Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda
Akitoa ushahidi wake jana huku akiongozwa na Wakili
Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka, Lolila ambaye ni shahidi wa
kwanza wa upande wa mashtaka alidai kuwa eneo hilo awali lilikuwa
likimilikiwa kihalali na Bakwata.
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata),
limemkana Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh
Ponda Issa Ponda na wenzake, baada ya kudai mahakamani kuwa eneo
walilovamia wakidai ni mali ya Waislamu linamilikiwa kihalali na kampuni
ya Agritanza.
Katibu Mkuu wa Bakwata, Sheikh Suleiman Lolila
alisema hayo jana wakati akitoa ushahidi katika kesi ya jinai
inayomkabili Ponda na wenzake 49 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
wakidaiwa pamoja na mambo mengine kuvamia na kupora ardhi na wizi wa
vifaa vya ujenzi.
Akitoa ushahidi wake jana huku akiongozwa na
Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka, Lolila ambaye ni shahidi
wa kwanza wa upande wa mashtaka alidai kuwa eneo hilo awali lilikuwa
likimilikiwa kihalali na Bakwata.
Hata hivyo, alidai kuwa baadaye Bakwata
walibadilishana na Kampuni ya Agritanza Limited baada ya kuona eneo
lililobaki halifai kujengwa chuo kikuu kutokana na ufinyu wake.
Alidai
kuwa awali eneo hilo lilikuwa kubwa lakini miaka ya 2000 lilianza
kumegwa na kuzigawia baadhi ya taasisi na wafanyabiashara na kwamba tume
iliundwa na kubaini kwamba hayo yalifanyika kinyume na utaratibu.
“Baada ya kumegwa eneo lililobakia ni finyu
ambalo halitoshi kujengwa chuo kikuu. Mimi nilikuwapo wakati Baraza la
Wadhamini wa Bakwata wakijadili jinsi ya kupata eneo kubwa na kuijadili
Kampuni ya Agritanza iliyokuwa na eneo la ekari 40 Kisarawe ili
tubadilishane,” alidai.
Shahidi huyo aliongeza kuwa Agritanza
ilikubali kubadilishana maeneo na kwamba wao walichukua ekari nne
zilizopo Markaz (Chang’ombe) na Bakwata ikachukua ekari 40 zilizopo
Kisarawe.
“Hayo yalifanyika baada ya kupata baraka
kutoka katika Baraza la Maulamaa lililokaa na kuamua hivyo Januari 22,
2011,” alisema shahidi huyo na kuongeza:
“Baada ya kufanyika
mabadilishano, Agritanza walianza kushughulikia usajili wa kiwanja namba
311/3/4 na walipata. Hivyo kwa sasa ni wamiliki halali, tulishamalizana
nao.”
Shahidi huyo aliendelea kudai kuwa eneo hilo
Serikali ililitoa kwa Wamisri kwa ajili ya kujenga chuo chini ya
usimamizi wa Bakwata.
Alidai kuwa kwa mujibu wa mkataba huo
uliosainiwa mwaka 2003, endapo Wamisri wataondoka Tanzania watarejesha
eneo hilo katika umiliki wa Bakwata.
Shahidi huyo pia alitoa kielelezo cha makubaliano ya Baraza la Wadhamini wa Bakwata na Agritanza, kuhusu kubadilishana uwanja.
Hata hivyo, Wakili wa utetezi, Juma Nassoro
alipinga kwa madai kwamba kisheria walitakiwa kutoa notisi kabla ya
kuwasilisha kielelezo hicho mahakamani.
Akijibu hoja hizo, Wakili Kweka alidai kuwa
barua halisi wanayo na kwamba ipo katika kumbukumbu za Bakwata, huku
akisisitiza kuwa shahidi anastahili kutoa kielelezo hicho kwa sababu
saini yake ipo.
Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa anayesikiliza
kesi hiyo, alikikataa kielelezo hicho akisema Serikali ilitakiwa kutoa
notisi kabla ya kuwasilisha kielelezo hicho.
Hakimu Nongwa alisema kwa kuwa barua halisi
ipo wanatakiwa kuiwasilisha mahakamani, lakini akasema endapo barua
halisi haipo, basi taarifa ya jana itatambulika kuwa notisi na
wataruhusiwa kuiwasilisha.
No comments:
Post a Comment