Chadema: Hatuchukui tena makapi ya CCM

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa akizungumza waandishi wa gazeti la Mwananchi katika  mahojiano maalumu  ofisini kwake Makao Makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam wiki iliyopita. Picha na Edwin Mjwahuzi 


Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema hakitasubiri wanachama watakaoachwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye uteuzi wa wagombea katika uchaguzi mkuu ujao.

Kutokana na tamaa ya kuingiza watu wengi kwenye Bunge, vyama vya upinzani vimekuwa na tabia ya kuwapokea wanachama wa CCM wanaoshindwa kwenye kura za maoni na baadaye kuwapa nafasi ya kugombea ubunge, lakini Dk Slaa anasema safari hii hawatakuwa tayari kufanya hivyo.

 “Tulishasema kwamba kwa ngazi zozote hata ngazi za udiwani au ubunge hatusubiri mabaki, makapi yatakayotokea CCM ndiyo yaje kwetu,” alisema Dk Slaa katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam.

“Safari hii hatusubiri. Tulishasema kuwa wagombea wetu tunawaandaa mapema ili tusitegemee mtu anayekuja dakika za mwisho kuwa ndiyo atuokoe.”

Kauli ya Dk Slaa inaweka msisitizo katika ile iliyowahi kutolewa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kwamba hawatapokea wanasiasa watakaoihama CCM ili kupata nafasi za uongozi kwa tiketi ya Chadema.

Katika mahojiano hayo, Dk Slaa alisema: “Huwezi kuzuia kupokea mwanachama kokote alikotokea, lakini unapofika wakati wa kuweka watu katika nafasi, lazima ufikirie.”

Mwaka 2010, Chadema ilipokea wagombea wawili walioshindwa kwenye kura za maoni za CCM, John Shibuda aliyeshindwa katika kura za maoni za Maswa Magharibi na Freddy Mpendazoe ambaye alienguliwa kwenye kura za maoni za CCM Jimbo la Segerea.

Shibuda alifanikiwa kurudi bungeni baada ya kushinda uchaguzi wakati Mpendazoe alishindwa katika hali ya kutatanisha na juhudi zake za kutengua matokeo hayo mahakamani ziligonga mwamba.

“Tatizo hilo lilitokana na ugeni wetu,” alisema Dk Slaa akizungumzia kitendo cha Chadema kupokea wagombea walioshindwa CCM kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

“Lakini kwa wakati huu, Chadema ina wanachama wengi wenye sifa za kugombea hivyo hatuhitaji kusubiri mtu,” aliongea katibu huyo mkuu ambaye aliwahi kutangaza kuwa nafasi za wagombea ubunge wa Chadema katika majimbo yote nchini zitatangazwa kwenye magazeti na watakaojitokeza, watafanyiwa usaili.

Kuhusu uchaguzi mkuu wa chama hicho, Dk Slaa alisema utafanyika Desemba mwaka huu baada ya kuridhiwa na kikao cha Kamati Kuu kitakachofanyika Julai 18.

Alisema wanahakikisha uongozi unapatikana kuanzia ngazi za chini na watachukua hatua kwa maeneo ambayo watabaini viongozi wamepeana nyadhifa bila chaguzi madhubuti kufanyika.

No comments:

Post a Comment