JAJI Mkuu, Mohamed Chande Othman, ambaye amefafanua suala la yeye
kutoshiriki katika kesi ya aliyekuwa Mbunge wa Arusha
JAJI Mkuu, Mohamed Chande Othman ameeleza sababu
za kutokuwa kwenye jopo la majaji waliopangwa kusikiliza kesi ya
aliyekuwa mbunge wa Chadema mkoani Arusha, Godbless Lema.
Jaji mkuu, alitoa maelezo haya jana alipozungumza
na gazeti hili katika mahojiano maalumu kwenye mahafali ya 12 ya Chuo
cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).
“Ngoja nitolee ufafanuzi suala hilo ili jamii
itambue utaratibu wa uendeshaji wa Mahakama ya Rufani, ambayo ina majaji
16 nchini,” alisema Jaji Othman.
Jaji Othman alisema kimsingi hajajitoa
kushughulikia kesi hiyo, ila siku ambayo kesi hiyo inatajwa, atakuwa
nchini India kuhudhuria Mkutano Mkuu wa 13 wa Majaji Wakuu Duniani.
Maelezo hayo ya Jaji Chande yamekuja siku tatu
baada ya gazeti hili kuripoti kuwa, mkuu huyo wa mhimili wa Mahakama
nchini amejitoa kusikiliza kesi hiyo na nafasi yake imechukuliwa na Jaji
Bernard Luanda.
“Kwanza ifahamike kwamba, jaji wa Mahakama ya
rufani hana ubia na kesi yoyote kwa mujibu wa utaratibu. Jaji yeyote
kati ya majaji 16 wa mahakama ya rufani nchini ana mamlaka ya kusikiliza
kesi yoyote ya rufani,” alieleza Jaji Othman.
Jaji Othman alifafanua kuwa, rufani ya Lema ni
miongoni mwa kesi tatu za uchaguzi zilizobaki ambazo kwa mujibu wa
taratibu za kisheria, huanza kusikilizwa baada ya muda wa mwaka mmoja na
hukumu yake ni lazima itolewe ndani ya mwaka mmoja tangu kuanza kwake.
“Hivyo basi, kwa vile Jaji yeyote wa Mahakama ya
Rufaa anaweza kuisikiliza kesi hiyo, hakukuwa na sababu inisubiri mimi,”
alisema.
Jaji Othman alitaja kesi nyingine za uchaguzi
zitakazoanza kufanyiwa vikao vya rufani na jopo la majaji wa Mahakama ya
Rufani kuwa, ni ile ya Jimbo la Ubungo kati ya Hawa Ng’umbi na John
Mnyika ambayo itakuwa chini ya jopo la majaji watatu; Jaji Nathalia
Kimaro, Jaji Salum, Salum Masati na Jaji Katherine Oriyo.
Nyingine ni ya Jimbo la Ilemela ya Yusuph Yussuph
Masengela Lupilya na wenzake wawili dhidi ya Highness Kiwia na wenzake
wawili, ambayo itakuwa chini ya jopo la Majaji Januari Msofe, Jaji Beard
Luanda na Jaji Salum Massati.
Alisema rufani ya Lema haijaanza kusikilizwa kwa jaji yeyote, hivyo yeye asingeweza kujitoa kwa kuwa hajapangiwa.
“Kinachotatiza hapa ni kwamba, watu
wanaifungamanisha rufani hii na ile ya Arusha ambayo mimi nilikuwa
miongoni mwa jopo la majaji kama mwenyekiti.
“Ile ilikuwa ni pingamizi ya rufani, wakati hii ya Dar es salaam
ni rufani ambayo lazima isikilizwe hadi kufikia hukumu,” alisema Jaji
Chande.
Alisisitiza kuwa, hajajitoa wala hajaombwa kujitoa
kwenye rufani kwa kuwa haifungamani na ile ya Arusha ambayo alikuwa
mwenyekiti wa Jopo la Majaji, huku akifafanua kuwa kesi hiyo ya Arusha
ilikuwa ya kupinga rufani na hii ya sasa inayosikilizwa Dar es salaam ni
ya rufaa na inaanza upya kisheria.
Alieleza kuwa, Desemba 4, mwaka huu vitaanza vikao
vya majaji wa mahakama ya rufaa vya kupitia kesi za rufani za uchaguzi
zilizopangwa kufanyika Dar es Salaam, Zanzibar na Iringa wakati atakuwa
kwenye mkutano mkuu wa majaji duniani utakaofanyika Lucknow, India.
Kuhusu kesi hiyo kuhamishiwa Dar es Salaam, Jaji Othman alisema wanasheria wa Godbles Lema ndiyo walioomba ihamishiwe huko.
“Suala la kuhamishiwa rufani hiyo Dar es Salaam si
la Mahakama ya Rufani bali waaliomba wanasheria wa Lema na hii
inakubalika kwa lengo la kukimbizana na muda kabla ya kufikia tamati,
kwani mahakama imepewa muda wa kumaliza kesi zote za uchaguzi kabla ya
Uchaguzi Mkuu ujao,” alisema Chande.
Mahakama hiyo ilikubali hoja ya wajibu rufaa kuwa,
rufaa hiyo ilikuwa na dosari kutokana na tofauti ya vifungu vya sheria
vilivyotumika katika hukumu iliyomvua ubunge Lema na vilivyotumika
katika hati ya kukaza hukumu, iliyowasilishwa mahakamani sambamba na
rufaa hiyo.
Hata hivyo, kilichomwokoa Lema ni kifungu cha 111
cha Kanuni za Mahakama, ambapo mahakama hiyo ilisema kuwa chini ya
kanuni hiyo, dosari hizo zinaweza kurekebishwa.
Jaji Chande ndiye aliyekuwa kiongozi wa jopo la
majaji watatu katika kesi hiyo akiwamo Salum Massati na Natalia Kimaro.
Jaji Mkuu aliingia kwenye kesi hiyo akichukua nafasi ya Jaji Mbarouk
Salim Mbarouk aliyekuwa amepangwa awali, ambaye sababu za kuondolewa
hazikuwekwa wazi.
No comments:
Post a Comment