Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Ernest Mangu,
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, lakini alisema jitihada za
wafanyakazi wa meli hiyo pamoja na kikosi cha Zimamoto zilifanikisha
kuudhibiti moto huo kabla haujasababisha madhara makubwa.
Alisema tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 9:00 alasiri katika
bandari ya Mwanza Kaskazini wakati meli hiyo ikipakiwa mizigo tayari kwa
safari ya kuelekea Bukoba ambayo kwa kawaida huanza saa3: 00 usiku.
Kwa mujibu wa Kamanda Mangu, wakati meli hiyo ikiendelea kupakiwa
mizigo, mafundi waashi pia walikuwa wakiendelea na kazi ya kuchomelea
sehemu zilizokuwa zimetoboka.
Alibainisha kuwa cheche za moto ziliruka na kupenya hadi chini ya meli
inakokaa mizigo na kusababisha kuzuka kwa moto ambao uliunguza jumla ya
mito 400 ya makochi ambayo hata hivyo thamani yake haikukujulikana mara
moja.
“Taarifa tulizozipokea ni kwamba hakuna uharibifu mkubwa uliosababishwa
na moto huo isipokuwa mito 400 ya makochi iliyokuwa ikisafirishwa kama
mizigo ndiyo iliyoteketea kwa moto, lakini thamani yake bado
haijafahamika tunaendelea kuwasiliana na wahusika ili watueleze,”
alisema.
Hata hivyo, alisema aliwasiliana na Kampuni ya Huduma za Meli (MSC) na
wamemthibitishia kuwa meli hiyo ilitarajiwa kuendelea na safari ya
kwenda Bukoba kwa vile hakuna hitilafu yoyote ya kiufundi iliyotokea.
Ofisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra)
mkoani Mwanza, Japhet Loismeye, alisema ukaguzi uliofanywa umeonesha
meli hiyo haikupata matatizo yoyote ya kiufundi hivyo inaruhusiwa
kuendelea na safari baada ya taratibu zingine kukamilika.
No comments:
Post a Comment