Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana
SAKATA la gesi sasa limeingia hatua mpya, baada
ya watendaji wakuu wa CCM; Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana na Katibu wa
Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye kuitaka Serikali ikae na wana-Mtwara ili
kuona namna ya kumaliza mgogoro huo kwa amani.
Kinana na Nape walitoa kauli hizo kwa nyakati
tofauti jana. Wakati Kinana alisema hayo alipokuwa akizungumza katika
mkutano wa hadhara mkoani Kigoma, Nape alifanya hivyo kupitia mtandaowa
Twitter na baadaye kuthibitisha kauli hiyo alipoulizwa na mwandishi
wetu.
Wakati watendaji hao wa CCM wakitoa matamko
hayo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana alifanya vikao mfululizo mkoani
Mtwara akisaka suluhu ya mgogoro huo.
Kinana na Nape
Akizungumza katika mkutano
wa hadhara uliofanyika kwenye Ofisi za CCM Wilaya ya Uvinza, Kigoma,
Kinana aliitaka Serikali isikilize hoja za wakazi wa Mtwara na
kuzitafutia usumbufu sahihi.
Mbali na kutoa ushauri huo, aliitaka pia
Serikali kuwasaka watu wanaochochea mgogoro huo kwa kufanya vurugu na
kuharibu mali za watu na kuwafikisha mbele ya sheria.
“Serikali ikae
na wana-Mtwara na kuwasikiliza, wananchi hao wana hoja na Serikali
inapaswa kutoa majibu sahihi kwa hoja hizo. Lakini pia iwasake na
kuwachukulia hatua za kisheria waliosababisha uvunjifu wa amani,”
alisema Kinana.
Kwa upande wake, Nnauye aliitaka Serikali
kuwasikiliza wananchi wa Mtwara kwa kuwa madai yao ni ya msingi...
“Wakazi wa Mtwara na Lindi wanazo hoja za msingi juu ya suala la gesi,
hoja ambazo ni muhimu kusikilizwa na kupatiwa majibu sahihi.”
Nape alisema hoja za wakazi hao ni za msingi
lakini akaongeza kuwa kuna baadhi ya wahuni ambao wanatumia mwanya huo
kupora na kuharibu mali za watu. “Kuna uhusiano gani kati ya hoja yao ya
madai ya gesi na kuchoma nyumba za watu, kuharibu mali za umma na
magari ya watu. Kuna kundi la wahuni ambalo Serikali inatakiwa
kuhakikisha inapambana nalo na kuwachukulia hatua kali za kisheria,”
alisema Nape.
Pinda asaka suluhu
Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda jana alikuwa na kibarua kizito kusaka suluhu ya mgogoro wa gesi
baada ya kuzungumza na makundi mbalimbali ya kijamii kupata mawazo yao.
Pinda aliyeongozana na Waziri wa Mambo ya
Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema na
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja alianza kazi hiyo juzi
kwa kufanya vikao vya ndani na viongozi wa Serikali mkoa wa Mtwara.
Habari kutoka Mtwara zinaeleza kuwa kutwa nzima ya jana, Waziri Mkuu
Pinda alikuwa akifanya mikutano mbalimbali na makundi kadhaa kwa lengo
la kupata suluhu ya mgogoro huo wa gesi.
“Alianza kwa kufanya mazungumzo ya ndani na
viongozi wa dini, wanaharakati, wanasiasa na baadaye viongozi wa
Serikali za Mitaa,” kilieleza chanzo cha habari kutoka Mtwara.
Mbali
na viongozi hao, Pinda pia alizungumza na wafanyabiashara, viongozi wa
CCM na madiwani kabla ya mkutano wake na waandishi wa habari aliopanga
kuufanya baadaye jioni.
Mmoja wa madiwani waliohudhuria mkutano huo
wa Pinda alilieleza gazeti hili kuwa, Waziri Mkuu aliwaambia kuwa
mkutano wake huo ni kwa ajili ya kukusanya maoni.
“Amesema amekuja kukusanya maoni na baadaye
atakwenda kushauriana na Rais Jakaya Kikwete na atatoa tamko kuhusu
hatima ya suala hilo baadaye,” alisema diwani huyo akimnukuu Waziri Mkuu
Pinda.
Gesi kuteka Bunge
Mkutano wa Kumi wa Bunge unaanza leo mjini Dodoma, huku suala la gesi likitarajiwa kutawala mijadala mbalimbali ya wabunge.
Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Habib Mnyaa ni miongoni mwa wabunge
waliotangaza mapema kuwa watazungumzia suala hilo bungeni. Mnyaa alisema
anakusudia kuwasilisha hoja binafsi za maombi ya wakazi wa Mtwara
kupinga gesi kupelekwa Dar es Salaam.
Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Mawasiliano ya
Bunge, Deogratius Igidio aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa
shughuli zote zitakazofanyika ndani ya ukumbi huo zitajulikana leo baada
ya Kikao cha Kamati ya Uongozi.Katika kipindi cha wiki nne sasa
kumekuwa na maandamano, malumbano na vitendo vya ghasia kuhusiana na
mradi wa kujenga bomba la kusafirishia gesi asilia kutoka Mtwara hadi
Dar es Salaam hatua ambayo inapingwa na wananchi wa eneo hilo ambao
wanadai kuwa wamesahauliwa katika miradi ya maendeleo.
Wananchi hao wa Mtwara wanataka kusitishwa kwa
mpango wa kusafirisha gesi hiyo kwa madai kuwa, eneo la Mtwara
halijaendelezwa na mara zote Serikali haijaweka vipaumbele kwa ajili ya
kusukuma mbele eneo hilo.
Wanataka uendelezwaji wa gesi hiyo ufanywe
mkoani humo kwa madai kuwa utasaidia kuchochea shughuli za maendeleo na
kuufanya uanze kuinuka kiuchumi.
Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa ambaye pia ni
mwenyeji wa mkoa huo ametoa wito wa pande zote kukutana na kujadiliana
ili kumaliza mvutano huo akisema ni jambo la kufedhehesha na kusikitisha
kuona wananchi wakianzisha maandamano na kupinga mradi huo wa Serikali.
Chadema hakitaki
Chadema kimeitaka Serikali
kusitisha mpango wa kusafirisha gesi iliyogunduliwa mkoani Mtwara
kwenda Dar es Salaam mpaka itakapokutana na wananchi na kufikia
maridhiano kwa pamoja.
Chama hicho pia kimeitaka Serikali iweke wazi
mikataba yote 26 ya kampuni ilizoingia nayo kwa ajili ya kuchimba
nishati hiyo ili wananchi waweze kuijua.
Mwenyekiti Freeman Mbowe alitoa wito huo jana
alipokuwa akifungua mkutano wa siku moja wa Baraza Kuu la chama hicho,
Dar es Salaam... “Kwa muda mrefu watu wamekuwa wakiuliza Chadema nini
kauli yenu kuhusu mgogoro huo na kutaka kujua tuko na wananchi au
Serikali? Chadema iko nyuma ya wananchi,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Serikali iache kufanya kazi ikiwa Dar es
Salaam iende kwa wananchi na kuzungumza nao na wakikubaliana kwa pamoja
ndipo mradi huo utekelezwe.”
Habari hii imeandikwa na Raymond Kaminyoge, Kigoma; Ibrahim Yamola, Dar na Habel Chidawali na Ibrahim Bakari, Dodoma.
No comments:
Post a Comment