WATU 54, wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Katibu wa
Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, waliokamatwa
kwa tuhuma za kufanya maandamano haramu, jana walifikishwa kortini.
Washtakiwa hao walikamatwa Ijumaa iliyopita
wakidaiwa kufanya maandamano haramu kwa lengo la kwenda kwa Ofisi ya
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ili kumshinikiza kumpa dhamana Sheikh Ponda
na mwenzake Sheikh Mukadamu Swalehe.
Walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, juzi na kusomewa mashtaka manne yakiwamo ya kufanya
maandamano yaliyozuiliwa na polisi.
Wakili wa Serikali, Zuberi
Mkakati alidai kuwa upelelezi umekamilika. Jana washtakiwa hao
walisomewa maelezo ya awali (PH) na kisha kesi hiyo inayosikilizwa na
Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo, ikaanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa
mashtaka.
Akiwasomea mashtaka yao, Wakili wa Serikali
Peter Njike akisaidiana na mawakili wengine wa Serikali, Bernard
Kongola, Joseph Maugo na Nassoro Katuga, alidai kuwa washtakiwa hao
walikamatwa wakifanya maandamano haramu Februari 15, 2013.
Wakili Njike alidai kuwa awali polisi walitoa
zuio la maandamano hayo, lakini washtakiwa hao walikaidi na kwamba hata
siku ya tukio polisi waliwaamuru kutawanyika katika mikusanyiko
waliyokuwa wakiifanya, lakini walikaidi, ndipo wakakamatwa na kufikishwa
mahakamani.
Mshtakiwa wa kwanza Salum Makame, alikiri
kukutwa na kisu na kipaza sauti lakini akakana kuwa hakuwa mfuasi wa
Ponda. Wengine pia wakikana kuwa wafuasi wa Ponda wala kufanya
maandamano hayo.
Kutokana na washtakiwa hao kukana, upande wa
mashtaka ulianza kutoa ushahidi ukianzia na Mkuu wa Upelelezi Kanda ya
Dar es Salaam (ZPC), Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Ahmed Msangi.
Katika ushahidi wake, ACP Msangi alidai kuwa
akiwa Kaimu wa Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Februari 11,
2012 alipokea barua ya taarifa ya kuwepo kwa maandamano hayo kutoka kwa
Shura ya Maimamu Tanzania na Jumuiya na Taasisi za Kiislamu.
Alidai kuwa barua hiyo iliyosainiwa na Amiri
wa Shura ya Maimamu, Temeke, Sheikh Juma Idd, ilieleza kuwa watafanya
maandamano Februari 15,2013, baada ya swala ya Ijumaa kutokea misikiti
yote Dar na kwamba wanaomba ulinzi.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi leo itakapoendelea tena leo.
No comments:
Post a Comment