Jeshi la Polisi, jana liliuzuia msafara wa
mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa kwenda Usangi,
wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro kushiriki mazishi ya kada wa CCM,
Peter Kisumo, likitaka kupunguzwa kwa idadi ya watu.
Mbali
na kuzuia msafara huo, chombo hicho cha Dola kimepiga marufuku shughuli
za kutafuta udhamini kwa wagombea urais wa vyama vya siasa kuambatana
na misafara.
Lowassa, ambaye aliwasili Kilimanjaro jana
asubuhi kabla ya kuanza safari ya kwenda Mwanga, alijikuta akikumbana
na kizuizi cha polisi walioziba barabara kwa magari yao eneo la Kijiji
cha Mroro, mita chache kutoka Mji wa Mwanga, wakati akielekea na msafara
wake katika Tarafa ya Usangi kuhudhuria mazishi ya mwanasiasa huyo
mkongwe aliyefariki wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.
Lowassa
hakukubaliana na agizo la polisi la kumruhusu aendelee na safari na
kuwaacha wafuasi wake kwenye msafara huo, ambao awali walitakiwa
wasibebe bendera, lakini baadaye wakazuiwa.
Kisumo alizikwa jana katika mazishi yaliyohudhuriwa na maelfu ya waombolezaji, wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
“Kwa
kuwa tumezuiwa na polisi, kitendo hiki kimeondoa mwafaka wa kitaifa
kwamba mpinzani hawezi kumzika mtu wa CCM na wa CCM hawezi kumzika
mpinzani.... mpasuko huu ni mkubwa. Wameyataka wao,” alisema Mwenyekiti
wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia baada ya polisi kuwazuia.
“Kwa kuwa wametuzuia kwenda kumzika Mzee Kisumo, sisi tunarudi lakini Watanzania wapewe taarifa kuwa CCM inalipasua Taifa.”
Alipoulizwa
sababu za polisi kuwazuia, Mbatia alisema: “Wanahofia Mheshimiwa
Lowassa na msafara wake. Magari mangapi? Magari 10 tu ya Mheshimiwa
Lowassa! Magari gani hayo?”
Ilivyokuwa
Msafara
huo ulikuwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani ambao ni
pamoja na Mbunge wa Moshi Mjini, Phillemon Ndesamburo, Joseph Selasini
(Rombo), Mbatia na na Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mremaambaye pia ni
Mbunge wa Vunjo pamoja na viongozi wa Chadema ngazi ya mkoa na wilaya.
Msafara
huo ulipofika Mroro, ulikutana na kizuizi cha polisi pamoja na askari
wa kuzuia ghasia waliowataka watoe bendera na kuachana na msafara huo.
Kutokana
na kauli hiyo, Mbatia, ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) aliwataka madereva wa bodaboda kutoa bendera
zao na kutoongozana na msafara, agizo ambalo walilitii na kuondoka
lakini polisi walikataa magari kuvuka kizuizi hicho.
Baadaye,
Mbatia alizungumza kwa simu na Inspekta Jenerali wa Polisi, Ernest
Mangu kabla ya kumpelekea simu Lowassa ambaye naye alizungumza naye na
kusema wameruhusiwa, lakini askari waliokuwa wameweka doria walikataa
kuwaruhusu.
Kutokana na hali hiyo, Mbatia baadaye
alizungumza kwa simu na kudai anawasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa
wa Kilimanjaro, Fulgence Mponji lakini askari waliokuwapo walidai kuwa
wamepewa maagizo kuzuia msafara huo.
Msafara huo ulikaa
eneo hilo zaidi ya saa mbili na baadaye polisi waliruhusu gari ya
Lowassa, Mbatia na Ndesamburo kupita, lakini watu waliokuwa kwenye
msafara wabaki kitendo ambacho viongozi hao walikipinga na kuamua kurudi
Moshi.
“Tumeongea na IGP, RPC lakini tunaambiwa OCD
amekataa, tunataka Watanzania wajue kuwa CCM wameanza kupasua amani ya
Taifa hili,” alisema Mbatia.
Baada ya kukubaliana,
Mbatia aliwataka wananchi waliokuwa wanakwenda kwenye msiba kwa msafara
wao kuingia kwenye magari na kuanza safari ya kurejea Moshi na baada ya
kufika Njia Panda Himo, walikutana na wananchi wengi waliokuwa wakitaka
kumuona Lowassa na kufunga barabara.
Polisi
walilazimika kutumia bomu la machozi kuwatawanya, lakini wengi waligoma
kuondoka na Lowassa alilazimika kusimama kwenye gari na kuwapungia ndipo
walipokubali kusogea pembeni kupisha msafara uendelee na safari.
Alipoulizwa
kuhusu suala hilo, Kamanda Mponji alikiri jeshi lake kuzuia msafara
huo, akisema kazi yake ni kuhakikisha Rais anamaliza safari yake
Kilimanjaro kwa amani.
Mazishi ya mwanasiasa huyo
mkongwe yalitarajiwa kumkutanisha Lowassa na Rais Kikwete, marafiki
wawili wa muda mrefu ambao katika siku za karibuni wanaonekana
kutofautiana baada ya jina la waziri huyo mkuu wa zamani kuenguliwa
kwenye mchakato wa urais kwa tiketi ya CCM mapema Julai.
Lowassa,
ambaye amepitishwa na Chadema kugombea urais na ambaye ataungwa mkono
na vyama vinne vya NCCR-Mageuzi, NLD, Chadema na CUF, anatarajiwa kuanza
kusaka wadhamini leo mkoani Mbeya na baadaye ataelekea Mwanza.
Maandamano yazuiwa Mbeya
Lakini
wakati akianza ziara hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed
Msangi amesema katika taarifa yake kwamba wamekubaliana na viongozi wa
Chadema kwamba hakutakuwa na maandamano, bali utakuwapo msafara wa
kawaida bila kuathiri shughuli za wakazi.
Msangi alisema sababu kubwa ya kuafikiana hivyo ni za kiusalama kutokana na ukweli kwamba barabara inayotumika ni moja.
Misafara kwenda NEC marufuku
Katika
hatua nyingine, Jeshi la Polisi limepiga marufuku maandamano ya aina
yoyote ya vyama vya siasa wakati wa kwenda kuchukua fomu, kuzirudisha na
kutafuta wadhamini mikoani.
Hatua hiyo ya polisi
imekuja ikiwa ni siku kadhaa baada ya wafuasi wa vyama viwili vikubwa;
CCM na Chadema kujitokeza kwa wingi kuwasindikiza wagombea wao kwenda
kuchukua NEC na kusababisha msongamano katikati ya jiji.
Naibu
Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki alisema kutokana na
malalamiko mengi kutoka kwa wananchi walioshindwa kufika kwa wakati
katika shughuli nyingine za kijamii, wameamua kusitisha utaratibu huo.
Alisema
misafara hiyo ilisababisha usumbufu na malalamiko mengi kutokana na
wananchi kutopata huduma kwa wakati, wagonjwa kushindwa kufika
hospitalini kwa wakati, kuchelewa ofisini na watu kushindwa kupata
huduma za kijamii kutokana na maduka kufungwa.
Alieleza
kuwa hali hiyo ilijitokeza siku walipochukua fomu wagombea urais wa CCM
na Chadema, hivyo kwa sababu za kiusalama, polisi imesitisha maandamano
ya aina yoyote.
Kaniki alisema unaandaliwa utaratibu
maalumu wa kuwakutanisha wadau wote wa siasa ili kuona namna bora ya
kuhakikisha mchakato mzima wa uchaguzi unafanyika katika hali ya amani
na utulivu.
Viongozi wa vyama walonga
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya viongozi wa vyama ambavyo wagombea
wake wameshachukua fomu, walipinga hatua hiyo ya polisi, wakisema ni
sawa na kuwanyima wananchi haki ya msingi inayokubalika kikatiba.
Katibu
Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema polisi ilipaswa kuchukua
hatua mara baada ya CCM kufanya maandamano yao, lakini si kutoa tamko
hilo baada ya Chadema.
Alikanusha kuwapo kwa sababu za
kiusalama, akieleza kuwa kazi ya polisi ni kulinda usalama na hivyo
wanaweza kupanga maandamano yaanzie wapi na kuishia wapi ili kupunguza
vurugu.
Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa alisema
jeshi hilo lilijichanganya kwa kutoa taarifa awali kuwa linaruhusu
maandamano hayo, lakini akasema kama limejiridhisha kuwa kwa kufanya
hivyo linalinda usalama wa raia, haoni kama kuna tatizo.
“Wapo
sahihi kabisa kuzuia, kwani kuna madai kuwa baadhi ya vijana walifanya
vurugu, walilewa. Kuna dalili za kuhatarisha usalama kwa mwenendo huo, ”
alisema.
Mgombea wa urais kupitia TLP, Maxmillian
Lyimo alisema polisi wanapotoa kauli wawe makini wasije kuonekana
wanapendelea upande fulani kwani wakati wa CCM walikaa kimya, lakini
baada ya Chadema ndipo wametoa tamko. Alisema wao ndiyo wenye jukumu la
kulinda usalama wa raia na mali zao, hivyo wanapaswa kuhakikisha
mikusanyiko hiyo inalindwa.
Katibu Mkuu wa CCK, Renatus
Muabhi alisema watu wanatumia vibaya uhuru waliopewa, lakini akataka
ieleze sababu ya kuzuia na kama ni usalama, ni wajibu wa polisi.
Mgombea
urais kwa tiketi ya Chaumma, Hashim Rungwe alisema hakuna haja ya
kuwepo kwa maandamano wakati kuna kampeni ambazo wafuasi na wanachama
watahudhuria hadi wachoke.
Kauli ya Kova
Mapema
jana, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ilisema haitatumia mabomu
na nguvu wakati wa uchaguzi na badala yake itashirikiana na viongozi wa
vyama vya siasa ili kudumisha amani na utulivu.
Kamanda
wa kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova alisema polisi imejipanga
kikamilifu kudhibiti vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani katika
kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu.
No comments:
Post a Comment