Washukiwa wa ICC Kenya kuunda Muungano


Uhuru Kenyatta ni mmoja wa washukiwa wakuu wa ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007

Washukiwa wawili wakuu wa ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya, Uhuru Kenyatta na William Ruto wanajadiliana kwa lengo la kuunda muungano wa kisiasa watakaotumia kugombea uongozi wa nchi.

Taarifa za awali zilisema kuwa wawili hao tayari wameunda muungano huo ingawa baadaye afisa wa mawasiliano wa vigogo hao alikana kuwepo makubaliano yoyote.

Na hataua ya wawili hawa inakuja wakati mahakama ikitarajiwa kutoa uamuzi kuhusu ikiwa wanaweza kugombea uongozi wakati wanakbiliwa na tuhuma za kuhusikana ghasia za baada ya uchaguzi ambapo mamia ya watu waliuawa.

Wanasema wameamua kuunda muungano watakaoutumia kuwania nafasi ya rais na makamu wake katika uchaguzi mkuu mwaka ujao kama ishara ya kuwapatanisha wakenya.

Wanatarajiwa kufika mbele ya mahakama ya ICC baada ya uchaguzi mwaka ujao kujibu mashtaka ya kuhusika na ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi mwaka 2007-2008

Kenyatta ambaye ni naibu waziri mkuu na Ruto ambaye ni mbunge , wanasema kuwa muungano wao utakuwa wenye kauli mbiu ya kupigia debe umoja wa kitaifa, ustawi na kupatanisha wakenya .

Katika uchaguzi uliopita, wawili hao walikuwa pande pinzani. Na ulikuwa uchaguzi ulioshuhudia upinzani mkali zaidi katika historia ya Kenya.

Ulifuatiwa na ghasia za kikabila ambapo mamia ya watu waliuawa na maelfu wengine kuachwa bila makao mwaka 2007.

Wawili hao wamekanusha madai ya kuhusika na ghasia za baada ya uchaguzi hasa kupanga makundi ya watu walioshambulia makundi hasimu.

No comments:

Post a Comment