Kyerwa. Wananchi wanaopata
huduma za afya katika kituo cha afya Murongo wilayani Kyerwa mkoani
Kagera, wameuomba uongozi wa kituo hicho kujenga chumba cha kuhifadhia
maiti ili kuwaondolea adha wananchi wanayokumbana nayo baada ya
kushuhudia maiti zikilazwa kwenye vitanda vya wagonjwa.
Wakizungumza na gazeti hili jana, wananchi hao
walisema kuwa kutokana na kituo hicho kutokuwa na chumba cha kuhifadhia
maiti wameiomba bodi ya afya ili kusaidia ujenzi wa chumba cha
kuhifadhia maiti, kuondoa adha wanayokumbana nayo ya kushuhudia maiti
zikilazwa kwenye vitanda vya wagonjwa.
Mmoja wa wananchi hao, Sebastiani Katunzi alisema
wanapopata msiba katika hospitali hiyo wanakumbana na changamoto nyingi,
kwani maiti zinalazwa kwenye vitanda vya wagonjwa jambo linalowatia
wasiwasi wagonjwa waliopo wodini.
“Tumeiomba bodi ya afya wilayani hapa isaidie
kujenga chumba cha kuhifadhia maiti, kwani watu tunapopata misiba
tunakuwa na wasiwasi, kwani tunashuhudia maiti zikilazwa kwenye vitanda
vya wagonjwa jambo ambalo siyo jema,” alisema Katunzi
Mganga Mkuu wa kituo hicho, Alobogasti
Nkabyemanyira alisema kituo hicho cha afya Morongo tangu kianzishwe
wagonjwa waliokuwa wanalazwa walikuwa ni wachache, hivyo ingetokea
mgonjwa akafariki alikuwa anasafirishwa siku hiyo.
Nkabyemanyira alikiri kuwapo kwa tatizo hilo la
kutokuwa na chumba cha kuhifadhia maiti na kueleza kwamba wagonjwa
wameongezeka kiasi kikubwa na kusababisha kuwapo kwa upungufu wa
vitanda pia.
“Ni kweli kuna tatizo, lakini tutawasilina na
uongozi wa wilaya ili bajeti ya mwaka ujao iweze kukidhi mahitaji kama
hayo,” alisema Dk Nkabyemanyira.
No comments:
Post a Comment