao kwa namna moja ama nyingine wanahusika na shule hiyo.

Mwandishi huyo anaonya kuwa hofu ya kufanyiwa mabaya ndiyo sababu waandishi walio wengi wanaogopa kuandika ukweli kuhusiana na shule hiyo kwamba baadhi ya wanafunzi wanalala katika madarasa tofauti katika shule hiyo.

“Kuna  waandishi waliwahi kufuatilia suala hili na kuhoji kwa nini mabweni hayajengwi, matokeo yake siyo tu kwamba hawakupewa ushirikiano na wale ambao wanahusika kutolea maelezo jambo hilo, bali walionekana kama wanaingilia mambo yasiyowahusu, wengine hata wakajikuta katika hofu kuhusu maisha yao,” alionya mwandishi huyo.

Hata hivyo niliendelea kufuatilia kutokana na ukweli kwamba lengo la makala hii siyo kudhalilisha yeyote, bali kueleza ukweli ili kuangalia namna gani wanafunzi wanaweza kusaidiwa kwa kujengewa mabweni.

Kama yupo mwenye nguvu za kusumbua wale ambao wanaeleza ukweli kuhusiana na hali mbaya ya maisha ya wanafunzi kwa kukosa mabweni, nguvu hizo azielekeze kuhakikisha mabweni yanajengwa, tena ikiwezekana haraka.

Nguvu zake zitakuwa za maana zaidi ikiwa atafikiria namna ya kusaidia kupatikana kwa mabweni kuliko kukasirika kwa sababu ya kuandikwa ukweli kwamba Shule ya Sekondari William Lukuvi haina mabweni kiasi kwamba wanafunzi wanalazimika kulala darasani.

Katika kufuatilia ilibainika kuwa ni kweli kuna ugumu wa kupata ushirikiano, na pia hata baadhi ya waandishi wa habari wana hofu, kwa mfano kuna mwandishi alifanikiwa kupiga picha miezi kadhaa iliyopita wanafunzi wakiwa darasani wamelala, hakuweza kuzitumia, huku ulinzi ukiwekwa kuhakikisha hakuna mwandishi anayefanikiwa kufahamu hali hiyo ya watoto kulala darasani.

 Changamoto

Japokuwa kuna changamoto kadhaa, lakini kutokuwa na mabweni inaonekana ni changamoto kubwa katika Shule ya Sekondari ya William Lukuvi iliyopo Jimbo la Isimani, wilaya ya Iringa.Shule hiyo ipo takribani kilomita 50 kutoka Manispaa ya Iringa.

Shule hiyo imepewa jina hilo kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Isimani, na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi, anayepongezwa kwa harakati mbalimbali za kuleta maendeleo katika jimbo hilo.

Shule hiyo imejengwa na wananchi wa Kata ya Ilolompya ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa shule ya sekondari katika kila kata ili kuhakikisha watoto wanaomaliza elimu ya msingi wanapata fursa ya kuendelea na elimu ya sekondari.

Sekondari ya William Lukuvi imejengwa na wananchi wa Kata ya Ilolompya kwa lengo la kuwahudumia wananchi wa vijiji vinne vya Magozi, Ilolo, Luganga na Mkombilenga; shule iko mbali na baadhi ya vijiji kiasi kwamba inalazimika baadhi ya wanafunzi kubaki shuleni kutokana na kushindwa kurudi nyumbani kwao kutokana na umbali na pia usalama kwani baadhi ya maeneo wanayopita ni mapori yanaonekana kutokuwa salama hasa nyakati za usiku.

Shule ina zaidi ya wanafunzi 251 wakiwemo wavulana 145 na wasichana 106 ambapo kidato cha kwanza kuna wanafunzi 100 wavulana 52 na wasichana 49, kidato cha pili 74 wavulana 49 na wasichana 25.

Kidato cha tatu 39 wanafunzi wakiwemo wavulana 26 na wasichana 13, kidato cha nne ni 36 ambapo wavulana 22 na wasichana 14. Tatizo la bweni ni kubwa hali inayosababisha wanafunzi wavulana kutumia chumba cha darasa kwa ajili ya matumizi ya kulala wakati wasichana wakitumia jengo ambalo linatumika kwa muda mfupi wakisubiri kukamilika kwa bweni lao.

Wengi wa wanafunzi wanatoka umbali wa kati ya kilomita moja hadi nne kufika shule na kuwa kwa wale wanaotoka umbali wa kilomita nne, maana yake ni kuwa wanatembea kilomita nane kwenda shule na kurudi nyumbani.

Umbali huo wa zaidi ya kilomita nane yaani kwenda na kurudi, umekuwa ukilalamikiwa na baadhi ya wanafunzi kuwa unawasababishia wengi wao kuchoka, hivyo kusababisha kurudisha nyuma maendeleo yao kimasomo.

Usikose mfululizo wa makala hii kesho kujua kinachoendelea, pamoja na kauli za uongozi wa shule.

No comments:

Post a Comment