Kanisa lachomwa Zanzibar

Mkuu wa Jeshi la Polisi,Said Mwema 


SIKU tatu baada ya kuuawa kwa kupigwa risasi Padri Evarist Mushi Mjini Zanzibar, Kanisa la The Pool of Siloam lililoko katika Shehia ya Kianga, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, limechomwa moto na watu wasiojulikana na kuharibu madhabahu yake.


Kuchomwa moto kwa sehemu ya kanisa hilo, kumetonesha kidonda cha kifo cha Padri Mushi ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi kichwani, Jumapili asubuhi mjini Zanzibar. Padri huyo anazikwa leo.


Akizungumza katika kanisa hilo, Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai upande wa Zanzibar ambaye pia ni Naibu Kamishna wa Polisi, Yusuf Ilembo alisema tukio hilo limetokea kati ya saa tisa usiku na saa 10 alfajiri ya kuamkia jana.


“Mlinzi aliona watu watatu wakiwa ndani ya eneo la kanisa na alipowakaribia wakaendelea kupanda ngazi kwenda juu. Baadaye walirudi na kuanza kumrushia mawe akakimbilia nje kupitia dirishani. Ghafla akaona moto unawaka, kumbe walikuwa wamechoma viti vya plastiki vilivyokuwa ndani,” alisema Naibu Kamishna Ilembo.


Mlinzi huyo, Mussa Jackson alisema: “Niliona watu watatu wakipita na baadaye wakawa wanarusha mawe, mwisho nikakimbia na kumwambia jirani na kumpigia simu mchungaji msaidizi. Wakati nakwenda kwa jirani nikaona moto mkali unawaka kanisani, sikujua wameuwashaje.”


Mchungaji Msaidizi wa Kanisa hilo, Penuel Elisha alisema tukio hilo ni la pili kwa kanisa hilo kwani mwaka 2011 zaidi ya watu 80 wakiwa na mapanga, nyundo na magongo walilivamia na kulivunja kabisa.


Alilishukuru Jeshi la Polisi kwa kuwahi kuwasaidia katika tukio la jana.
Licha ya kutotaka kuonyesha uhasama na msikiti uliopo eneo hilo, Penuel alisema siku moja kabla ya tukio hilo viongozi wa msikiti huo walihoji uhalali wa kujengwa kwa kanisa hilo.


“Siku moja kabla ya tukio la mwaka 2011, viongozi wa msikiti walihoji uhalali wa sisi kujenga kanisa hapa. Sisi tukawaonyesha vibali vyote. Lakini kesho yake kanisa likabomolewa. Hatuna mgogoro na msikiti, kwanza hayo matukio ni ya kawaida tu hapa Zanzibar,” alisema Penuel.


Alipoulizwa kuhusu kuwapo kwa uhasama kati ya msikiti na kanisa hilo, Imamu wa msikiti huo, Hassan Migirimu alikanusha akisema kuwa mzozo huo ulikuwa kati ya kanisa na Sheha Assed Mvita ambaye amefariki dunia.


“Sisi hatuna mgogoro na hilo kanisa aliyekuwa akihoji uhalali wake ni marehemu Assed Mvita. Hatujawahi kugombana na kanisa hilo hata siku moja,” alisema Imamu Migirimu.


Padri Mushi kuzikwa leo
Padri Mushi anatarajiwa kuzikwa leo eneo la Kitope na ibada ya mazishi itaanza saa nne asubuhi katika Parokia ya Mtakatifu Joseph Minara Miwili.


“Baada ya kikao cha Baraza la Walei tulikubaliana kuwa ibada ya mazishi itafanyika hapa Parokia ya St. Joseph Minara Miwili na mwili wake utazikwa Kitope wanakozi kwa viongozi wa kanisa,” Askofu wa Kanisa Katoliki Zanzibar, Augustino Shao alisema jana.
Akizungumzia sababu ya Padri Mushi kuzikwa Zanzibar badala ya kusafirishwa kwenda kwao Moshi mkoani Kilimanjaro, Askofu Shao: “Padri Mushi ameishi Zanzibar tangu akiwa na miaka 18 hivyo ni mkazi wa Zanzibar... Hakuna sababu ya kusafirishwa. Mimi ndiye niliyekuwa mlezi wake hivyo hakuna sababu ya kumpeleka kuzika kwa askofu mwingine.”Awali, ilielezwa kuwa Rais Jakaya Kikwete angeongoza viongozi wa Serikali katika mazishi hayo. Hata hivyo, hakuna na taarifa rasmi iliyotolewa.


Marehemu Padri Evarist Mushi alizaliwa Juni 15, 1957 katika Kijiji cha Uru Kimanganuni, Kilimanjaro na baada ya kumaliza elimu ya juu ya sekondari mwaka 1976, alijiunga na Seminari Kuu Kibosho alikopata elimu ya falsafa kati ya mwaka 1978 na 1979.
Mwaka 1980 alijiunga na Seminari ya Kuu ya Mtakatifu Paulo, Kipalapala mkoani Tabora alikopata elimu ya tauhidi (theology) hadi mwaka 1982.


Mwaka 1984 alirudi Kipalapala mkoani Tabora kuendelea na masomo na mwaka huo huo alipata Daraja la Ushemasi katika Parokia ya Bikira Maria wa Rosari Kitope mjini Zanzibar.
Desemba mwaka huo pia alipewa daraja la upadri na Mhashamu Baba Askofu Bernard Ngaviliau katika Kanisa la Mt. Joseph Minara Miwili Zanzibar.


Katika maisha yake ya upadri alishikilia vyeo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa Paroko wa Parokia ya Bikira Maria wa Rosari, Kitope mwaka 1985, Paroko wa Parokia ya Moyo Safi wa Maria wa Wete Pemba na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Antoni wa Padua Machui.
Mwaka 1995 alikwenda Chuo cha Amecea Pastoral Institute Gaba kilichopo Eldoret, Kenya alikopata elimu ya kichungaji na mwaka 2003 alikwenda Marekani kusomea Shahada ya Uzamili ya Masomo ya Elimu katika Mitalaa na Ushauri.


EU yalaani mauaji
Ujumbe wa Umoja wa Ulaya, (EU) umelaani mashambulizi ya hivi karibuni ya viongozi wa dini na zaidi mauaji ya Padri Mushi aliyeuawa kwa kupigwa risasi Februari 17 mjini Zanzibar.


Taarifa ya EU iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Siasa, Habari na Mawasiliano, Tom Vens imezitaka mamlaka husika kuchukua hatua za makusudi kuwakamata wahusika na kufanya uchunguzi wa kina wa mauaji hayo pamoja na mashambulizi yaliyopita ya viongozi wa dini na kusema uhuru wa kuabudu ni haki ya kila mtu inayohitaji kulindwa na kuheshimiwa.


Wamarekani
Polisi imesema ipo tayari kuishirikisha Marekani katika kuwasaka watu waliohusika na mauaji ya Padri Mushi.


Akizungumza kwa simu jana, Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Senso alisema kuna mambo mengi ambayo Marekani imekuwa ikiisaidia Tanzania na kufanikisha hivyo Polisi inaamini kwamba hata jambo hilo litafanikiwa.


“Ni kitu kizuri kwa sababu tumekuwa tukishirikiana nao katika mambo mengi. Hii haitakuwa mara yao ya kwanza, tutashirikiana nao katika kuhakikisha kwa mba nchi yetu inakuwa salama zaidi... unajua siyo lazima kila kitu utangaze lakini tunashirikiana nao sana na teknolojia yao ipo juu,” alisema Senso.


Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema kushirikiana na Marekani hakumaanishi kwamba Tanzania haina wapelelezi wazuri, bali ni kutaka kuongezewa nguvu ambayo labda inaweza kufanikisha kuwanasa wahusika halisi.

No comments:

Post a Comment