.
=====================================================================
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amewasili nchini Kenya Jumanne, 11 Septemba , 2012, kuanza Ziara Rasmi
ya Kiserikali (State Visit) ya siku tatu ikiwa ni ziara yake ya kwanza
rasmi nchini humo ingawa ameshawahi kufanya ziara kadhaa za kikazi
nchini Kenya.
Kwenye
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi, Rais
Kikwete ambaye amefuatana na mkewe, Mama Salma Kikwete, amepokewa na
mwenyeji wake, Rais Mwai E. Kibaki na kwa mbwembwe zote za kiprotokali
zinazoambatana na ziara rasmi za kiserikali.
Baadaye
mchana, Rais amekwenda Ikulu ya Kenya ambako ametia saini kitabu cha
wageni, akafanya mazungumzo ya faragha na Rais Mwai Kibaki kabla ya
kufanyika kwa Mazungumzo Rasmi ya Kiserikali kati ya nchi hizo mbili
majirani na wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC).
Baada
ya mazungumzo hayo, Rais Kikwete na ujumbe wake amekwenda kwenye Chuo
Kikuu cha Kenyatta ambako wamepokewa na Waziri wa Elimu ya Juu,
Mheshimiwa Margaret Kamar, Mkuu wa Chuo hicho, Jaji Mstaafu Onesmus
Mutungi na Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Olive Mugendi.
Kwenye
chuo hicho ambacho Desemba 8, mwaka 2008, kilimtunuku Rais Kikwete
Shahada ya Uzamivu ya Heshima, amefungua rasmi Jengo la Shule ya Ukarimu
na Utalii ya Chuo hicho.
Akizungumza
wakati wa ufunguzi wa Shule hiyo, Rais Kikwete amesema kuwa utalii ni
sekta muhimu sana katika chumi za nchi za Afrika Mashariki na ambayo
mchango wake unagusa maisha ya maelfu kwa maelfu ya wananchi wa nchi za
ukanda huo.
Rais
pia amesema kuwa nchi hizo za Afrika Mashariki sasa zimekuwa ni eneo
lenye mvuto mkubwa katika nyanja ya utalii ambao unaweza kuwaingizia
wananchi na mataifa ya Afrika Mashariki mapato zaidi kama changamoto
zinazoikabili sekta ya utalii kwa sasa zitashughulikiwa ipasavyo na kwa
pamoja na nchi hizo.
Miongoni
mwa changamoto ambazo Rais Kikwete amezitaja ni ukosefu wa miundombinu
ya kutosha kufanikisha kwa namna bora zaidi sekta ya utalii, ukosefu wa
juhudi za pamoja kuitangaza Afrika Mashariki kama eneo muhimu la utalii,
na umuhimu wa kuboresha kiwango cha usalama wa watalii.
Aidha,
Rais Kikwete amezielezea changamoto nyingine kuwa ni pamoja na umuhimu
wa kuwepo na viza ya pamoja ya utalii kwa nchi zote za Afrika Mashariki,
kuwepo kwa safari za ndege za kutosha kutoka kwenye mataifa makubwa
yanayozalisha watalii kwa wingi kuja Afrika Mashariki na umuhimu wa
kupungua kwa nauli za ndege za kuja Afrika Mashariki.
Jioni,
Rais Kikwete ametembelea Taasisi ya Utatifi wa Kilimo ya Kenya (KARI)
ambako anatarajiwa kupokelewa na Waziri wa Kilimo wa Kenya, Mheshimiwa
Dr. Sally J. Kosgei na usiku alikuwa mgeni rasmi kwenye Dhifa ya Kitaifa
ambayo itaandaliwa na mwenyeji wake, Rais Mwai Kibaki.
Leo
Jumatano 11 Septemba, 2012 Rais Kikwete ataweka shada la maua kwenye
Kaburi la Mwanzilishi wa Taifa la Kenya, Hayati Jomo Kenyatta, kwenye
Viwanja vya Bunge la Kenya na kutembelea Kiwanda cha Maziwa cha
Brookside Diary kwenye Barabara ya Thika.
Kwa
mujibu wa ratiba ya ziara yake, Rais Kikwete atatembelea Chuo cha Taifa
cha Ulinzi cha Kenya (National Defence College) kilichoko Karen,
Nairobi, ambako atapokelewa na Waziri wa Nchi wa Ulinzi, Mheshimiwa
Yusuf Haji na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, Jenerali Julius
Karangi.
Baadaye,
Rais Kikwete atakwenda kutembelea Kituo cha Magonjwa ya Moyo na Kansa
kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan ambako atapokelewa na Waziri
wa Huduma za Matibabu, Mheshimiwa Anyang Nyong’o.
Baadaye
jioni, Rais Kikwete, ambaye anaongozana na kundi kubwa la
Wafanyabiashara wa Tanzania, atashiriki chakula cha jioni ambacho
ameandaliwa na Jumuiya ya Wafanya Biashara ya Kenya.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
11 Septemba, 2012
No comments:
Post a Comment