Upinzani, Tume watofautiana uandikishaji Zanzibar


Zanzibar. Wakati Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), ikitangaza siku mbili kwa kila kituo kuanza uandikishaji wa wapiga kura wapya baada ya Kura ya Maoni, vyama vya siasa vimedai muda huo hautoshi kulinganisha na mahitaji makubwa ya wananchi kujiandikisha kupiga kura.

Mkuu wa Divisheni wa Zec, Idrisa Haji Jecha alisema mjini Unguja juzi kuwa kila kituo kimepangiwa kutumia muda huo kuandikisha wapiga kura, hasa wale waliofikia miaka 18 na ambao hawakupata nafasi kwa sababu mbalimbali.

Jecha alisema matayarisho ya kazi hiyo yamekamilika, ikiwa ni pamoja na Zec kuagiza vifaa vya kisasa kufanikisha kazi hiyo.

“Kila kituo kitaandikisha wapiga kura wapya kwa siku mbili, tunategemea kila kitu kitakwenda kama kilivyopangwa na uchaguzi utakuwa wa kisayansi,” alisema Jecha.

Alisema ratiba ya Uchaguzi Mkuu imekamilika na kwamba utafanyika Oktoba 25, uteuzi wa wagombea nafasi za urais, ubunge, uwakilishi na udiwani utakuwa Agosti 17 na kampeni zitaanza Septemba 7 hadi Oktoba 24.

Kiasi cha Sh7.1 bilioni zitatumika kufanikisha uchaguzi Zanzibar, mbali na michango ya mashirika ya maendeleo ya kimataifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa Chama cha Wananchi (CUF), Omar Ali Shehe alisema muda uliowekwa na Zec hautoshi na ameshauri tume kuuongeza.

“Kuna idadi kubwa ya watu hadi sasa hawajapewa vyeti vya kuzaliwa na wengine hawana vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, nadhani muda hautatosha,” alisema Shehe.

Alisema kimsingi, idadi ya wapiga kura wapya ni wengi Unguja na Pemba, hivyo kuna kila dalili wapiga kura wapya watakosa fursa hiyo.

“Tungependa kuona wananchi wanapata muda wa kutosha kujiandikisha kutokana na hamasa kubwa waliyonayo kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka huu,” alisema Shehe.

Katibu Mkuu wa Tadea, Juma Ali Khatib alisema ili kuondoa malalamiko na mivutano, kuna haja kwa Zec kuongeza muda wa uandikishaji.

Khatib alisema kutokana na mwamko uliopo sasa, siku zilizotangazwa ni chache na wengi wanaweza kubaki bila kuandikishwa kama muda hautaongezwa.

Kuhusiana na suala la baadhi ya watu kukosa vyeti vya kuzaliwa au vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, alisema linaweza kuleta migongano.

“Kwanza muda uliotolewa na Zec hautoshi, lakini pia unawanyima wananchi wengi kupata fursa ya kujiandikisha. Ni vizuri suala la vitambulisho likamalizwa kwanza, ndipo kazi ya uandikishaji wapiga kura ifanyike,” alisema Khatib.

No comments:

Post a Comment