KAMATI ya Hesabu za Mashirika ya Umma (Poac),
imempa onyo kali Kaimu Mkurugenzi wa wa Shirika la Utafiti na Maendeleo
ya Viwanda Tanzania (Tirdo) Ludovick Manege,baada ya kubainika kuwa
alikuwa akitoa maelezo ya uongo ya kushindwa kuwaruhusu wakaguzi kutoka
Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) kufanya
ukaguzi wa gharama za vifaa vya ofisini vilivyonunuliwa Ujerumani na
shirika hilo vyenye thamani ya Sh155milioni.
Mbali na onyo hilo, kamati hiyo pia imemtaka CAG
kufanya ukaguzi maalumu ili kubaini kiasi cha fedha kinachotumika kwa
ajili ya uendeleshaji wa shughuli mbalimbali yakiwamo malipo hewa ya
aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika hilo, Asifael Nanyaro.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam jana, Kaimu Mwenyekiti wa kamati, Mohamed Chombo alisema kuwa,
watendaji wa Tirdo walishindwa kutoa ushirikiano kwa wakaguzi kutoka
Ofisi ya CAG wakati walipokwenda kukagua vifaa hivyo, jambo ambalo
liliwafanya wakae zaidi ya saa matano.
“Tunakupa onyo kali ili iwe fundisho siku nyingine
unapokuja kuzungumza na kamati kuacha kusema uongo, hii inaonyesha wazi
kuwa, hata utendaji wao ni wa ubabaishaji, jambo ambalo limesababisha
kutudanganya,” alisema Chombo.
Alisema,Nanyaro, aliidhinishiwa kulipwa fedha hizo
za pango la nyumba bila ya kufuata taratibu za kisheria wakati alikuwa
akiishi kwenye nyumba za Serikali.
“Kitendo cha Mkurugenzi wa zamani kulipwa
Sh22milioni kama pango la nyumba wakati alikuwa akiishi kwenye nyumba za
Serikali ni ubadhirifu, jambo ambalo kamati yetu imebaini kwa
kushirikiana na ripoti ya CAG,”aliongeza. Manege alikiri kuwapo kwa
tatizo hilo na kudai kuwa, mkurugenzi huyo mstaafu alipewa fedha hizo
kimakosa,lakini walijaribu kumshawishi ili arudishe alikataa.
“Tulimshawishi kurudisha fedha hizi lakini
alikataa, badala yake alitujibu kuwa, yeye ni mteule wa Rais na kwamba
ametoka jeshini hivyo alistahili malipo hayo,” alisema Manege.
Aliongeza Menejimenti iliwasilisha suala hilo
Wizara ya Viwanda na Biashara ili waweze kuangalia njia mbadala ya
kurudisha fedha hizo Hazina. Alisema kutokana na hali hiyo wakaandaa
utaratibu wa kumkata fedha kwenye mafao yake ili waweze kurudisha fedha
hizo ambazo zililipwa kinyume na sheria.
Kwa mujibu wa Chombo, kamati hiyo itamwita Waziri
wa Viwanda na Biashara, Abdalah Kigoda ili waweze kujadiliana jinsi ya
uteuzi wa mkurugenzi mpya kwenye shirika hilo hivi karibuni, jambo
ambalo wanaamini linaweza kuboresha utendaji.
No comments:
Post a Comment