Watoto wengi walikufa kutokana na utapia mlo
Takriban watu 260,000 walifariki dunia wakati wa ukame ulioikumba Somalia kuanzia mwaka 2010 hadi 2012, utafiti umebaini.
Nusu ya waliofariki dunia walikuwa ni watoto
wenye umri chini ya miaka mitano, inaeleza ripoti ya shirika la Umoja wa
Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO, pamoja Mtandao wa Kuonya Mapema
Kuhusu Majanga ya Ukame unaofadhiliwa na Marekani.
Idadi ya vifo ilikuwa kubwa kuliko ile iliyokadiriwa ya watu 220,000 waliofariki wakati wa ukame wa mwaka 1992.
Janga hilo lilisababishwa na ukame mkali, uliochochewa na mapigano kati ya makundi hasimu yaliyokuwa yakigombea madaraka.
Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza ulitangaza
hali ya ukame Julai 2011 katika mikoa ya Somalia ya Bakool uliopo kusini
na ule wa chini wa Shabelle, ambayo ilikuwa inadhibitiwa na kundi la
wanamgambo wa Al – Shabab wenye mafungamano na Al – Qaeda.
Lakini kundi hilo lilikanusha kuwepo kwa hali
hiyo na kuyapiga marufuku mashirika kadhaa ya misaada ya nchi za
magharibi kufanya shughuli zake katika maeneo hayo.
Baadaye ukame ulisambaa katika maeneo mengine
ukiwemo mkoa wa kati wa Shabelle na Afgoye na katika kambi za watu
wasiokuwa na makaazi katika maeneo yaliyokuwa yakidibitiwa na serikali
katika mji mkuu Mogadishu.
Mchumi Mwandamizi wa shirika la FAO, Mark
Smulders amesema, ukweli kuhusu ukubwa wa janga hilo la kibinadamu
umeibuka kwenye utafiti uliofanywa kwa kushirikiana na Mtandao wa Kuonya
Mapema Majanga ya Ukame, Fews Net.
“Kwa kawaida, kukadiria vifo wakati wa dharura
ni sayansi isiyo rasmi, lakini kutokana na ubora na kiwango cha takwimu
zilizokuwepo, tuna uhakika na utafiti huo”, amesema ofisa wa Fews Net
Chris Hillbruner.
“Utafiti huo unaeleza kuwa, kilichotokea Somalia
ni moja ya majanga mabaya kabisa ya ukame kuwahi kushuhudiwa katika
kipindi cha miaka 25 iliyopita, “ ameongeza.
Inakadiriwa kuwa 4.6% ya jumla ya idadi ya watu
na 10% ya watoto chini ya umri wa miaka mitano walifariki dunia huko
maeneo ya kusini na kati mwa Somalia, imeeleza ripoti hiyo.
“Ripoti hiyo imethibitisha kuwa hatua za ziada
zingechukuliwa kabla ya ukame huo haujatangazwa, amesema Phillippe
Lazzarini, Mratibu wa Shughuli za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini
Somalia.
Somalia ilikumbwa na ukame mkali mwaka 2011, ulioathiri zaidi ya watu milioni 13 katika eneo lote la Pembe ya Afrika.
Maelfu ya watu walikimbia makaazi yao wakisaka chakula. Umoja wa mataifa ulitangaza ukame huo kumalizika Februari 2012.
Kwa zaidi ya miaka 20 ya vita vya weyewe kwa
wenyewe, Somalia imeshuhudia wababe wa kivita wa koo, wanasiasa mahasimu
na vikundi vya wanamgambo vikigombea madaraka, hali iliyoruhusu
kushamiri kwa ukosefu wa utawala wa sheria.
Septemba mwaka jana, serikali inayoungwa mkono
na Umoja wa Mataifa iliingia madarakani baada ya miaka nane ya utawala
wa mpito, hatua iliyoleta utengamano katika baadhi ya maeneo.
No comments:
Post a Comment