Tanzania kupoteza Sh1.6 trilioni za gesi

“Kuvuja kwa mkataba huu kumesaidia kuona ukweli wa matamko ya viongozi kuhusu namna gani Tanzania itafaidika na utajiri wake wa gesi,” alisema Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe. 


Dar es Salaam. Wakati Tanzania inaelezwa itapoteza zaidi ya Sh1.6 trilioni kila mwaka kwa mujibu wa mkataba unaoonyesha mgawanyo wa mapato yatokanayo na gesi asilia (PSA), Serikali imeutetea ikisema unalinufaisha Taifa.

Mkataba huo uliovuja mitandaoni, unaonyesha kuwa Tanzania haitanufaika na rasilimali hiyo iliyogundulika Bahari ya Hindi, badala yake wawekezaji kutoka kampuni mbili ya Statoil ya Norway na ExconnMobil ya Marekani ndio watakaopata faida zaidi.

Kuvuja kwa mkataba huo kumekuja katika kipindi ambacho ugunduzi wa gesi hiyo asilia inayokadiriwa kufikia futi za ujazo trilioni 50 (trillion cubic feet)

hadi sasa, umekuwa kete muhimu kwa wanasiasa ambao wamekuwa wakiwatia moyo wananchi kuwa maliasili hiyo itakuwa na ahueni kubwa kimaisha.

Hata hivyo, baada ya mkataba huo kuvuja, hali imegeuka.

“Kuvuja kwa mkataba huu kumesaidia kuona ukweli wa matamko ya viongozi kuhusu namna gani Tanzania itafaidika na utajiri wake wa gesi,” alisema Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe.

Katika taarifa yake kwa gazeti hili, Zitto alisema mkataba huo unaonyesha kuwa makubaliano ambayo Serikali imeingia na wawekezaji hao yanaenda kinyume na mfano wa mkataba unaotakiwa kusainiwa (Model PSA).

Alisema kwa uchambuzi alioufanya kulingana na viwango vya mgawo wa mapato kati ya Model PSA na mkataba halisi, amebaini kwamba Tanzania itapata mgawo kidogo sana kinyume na ulivyopaswa kuwa.

Akimnukuu mwandishi wa jarida la African Arguments, Ben Taylor, Zitto alisema kiwango cha mapato ambacho kampuni ya Norway itapata ndani ya miaka 15 ya uzalishaji wa gesi, kitakuwa sawa na misaada yote ambayo nchi hiyo imeisaidia Tanzania tangu mwaka 1961.

Tangu Tanzania ipate uhuru, Norway imetoa misaada yenye thamani ya Dola 2.5 bilioni, wakati kwa mkataba huu na kampuni ambayo inamilikiwa na Serikali ya Norway, kwa miaka 15 watapata Dola 5.6 bilioni.

“Kwa hesabu hii, Norway itakuwa imerudisha misaada yake yote mara mbili zaidi ndani ya miaka saba tu huku Watanzania wenye rasilimali hiyo wakiwa hawanufaiki kabisa,” alisema Zitto ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).

“Mwanzoni, wengi tulidhani kuwa tatizo la mkataba huu ni eneo la umiliki wa kampuni tu (shareholding) kulingana na namna ulivyowasilishwa, kumbe mgawanyo mzima wa mapato unakwenda kinyume na maelezo ya Serikali na TPDC kwa umma.”

Zitto alifafanua kuwa kuvuja kwa mkataba huo kumesaidia kuona ukweli wa matamko ya viongozi ambao wamekuwa wakieleza jinsi Tanzania itakavyofaidika na utajiri wake wa gesi, ambayo ilizua tafrani mkoani Mtwara baada ya wananchi kufanya fujo wakishinikiza maliasili hiyo isisafirishwe nje ya mkoa huo.

Alisema sasa ni wakati mwafaka kwa Watanzania kuona mikataba yote ya gesi na mafuta ambayo Serikali imeingia na wawekezaji.

“Kama kwa mkataba huu mmoja tu, Taifa litapoteza trilioni za fedha kiasi hiki, hali ikoje kwa hiyo mikataba mingine 29?” alihoji Zitto.

Aliitaka Serikali ieleze ni hatua gani inachukua kurekebisha mkataba huu, pia wawekezaji hao waeleze watachukua hatua gani kuhakikisha wanaacha unyonyaji huu.

Hata hivyo, mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petrol (TPDC), Yona Kilaghane aliutetea mkataba huo akisema unalinufaisha taifa zaidi kuliko mwekezaji na hilo ndilo lilikuwa lengo kuu hata kabla ya kutiliana saini.

Kilaghane alisema watu wanaodhani mwekezaji ndiye anayenufaika, hawajui jinsi gani mkataba huo utakavyofanya kazi na kiasi gani cha fedha Taifa litapata.

“Ninao mkataba huo ofisini kwangu, ukihitaji kuujua njoo siku ya Jumanne nitakuonyesha na kukueleza jinsi tutakavyonufaika na rasilimali zetu,” alisema.

Alisisitiza kuwa manufaa kwa Taifa ni makubwa na yanazingatiwa kabla ya kusaini mkataba wowote.

Wakati Kilaghane akisema hivyo, juhudi za kuwapata wawekezaji hao kuzungumzia mkataba huo jana hazikufanikiwa.

 

No comments:

Post a Comment