Moto wa gesi wavuka nje ya mipaka


BALOZI wa Norway nchini, Ingunn Klepsvik ameonya kuhusu hatari za kugeuza suala la gesi ya Mtwara kuwa mtaji wa kisiasa.

Wakati Norway ikisema hayo, Mkurugenzi wa Uchumi katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk Nyamajeje Weggoro amesema mgogoro huo utamalizika kwa njia ya mazungumzo na majadiliano yaliyojaa lugha na kauli laini isiyo na vitisho wala kuwabeza wananchi.

Katika siku za karibuni, kumekuwa na mijadala, mizozo na maoni kutoka kwa kada mbalimbali kuhusiana na suala la gesi hiyo inayopatikana katika eneo la Msimbati, Mtwara.

Akitoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Sebastian Kolowa, Lushoto mkoani Tanga, Balozi Klepsvik alisisitiza kuhusu haja ya Watanzania kuweka mbele masilahi ya taifa badala ya kuangalia masilahi ya watu binafsi au taasisi.

“Norway ilipogundua nishati ya petroli tulikubaliana kitu kimoja kwamba suala hili lisihusishwe na kampeni za kisiasa. Hii itasaidia kuweka mbali masuala ya rasilimali na siasa,” alisema.

Balozi huyo alisema gesi ya Mtwara inapaswa kuwanufaisha wananchi wa Mtwara kwanza kabla ya watu wengine, lakini masilahi ya taifa lazima yawekwe mbele katika mjadala wa suala hilo.

Klepsvik alisisitiza kuhusu umuhimu wa kuwashirikisha wananchi katika masuala muhimu ya maendeleo na kueleza kuwa maendeleo endelevu yanapatikana kwa kuwahusisha watu wa kada zote hasa wanawake.

Hata hivyo, alisema endapo mambo yatafanyika kwa utaratibu wake, gesi iliyovumbuliwa inaweza kuwasaidia Watanzania kwa kiasi kikubwa katika maendeleo yao.

“Tulipogundua gesi na petroli, hatukuwa tunafahamu lolote, tuliita wageni wakatufanyia kazi ya kuchimba, wakati huo tulipeleka watu wetu vyuo vya nje kusoma na baada ya miaka 10 sasa tunashughulika wenyewe na kila kitu kwa manufaa ya taifa zima,” alisema Klepsvik.
EAC yashauri mazungumzo
Akizungumzia mgogoro huo, Dk Weggoro alisema umetokana na wananchi kutopata elimu ya kutosha kuhusu namna watakavyofaidika na rasilimali hiyo inayopatikana katika eneo lao.

“Mgogoro wa gesi Mtwara utamalizika kwa njia ya mazungumzo na majadiliano lakini siyo vitisho,” alisema alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya EAC jana.

Alisema haamini kama ni kweli wananchi wa Mtwara hawataki Watanzania wenzao wafaidike na gesi inayopatikana mkoani humo, bali wanahofia hatima ya maisha, faida na masilahi yao kutokana na rasilimali hiyo.

“Viongozi lazima wazungumze, wajadiliane na kufikia mwafaka na wananchi (wanaMtwara), kuhusu mambo yanayogusa maisha na masilahi yao. Ni vyema watu ambao maliasili na rasilimali zinapatikana katika maeneo yao wanufaike kwanza kabla ya wengine.”

 

Alisema hata ndani ya EAC, mipango na mikakati kuhusu rasilimali kama gesi na mafuta ni kuhakikisha wananchi wananufaika kwanza.

Alisema ndiyo maana baada ya mafuta kugundulika Uganda na gesi Tanzania na Kenya, tayari mipango imewekwa kuhakikisha rasilimali hiyo inasambazwa na kuzinufaisha nchi wanachama kwanza kwa kujenga mabomba kuunganisha nchi zote.

Kutokana na ukweli huo, mtaalamu huyo alisema wakati gesi ya Mtwara ikifaidisha Watanzania wote na taifa kwa ujumla, ni lazima faida hiyo ionekane kwa wana Mtwara.

Mtaalamu huyo ambaye ni Mtanzania alisema lazima wananchi wanaoishi kwenye maeneo yanayopatikana rasilimali, waone maisha na huduma zote za kijamii kama elimu, afya na miundombinu zinaboreka.

“Suala siyo gesi kutoka Kusini kwenda Dar es Salaam kwa sababu hata sasa tayari gesi inasafirishwa kutoka huko (mikoa ya Kusini), kwenda Dar es Salaam. Tofauti iliyopo ni kwamba bomba linalokusudiwa kujengwa ni kubwa kuliko lililopo sasa,” alisema Dk Weggoro.
Wapya wajitokeza
Mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Mtwara, yameungana na wananchi wa mkoa huo kupinga mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi hiyo hadi Dar es Salaam.

Yakitoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari mkoani hapa, mashirika hayo kupitia mtandao wake (Mrengo), yamesema yanaungana na wananchi kuishinikiza Serikali kusitisha mradi huo na badala yake ijenge mitambo ya kufua umeme wa megawati 300 pamoja na mitambo ya kugagua gesi mkoani Mtwara.

Sita ataka elimu
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema kwamba hekima, busara na kuelimishana ndiyo njia pekee itakayosuluhisha mgogoro huo wa gesi.

Akizungumza jana, Sitta alisema wakazi wa Mtwara wanapaswa kuelimishwa kwamba mitambo ya kufua umeme wanayoitaka iwekwe mkoani humo haiwezi kutoa manufaa kwao kama wanavyodhani kwa sababu waajiriwa ni wachache.
“Mitambo hii itatoa ajira kwa watu wachache sana. Maana mitambo ikishawekwa watahitajika wachache tu wa kusimamia uzalishaji,” alisema Sitta.

Hivyo, akasema wananchi hao wanatakiwa kuelimishwa kuwa vipo viwanda vingi na vyenye manufaa makubwa vinavyotarajiwa kujengwa Mtwara.
Alitoa mfano wa viwanda hivyo kuwa ni vya saruji, mbolea na upanuzi wa Bandari ya Mtwara.

“Viwanda hivi vya saruji, mbolea na upanuzi wa bandari ni zaidi ya mitambo ya umeme,” alisema Sitta akieleza kuwa mpango wa Serikali kuisafirisha gesi hadi Dar es Salaam ni sahihi kwa sababu umezingatia sababu za kiufundi.

Alisema kusafirisha umeme kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ni gharama zaidi ukilinganisha na usafirishaji wa gesi. Alisema kusafirisha umeme megawati kadhaa zitapotea njiani tofauti na gesi. Alisema kwa sasa Mtwara inatumia megawati 15 tu na tayari kuna mtambo wa kiwango hicho unaotumia gesi.

Alisema Dar es Salaam ambayo ni mji wa viwanda unahitaji zaidi ya megawati 1,000 ili kujitosheleza jambo ambalo lina halalisha uzalishaji kufanyika Dar es Salaam.

 Alisema mahitaji ya umeme Mtwara yanavyozidi kukua ndivyo hivyo na mitambo ya uzalishaji itakavyoongezwa na kusema ipo siku Serikali itapaswa kuzalisha umeme mwingi Mtwara ili uuzwe nchi jirani kama Msumbiji... “Hivyo wakazi wa Mtwara hawapaswi kuwa na wasiwasi kuhusu vitega uchumi kujengwa mkoani mwao.”

No comments:

Post a Comment