SIASA za makundi ndani ya CCM,
zimeendelea kujidhihirisha wazi baada ya Katibu wa chama hicho Mkoa wa
Arusha, Mary Chatanda kukwepa kumtambulisha Waziri Mkuu wa zamani na
Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) kupitia Wilaya ya Monduli, Edward
Lowassa aliyekuwa meza kuu.
Tukio hilo la aina yake lilitokea jana
wakati Chatanda akitambulisha wageni waalikwa na viongozi wa Chama na
Serikali waliokuwa meza kuu katika mkutano wa uchaguzi wa nafasi ya
Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha.
Mara baada ya Msema Chochote (MC) kumpa
kipaza sauti, Chatanda alianza kwa kuwatambulisha viongozi hao na
kuwapa nafasi ya kusalimia, lakini ilipofika kwa Lowassa alimruka na
kumkaribisha Mwenyekiti wa Mkoa aliyemaliza muda wake, Onesmo Nangole
ili kumkaribisha mgeni rasmi kufungua mkutano huo.
Kutokana na hali hiyo, wajumbe wa
mkutano huo walianza kupaza sauti huku wakisisitiza ‘bado mjumbe mmoja,
bado mjumbe mmoja’ ndipo Chatanda alipomtambulisha Lowassa na
kumkaribisha kusalimia wajumbe.
Mara baada ya Lowassa, aliyekuwa kiti cha mbele meza kuu, kusimama
ukumbi ulilipuka kwa maneno ya CCM, CCM, CCM ambapo aliwapungia mkono
hadi waliponyamaza.
Hata hivyo, Lowassa licha ya kusimama hakusema chochote hadi wajumbe hao
waliponyamaza ndipo na yeye akaketi.
Chatanda ambaye anatajwa kuwa katika
kambi ya Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, amekuwa akilumbana mara
kwa mara na wana-CCM ambao wanamuunga mkono Lowassa katika chaguzi
mbalimbali.
Hata hivyo, baadaye jioni Lowassa
alitambulishwa na msimamizi wa uchaguzi huo, Jumanne Maghembe ambaye ni
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
Akizungumza wakati wa kumkaribisha Nangole, Lowassa alisema inawezekana
Chatanda alipitiwa kidogo kutokana na hekaheka za chaguzi zilizopita na
hasa baada ya watu aliokuwa anawataka kushindwa. Hata hivyo, Lowassa
alimpongeza katibu huyo kwa kazi nzuri alizofanya.
Lowassa amrushia dongo RC
Kwa upande mwingine, Lowassa alimrushia
dongo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo kuwa ni kijana mdogo,
lakini hana shaka naye na akasema kuwa ni mchapakazi na anapaswa
kusaidia kutatua matatizo mbalimbali yanayoukabili mkoa huo.
Baadaye jioni mwandishi alimfuata Chatanda na kutaka ufafanuzi kuhusiana
na hali hiyo ambapo alijibu kwa mkato kuwa “Sitaki maneno” na kupanda
katika gari lake na kuondoka. Hata hivyo, baadaye alimpigia simu
mwandishi na kusema, “Mpaka ifikie mwanaume anitaje, mimi ni jembe na
moto ni ule ule.”
Awali, katika mkutano huo wa uchaguzi
wajumbe wote walimchagua Lowassa kuongoza kikao hicho hatua ambayo
ilidhihirisha kuimarika kwa kambi yake mkoani hapo.
Lowassa mara baada ya kuchaguliwa kwa kura nyingi, aliwaeleza wajumbe
kuwa amewasikia na hatawaangusha. Katika uchaguzi huo, mchuano mkali
ulikuwa katika nafasi ya uenyekiti, ambapo Nangole ambaye taarifa
zinasema yuko kambi ya Lowassa, alikuwa anachuana na Sheikh Adam Chora
na Dk Salash Toure. Katika uchaguzi huo, kulikuwa na jumla ya wajumbe
855 kati ya wajumbe 897 ambao walipaswa kushiriki.
Matokeo
Akitangaza matokeo hayo, Maghembe alisema, Ole Nangole ameibuka mshindi
wa kiti cha uenyekiti baada ya kupata kura 604 na kufuatiwa na Sheikh
Chora ambaye alipata kura 213. Mgombea wa mwisho ambaye ni Dk Toure
aliambulia kura 15 ambapo jumla ya wapigakura walikuwa 833 na kura 3
ziliharibika.
Imeandaliwa na Mussa Juma na Moses Mashalla, Arusha , MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment