Profesa Lipumba aliyekuwa akizungumza na Mwananchi alisema, chama chake
kimeshangazwa na namna ofisi hiyo ya msajili ilivyotoa usajili wa
kudumu kwa chama kipya cha kisiasa Democratic Change ADC ambacho
kinadaiwa kuzoa wanachama wengi toka ndani ya CUF.Mwenyekiti
Cha Chama Wananchi(CUF), Ibrahimu Lipumba amemtuhumu Msajili wa Vyama
Vya Siasa Nchini, John Tendwa kuwa anaendesha njama za kukizorotesha
chama chake na ametaka mamalaka za kiutendaji kuanzisha uchunguzi wa
kimahesabu kwa ofisi ya msajili huyo.
Kauli ya Profesa Lipumba inakuja siku
chache baada ya ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kutoa usajili wa
kudumu kwa chama kipya ambacho wachunguzi wa mambo wanadai ni matokeo
ya mvutano wa kiuongozi uliokikumba chama hicho na kusababisha baadhi
ya wanasiasa ndani ya chama hicho kukitupa mkono na kuanzisha harakati
mpya.
Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, ofisi ya msajili wa vyama vya siasa
inacheza karata yenye sura ya upendeleo ambayo pia imelenga kuzorotesha
ngome ya vyama vya upinzani. “ Sisi tunashangaa msajili wa vyama kuwa
na haraka ya kutoa usajili huu wa kudumu hivi alikuwa na haraka gani
kufanya hivi?” alihoji Mwenyekiti huyo.
Alisema ofisi hiyo ya msajili, ilizuia
kwa makusudi juhudi za kusajiliwa kwa chama kipya cha CCJ ambacho
amedia kuwa kilikuwa na wafuasi toka chama tawala CCM lakini alichukua
mkondo mwingine kutoa usajili wa kudumu kwa chama hiko kipya kwa vile
waasisi wake ni kutoka chama cha CUF.
“ Huyu msajili ana lake jambo, mbona
wakati ule aliweka ngumu juhudi za kusajiliwa kwa chama cha CCJ? Au kwa
vile waasisi wake walikuwa wakitoka ndani ya CCM, ... Sasa kwa vile
wafuasi wa chama hiki wanatoka ndani ya Cuf basi haraka haraka ametoa
usajili wa kudumu,”alisema Profesa Lipumba.
Mwenyekiti huyo ambaye chama chake kinakusudia kufanya mkutano mkubwa
wa hadhara mwishoni mwa juma jijini Dar es Salaam, alisema kuna haja
sasa ya kuanzisha uchunguzi wa kimahesabu dhidi ya ofisi ya msajili ili
kufichua mambo yaliyojificha ndani yake.
“ Huyu msajili lazima sasa afanyiwe auditing, tujue anaendesha vipi
mambo yake maana tunatilia shaka utendaji wake, haiwezekani chama
kimoja leo kinakuja kuomba usajili kinanyimwa kisha baadaye kinakuja
kingine kinakubaliwa, lazima msajili huyu afanyiwe
auditing,”alisisitiza Profesa Lipumba.
Alipotakiwa kuelezea mwelekeo wa chama chake kutokana na kumeguka kwa
baadhi ya wanachama na viongozi wa kada ya kati waliojiunga na chama
kipya cha ADC, Profesa Lipumba alisema “ hilo kwetu halitunyimi
isingizi, isitoshe pia kila raia ana haki ya kuchagua na kujiunga na
chama chochote akipendacho”.
Hata hivyo alisema, anashangazwa na tukio la mwanasiasa Hamad Rashid
aliyetangaza kuwa mlezi wa chama hicho kipya cha siasa kwa kauli yake
ya kukusudia kutumia uchaguzi mdogo wa Jimbo la Bububu visiwani
Zanzibar kujipima namna kinavyokubalika kwa wapiga kura.
“Huyu Hamad Rashid ,sisi tumemtimua kwenye chama, amekwenda mahakamani
kupinga uamuzi wetu na sasa anatajwa kuwa mlezi wa chama kingine cha
siasa, hivi kweli mtu anaweza kuwa mwanachama wa vyama viwili kwa
wakati mmoja?” alihoji Profesa Lipumba na kuongeza kuwa:
“ Kwa vile suala hili liko mahakamani tunaamini mahakama inashuhudia mwenendo huu na itafanya kazi yake”.
Msajili wa vyama ajitetea
Msajili wa vyama vya siasa John Tendwa amesema kuwa usajili wa chama
hicho kipya haukuegemea matakwa ya upande fulani wa kisiasi bali
ulifanyika kwa kuzingatia sheria na kanuni na wakati huo huo, amefungua
milango kuwakaribisha wakaguzi wa mahesbu.
Alikosoa matamshi ya Profesa Lipumba aliyemtuhumu ofisi yake kukwamisha
juhudi za usajili wa Chama Cha CCJ ambacho harakati zake ziligonga
mwamba ikiwa imesalia miezi michache kabla ya kuanza mchaka mchaka wa
kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010 na hatimaye kuzaliwa kwa
chama kingine cha CCK.
“Hiki Chama Cha CCJ ambacho Lipumba anakitolea mfano, hakikujipanga
kilikuwa hakina wanachama, sasa mimi nitatoaje usajili kwa chama
hakijatimiza masharti,”alisema Tendwa.
Kwa mujibu wa Tendwa chama hicho hakikuchukua hatua zinazopaswa ikiwamo
kutoa taarifa za uongo kuhusu wanachama wake na kukosa wawakilishi wa
kutoka mikoani.
“ Jambo la kushangaza hata baadhi ya
viongozi wake hawakuwa wanachama. Mfano huyu Mpendazoe aliyehamia
Chadema alikuwa ni Public Secretary wa chama, lakini hakuwa na kadi ya
uanachama… ndugu yangu katika mazingira kama hayo chama kinawezaje
kupata usajili wa kudumu”.
Kwa upande mwingine msajili huyo,
alisema suala la utoaji usajili wa kudumu kwa chama chochote cha siasa
linafanyika katika mazingira ya uwazi na ndivyo ilivyofanyika kwa chama
kipya cha ADC ambacho alidai kuwa kilihitimisha masharti kwa wakati na
hatimaye kukubalika kuanza rasmi shughuli za kisiasa.
Amemtaka Profesa Lipumba pamoja na wataalamu wengine kujitokeza katika
ofisi yake kwa ajili ya kuendesha ukaguzi wa mahesabu na amesisitiza
kuwa ofisi yake hufanyiwa ukaguzi wa mahesabu kila baada ya miezi
mitatu.
Kupatiwa usajili wa kudumu kwa chama hicho kipya sasa kunafanya jumla
ya vyama vya siasa ambavyo vimepata baraka ya kuendesha siasa kufikia
20.
|
No comments:
Post a Comment