Malema azuiwa kuhutubia wachimba migodi
Mwanasiasa tatanishi nchini Afrika Kusini Julius
Malema amezuiwa kuwahutubia wafanyakazi wa migodini wanaogoma katika
mgodi wa Marikana.
Takriban wachimba migodi 2,000, walikusanyika
katika uwanja mmoja ulioko karibu na mgodi huo Kaskazini Magharibi mwa
Johannesburg kumsikiliza Malema.
Migomo ya wachimba migodi ambayo
inakumba nchi hiyo tayari imeathiri uzalishaji wa madini ya dhahabu na
Platinum katika nchi hiyo ambayo ina utajiri mkubwa wa maliasili.
Rais Jacob Zuma amesema kuwa hatua ya wachimba migodi imesababisha hasara ya karibu dola milioni 548 kwa sekta ya madini.
Akiongea kabla ya kongamano la vyama vya
wafanyakazi nchini humo, (Cosatu) Zuma alisema kuwa migomo ya mwaka huu
imekosesha hazina ya fedha dola milioni 388.
Wiki jana serikali ilisema kuwa itachukua hatua
za dharura dhidi ya wale wanaochochea fujo na hivyo kuisababishia sekta
ya madini mamilioni ya hasara.
Baada ya kutofautiana na polisi waliokuwa
wanalinda uwanja huo, Malema alisindikizwa na kikosi maalum cha polisi
hadi mbali sana na uwanja huo. Magari mawili ya polisi yenye silaha
yalifuata gari la Malema na juu angani kukawa na helikopta iliyokuwa
inamfuata pia.
Ametoa wito wa maandamano ya kitaifa baada ya hapo awali, kusema kuwa shughuli za migodi lazima zitatizwe.
Malema amekosolewa na wengi ambao wanamuona kama
mwenye njama ya kutumia masaibu ya wafanyakazi wa migodini kujinufaisha
kisiasa hasa baada ya wachimba migodi 34 kuuawa na polisi wakati wa
mgomo wao katika mgodi wa Marikana mwei jana.
No comments:
Post a Comment