Hussein Ramadhani ‘Sharo Milionea’ (27)
MMILIKI wa gari ambalo lilikuwa likiendeshwa na
msanii maarufu nchini, Hussein Ramadhan ‘Sharo Milionea’ na kupata nalo
ajali iliyosababisha kifo chake huko Muheza, Tanga, Mohammed Ismaili
maarufu kwa jina la Mudi Suma, ameibuka na kueleza uhusiano wake na
marehemu, huku akisema amekubali hasara.
Akizungumza kwa simu kutoka Muheza jana Suma
alisema hana mpango wa kudai fidia au kupeleka malalamiko yoyote kwa
ndugu wa marehemu kwa kuwa; “Kilichotokea ni kazi ya Mungu.” “Siwezi
kudai hata kidogo hivyo ni vitu vya kupita tu. Marehemu alikuwa ni zaidi
ya ndugu yangu, gari ni kitu kidogo sana katika uhusiano tuliokuwa
nao,” alisema Suma na kuongeza kwamba hata Marehemu Sharo Milionea naye
alikuwa amemwachia mali zake kadhaa ikiwamo gari.
“Siyo gari tu alilokuwa ameniachia. Kuna
mikataba yake ya kazi, Bajaji yake na funguo za chumbani kwake. Nasubiri
kukabidhi vitu hivyo baada ya kukaa na ndugu zake. Vitu viko kwenye
mikono salama,” alisema.
Kuhusu gari lake lililopata ajali, Suma
alisema lilikuwa na bima ndogo, lakini anapanga kwenda TRA atakaporejea
Dar es Salaam kufuatilia baadhi ya mambo.
“Kabla ya kuondoka bima ile
kubwa ilikuwa imekwisha kwa hiyo nikaamua kuikatia bima ndogo.
Nitakapofika kesho (leo) Dar es Salaam, nategemea kwenda ofisi za bima
kuzungumza nao,” alisema Suma.
Alipoulizwa kama kuna mtu mwingine
atakayeathirika kutokana na gari hilo kuharibika katika ajali mbali na
yeye, alijibu: “Hakuna tofauti na mimi mwenyewe na familia yangu.”
Kabla ya ajali
Suma alieleza kuwa kabla ya
kuanza safiri yake, Sharo Milionea alifika nyumbani kwake mchana na
kumweleza kuwa afya yake haikuwa nzuri.
“Kabla ya kuondoka aliniambia kuwa hajielewi
elewi na kifua kilikuwa kinambana. Nikamshauri asiondoke peke yake,
atafute mtu wa kuondoka naye ambaye atamsaidia kuendesha gari njiani,”
alisema Suma na kuongeza:
“Tulianza kuwapigia simu jamaa zetu wanne wa
kusafiri naye lakini kila tuliyemwambia hakuwa tayari. Ilikuwa ni
changamoto mpaka ilipofika saa 10:45 hivi jioni, akaamua kuondoka peke
yake. Wakati anatoa gari getini kwangu, nikamwambia, basi jaribu kuwa
mwangalifu sana, maana alikuwa kweli anasumbuliwa na kifua.
Tukakubaliana kwamba atakaporudi aende hospitali kucheki afya yake.”
Kuhusu uhusiano wake na marehemu, Suma
alisema: “Mimi ni mfanyabiashara na yeye alikuwa msanii, lakini ilitokea
tukawa marafiki sana mpaka ikafikia wakati nikaona kuwa ni ndugu yangu.
Nilimwamini nikamtambua kama sehemu ya familia.”
Alisema marehemu alikuwa akitumia gari hilo
kila alipolihitaji na safari ya kwenda nalo Tanga kwa wazazi wake
ilikuwa ni ya tatu.“Siyo mara ya kwanza kuitumia gari lile, nilikuwa
nimemwamini sana. Safari ya kwanza alichukua na kusafiri nalo mwenyewe,
halafu safari ya pili ikafuata na hii ilikuwa safari ya tatu,” alisema
Suma.
Eneo la ajali wakimbia makazi
Baadhi ya
wakazi wa Kijiji cha Songa Kibaoni mahala ambako Sharo Milionea alipatia
ajali, wamezikimbia nyumba zao baada ya Mkuu wa Wilaya ya Muheza,
Subira Mgalu kutoa siku moja kwa waliopora mali za marehemu huyo
kuzisalimisha mara moja.
Mgalu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Ulinzi na Usalama Wilaya ya Muheza alisema jana kwamba usiku wa kuamkia
jana, baadhi ya nyumba kijijini hapo zilikuwa tupu baada ya wakazi wake
kuzikimbia.
No comments:
Post a Comment