Udoso ilichukua hatua hiyo baada baadhi ya vyombo vya habari nchini
kuripoti taarifa kuwa baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho wanajihusisha na
biashara hiyo ya ngono.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kwa niaba ya wanafunzi hao, Rais
wa Udoso, Yunge Paul, alisema kuwa tayari kazi hiyo imeanza na
watakaobainika watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Alisema kuwa watu hao wanashusha heshima ya chuo hicho kikubwa na kama taasisi ambayo imebeba wasomi wengi na ni kioo cha jamii.
Aidha, alisema taarifa hiyo ya kashfa ya ngono iliyoripotiwa na vyombo
vya habari imesononesha nchi nzima ukiwamo uongozi wa chuo.
“Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari kwa kweli imesononesha nchi
nzima ikiwamo Udom yenyewe na wanafunzi na hivyo kuwajengea mashaka hata
waajiri wao ambao wanatambua wapo hapo kwa ajili ya kusoma,” alisema.
Aliwaomba waandishi wa habari kushirikiana na taasisi hiyo katika
kuhakikisha wale wote wanaojihusisha na biashara hiyo wanabainika.
Wiki iliyopita kituo kimoja na televisheni kilionyesha picha za baadhi
ya wasichana wanaodaiwa kuwa ni wanafunzi wa chuo hicho wakifanya
biashara hiyo katika moja ya mitaa ya mjini hapa.
Pia katika mahojiano hayo, baadhi ya wanafunzi walionyesha kusikitishwa na vitendo hivyo na kuongeza kuwa vinawadhalilisha.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Idrissa Kikula,
alikaririwa akisema ni vigumu kuwabaini wanafunzi wanaojihusisha na
biashara.
Alisema watatumia Jeshi la Polisi kuwabaini wanafunzi hao ili wachukuliwe hatua.
No comments:
Post a Comment