Mugabe agusia uchaguzi wa mapema


Rais Robert Mugabe

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe amewasilisha Mahakamani pendekezo la kuifanyia kura ya maamuzi Katiba mpya mwezi Novemba kabla ya Uchaguzi wa Urais na Ubunge kufuatia baadaye mwezi Machi mwaka ujao.

Licha ya Kielelezo cha Katiba kuidhinishwa, viongozi wenye misimamo mikali katika chama cha Mugabe cha ZANU-PF wanapinga baadhi ya vifungu ikiwemo kile kinachopunguza uwezo wa rais.

 

Msemaji wa chama kikuu cha upinzani MDC, Douglas Mwonzora, amesema tarehe zilizopendekezwa na Mugabe haziwezi kuafikiwa na kwamba ZANU-PF inahitaji kubadili misimamo yake ili kuepuka ghasia kama zilizokumba Uchaguzi mkuu wa mwaka 2008.

Pande hizo mbili zimekosa kuafikiana juu ya kielelezo cha katiba mpya ambacho kinapaswa kupitisha kabla ya uchaguzi mpya kufanyika.

Hadi kufikia sasa , Rais Mugabe, 88,mwenye umri wa miaka 88, amekuwa akisisitiza kuwa uchaguzi ufanyike mwishoni mwa mwaka huu.

Chama cha MDC, kikiongozwa na Waziri Mkuu, Morgan Tsvangirai,akiungwa mkono na wapatanishi wa Afrika Kusini, kinasisitiza kuwa katiba mpya iwe tayari kabla ya uchaguzi kuhakikisha unafanyika kwa mazingira huru na ya haki.

Rais Mubage ambaye amekuwa mamlakani tangu mwaka 1980, anakana madai kuwa uchaguzi uliopita ulikumbwa na wizi wa kura kwa manufaa yake.

Bwana Tsvangirai alijiondoa kwenye kinyang'anyiro cha urais mwaka 2008, akilalamika kuwepo mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya wafuasi wake na jeshi la serikali pamoja na wafuasi wa Mugabe.

No comments:

Post a Comment