Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima (katikati)
akimsikiliza wakili wake, John Mallya (kulia) walipokuwa wakielekea
Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam jana alikoitwa kwa
mahojiano. Kushoto ni Mchungaji Msaidizi wa kanisa hilo, Yekonia
Bihagaza. Picha na Venance Nestory
Dar es Salaam. Wakati Askofu
wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima akijisalimisha kwa Jeshi
la Polisi, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda amemtaka aripoti
ofisini kwake keshokutwa kutoa maelezo kuhusiana na tuhuma za kumkashifu
kiongozi mwenzake wa dini.
Juzi, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
ilitoa amri kwa askofu huyo kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi Dar es
Salaam kutoa maelezo kuhusu tuhuma za kashfa na matusi dhidi ya Askofu
Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali
Pengo.
Askofu Gwajima alitii amri hiyo na jana alifika kituoni hapo saa 8.15 mchana kwa ajili ya kutoa maelezo.
Akizungumza muda mfupi kabla ya kwenda kutoa
maelezo, Askofu Gwajima alisema Baraza la Maaskofu Tanzania,
lilikubaliana kupinga Mahakama ya Kadhi lakini Askofu Pengo akawageuka..
“Tulikubaliana kwa pamoja kwamba hatutaki na
viongozi wote tulisaini makubaliano hayo akiwamo Kardinali Pengo lakini
tunashangaa alitugeuka,” alisema na kuongeza:
“Mimi kama kiongozi wa kiroho nilimkemea kiongozi mwenzangu wa kiroho.”
Alisema katika maneno aliyotoa hakuna neno lolote
ambalo ni la kashfa...“yale yote ambayo nimeongea ni maneno kutoka
kwenye Biblia. Kwa hiyo leo (jana) nimeshangaa kuitwa na polisi.
Nilitarajia kama kuitwa angeitwa yeye (Kardinali Pengo),” alisema Askofu
Gwajima na kuongeza kuwa, aliitikia wito huo ili kufahamu ni kwa nini
ameitwa. Mapema wiki hii, mitandao mbalimbali ya kijamii, ilisambaza
sauti ya Askofu Gwajima akitoa maneno makali ya kumkashifu Kardinali
Pengo.
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova alisema: “Taratibu za mahojiano zimeanza kwa mujibu wa
sheria na mtuhumiwa atapewa haki zote anazostahili kama vile kuwa na
ndugu na rafiki yake wa karibu anayemwamini au wakili wake.”
Akizungumzia kuhusiana na tuhuma zinazomkabili
Askofu Gwajima, Kova alisema ni pamoja na kumkashifu na kumtukana
hadharani Kardinali Pengo.
Kuitwa kwa DC Kinondoni
Katika hatua nyingine, Makonda amemwandikia barua
Askofu Gwajima akimtaka kufikia ofisini kwake kutoa ufafanuzi juu ya
maneno makali dhidi ya kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki.
Katika barua yake, Makonda alisema ofisi yake
inataka kufahamu kama uhuru wa kuabudu kikatiba ni kutokuheshimu watu
wengine. “Hatuamini kama imefika wakati kwenye nyumba za ibada kumegeuka
sehemu ya kutukana na kuwasema watu badala ya kuhubiri habari njema.
Tunataka kujidhihirisha malengo hasa ya kutumia maneno hayo ni nini.”
No comments:
Post a Comment