TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Oktoba 12, 2012
VPL KUENDELEA KUTIMUA VUMBI KESHO.
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom inaendelea kesho (Oktoba 13 mwaka huu)
kwa timu kumi kupambana kwenye viwanja vitano tofauti katika raundi ya
saba ya ligi hiyo yenye timu 14.
Polisi Morogoro itaikaribisha Azam
kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro wakati mwamuzi wa FIFA, Oden
Mbaga atakuwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya kuchezesha
mechi kati ya wenyeji Tanzania Prisons na Oljoro JKT.
Jijini Tanga, Simba itakuwa mgeni wa
Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani katika mechi itakayochezeshwa
na mwamuzi Simon Mberwa kutoka Pwani akisaidiwa na Godfrey Kihwili na
Abdallah Uhako wote kutoka Arusha.
Mechi nyingine za kesho ni Ruvu
Shooting dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi,
na Mtibwa Sugar watacheza na Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Manungu,
Turiani mkoani Morogoro.
Wakati huo huo, Azam imeomba mechi zake
za nyumbani dhidi ya Yanga na Simba zichezwe kwenye uwanja wake wa Azam
Complex ulioko Chamazi badala ya Uwanja wa Taifa.
Nayo Ruvu Shooting imeomba mechi yake ya ugenini dhidi ya Yanga ya
Oktoba 20 mwaka huu ichezwe Uwanja wa Taifa badala ya Uwanja wa Azam
Complex.
Maombi hayo yatawasilishwa kwenye kikao cha Kamati ya Ligi ya TFF
kinachotarajiwa kufanyika kesho (Oktoba 13 mwaka huu) kwa ajili ya
kufanyiwa uamuzi.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF
No comments:
Post a Comment