Zambi: Serikali mbili ni maagizo ya JK

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi. 


Mbeya. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi amefichua sababu za chama hicho kushikilia msimamo wa muundo wa serikali mbili katika mjadala wa Katiba Mpya, akisema ni “maagizo ya mwenyekiti wa CCM”.

Mjadala wa Katiba Mpya ulikumbwa na mtikisiko baada ya Rais Jakaya Kikwete kueleza kitu alichokiita maoni yake binafsi wakati akizindua Bunge la Katiba kwa kueleza kuwa angependa muundo wa Muungano wa serikali mbili tofauti na Rasimu ya Katiba iliyopendekeza serikali tatu.

Mjadala huo ulivurugika kabisa baada ya kundi la wajumbe kutoka vyama vya upinzani waliounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia vikao likidai mjadala umepoteza mwelekeo kwa kuweka kando maoni ya wananchi ya kutaka muundo wa serikali tatu.

Akifungua mkutano wa Baraza la Utendaji la Umoja wa Vijana wa CCM wa Mkoa wa Mbeya juzi jioni, Zambi alisema mwenyekiti wa CCM alishawaambia kwamba msimamo wa chama ni kuhakikisha zinabaki serikali mbili kwenye Katiba Mpya.

 ‘’Vijana sasa lazima niwaeleze ukweli kuhusu muundo wa serikali, ni kwamba piga ua, CCM inataka kuimarisha muundo wa serikali mbili na hili ni agizo la mwenyekiti wetu Rais Jakaya Kikwete,” alisema huku akishangiliwa.

Alisema suala la Muungano ni maelewano na kwamba baadhi ya shughuli muhimu za Zanzibar zimehamishiwa Bara wakati nyingine za Bara zimehamishiwa Zanzibar.

 Hata hivyo, alisema kero iliyopo kwa sasa kwenye Muungano huo ni namna ya kugawana mapato makubwa ambayo alisema Serikali inaendelea kuyafanyia kazi.

 “Rais Kikwete katika kutueleza msimamo wa chama, pia alifafanua vizuri suala la serikali tatu kuongeza gharama za uendeshaji, jambo ambalo hata mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba aliliona, ingawa alifafanua kwamba halina namna,” alisema.

 Zambi, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, alisema anamshangaa Mwenyekiti wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe anapotamka kwamba serikali tatu ni lazima.

“Vijana wote na wanaCCM mkoani Mbeya naomba muelewe kwamba sisi chini ya mwenyekiti wetu wa CCM, Rais Kikwete, tumeamua muundo wa serikali mbili tu,” alisema.

Alisisitiza kwamba kama wachache hawataafiki msimamo huo kwa busara, Serikali ya CCM itaendelea na katiba iliyopo.

Akieleza sababu za msimamo wake wa serikali mbili wakati akizindua Bunge la Katiba, Rais Kikwete alizungumzia gharama za uendeshaji wa serikali tatu akisema katika muundo wa serikali tatu, Serikali ya Muungano haitakuwa na vyanzo vya uhakika vya fedha na kwamba hilo linaweza kusababisha kushindwa kulipa mishahara kama ya wanajeshi na hivyo kusababisha chombo hicho cha dola kuchukua serikali

Awali kabla ya kuanza kwa Bunge la Katiba, kulikuwa na habari kwamba CCM imesambaza waraka wa kutaka wabunge wake wapigie debe muundo wa serikali mbili na baadaye Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema chama hicho kina masilahi na muundo huo.

Ukawa imegoma kurudi kwenye Bunge la Katiba ikidai kuwa itafanya hivyo tu ikiwa kutakuwepo makubaliano ya kuheshimu maoni ya wananchi kama yalivyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na siyo kuingiza maoni mapya.

Kauli ya Zambi imekuja wakati mmoja wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, akisema anamshangaa Rais Kikwete kwa kuiponda rasimu wakati alikuwa anapewa taarifa katika kila hatua waliyokuwa wakifikia. Hivi karibuni, mmoja wa wajumbe hao, Dk Salim Ahmed Salim alinukuliwa na gazeti hili akisema kuwa Tume ya Katiba ilikuwa ikimpatia Rais taarifa za kila hatua zilizokuwa zikifanyika.

Naye Katibu Mkuu wa Chadema, Willibrod Slaa akihojiwa na gazeti hili mwishoni mwa wiki alisisitiza kwamba mwenye rungu la kutengua  utata wa Katiba Mpya ni Rais Jakaya Kikwete.

Awali, Katika hotuba yake, Zambi pia alizungumzia hali ya kisiasa mkoani Mbeya akisema CCM imeanza kupata nguvu baada ya wananchi kuelewa ukweli kwamba maisha bora hayatakuja kwa watu ‘wanaocheza pool, wanaoshinda baa wala wavivu’.

Pia aliwataka vijana mkoani  hapa kuacha kushabikia mabadiliko ya vyama vya siasa akisisitiza kuzichunguza nchi za Malawi, Zambia na Kenya kujua wananchi wamefaidikaje kimaisha baada ya kubadilisha vyama vya siasa mara kadhaa.

“Nasisitiza, hakuna Serikali itakayowanunulia nguo watu wake, itakayowalisha watu wote bure au kuwapatia viatu  watu wasiofanya kazi yoyote. Kazi ya Serikali ni kuboresha huduma za jamii,” alisema.

Kuhusu hali ya chakula nchini, alisema wakulima watavuna karibu tani milioni 15 wakati mahitaji ya Watanzania ni tani milioni 12 za nafaka. Mwaka jana zilivunwa tani 14 milioni.

No comments:

Post a Comment