Makahaba wagonganisha ma-RPC Dar
MAKAMANDA
wawili wa polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam, wamekwaruzana.
Makamanda hao, Charles Kenyela wa Mkoa wa Kinondoni na Kamanda wa
Polisi, Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo, wamekwaruzana na kurushiana
maneno yasiyofaa kuhusu namna ya utendaji kazi wa Jeshi la Polisi.
Kutofautiana huko kumeibuka baada ya wiki iliyopita, Kamanda
Kenyela kufanya operesheni ya kuwakamata wanawake wanaofanya biashara ya
ukahaba, maarufu kama machangudoa na kuwafikisha kwenye vyombo vya
sheria.
Baada ya Kamanda Kenyela kuendesha operesheni hiyo,
Kamanda Kiondo wa Temeke, alinukuliwa na vyombo vya habari jana,
akikosoa zoezi hilo na kusema hakuna sheria nchini inayozuia mwanamke
kujiuza.
Katika maelezo yake, Kamanda Kiondo alisema, operesheni
hiyo ilifanywa kwa kukurupuka na kwamba kamanda huyo hajasomea elimu ya
jamii juu ya madanguro.
Kwa mujibu wa Kamanda Kiondo, kama
Kamanda Kenyela angekuwa anaielewa vizuri elimu hiyo, kamwe
asingedhubutu kuwakamata wanawake hao bali angewapatia elimu na ushauri
dhidi ya maradhi wanayoweza kuambukizwa.
Pamoja na hayo, alihoji
kuna umuhimu gani wa kuwakamata machangudoa wakati hakuna sheria
inayomtaka awafikishe mahakamani badala yake anayetakiwa kushitakiwa ni
mtu anayetoa nyumba ili itumike kama danguro.
Naye, Kamanda
Kenyela alipozungumza na MTANZANIA jana juu ya kauli za kejeli
zilizotolewa na mwenzake huyo, alisema amestushwa na taarifa ya Kamanda
Kiondo kwa kuwa amemdhalilisha kupitia vyombo vya habari.
“Yaani
mwandishi sipati picha kama Kamanda Kiondo ambaye hana miezi sita kwenye
nafasi hiyo tangu ateuliwe, anaweza kunidhalilisha juu ya utendaji
wangu wa kazi, kwanza inakuwaje azungumzie mambo ya Kinondoni wakati
mimi nipo?
“Kama alijua nimekosea, alipaswa kunipigia simu kwanza
tushauriane kabla ya kusema kwenye vyombo vya habari au angenisema kwa
wakubwa wetu ambao wangeniita na kunishauri ili nisitishe operesheni
hiyo, kama kweli ninakwenda kinyume.
“Amenidhalilisha sana na
unajua ni vigumu kwa kamanda kama yule kutoka kwenye himaya yake na
kuzungumzia himaya ya kamanda mwingine wakati mhusika yupo.
“Kibaya
zaidi anasema eti mimi sina elimu ya jamii juu ya madanguro, lakini
binafsi siwezi kuona vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani au
usumbufu kwa raia wengine, halafu nikakaa kimya, sitaacha kuchukua
hatua.
“Ninachoweza kumwambia Kamanda Kiondo ni kwamba, sina
ugomvi naye na pia sitaki malumbano naye, kazi ya kudhibiti uhalifu
haihitaji mpango mmoja lazima tutumie njia mbadala kuhakikisha
tunatimiza majukumu yetu ya kulinda raia na mali zao, nafikiri suala
hilo linazungumzika tuache litapata suluhisho,” alisema Kamanda Kenyela
akionyesha kukerwa na kauli za Kamanda Kiondo.
Kova aingilia kati
Kutokana na malumbano hayo,
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova,
aliliambia MTANZANIA kwa simu kwamba atawakutanisha makamanda wa polisi
Kanda Maalum ya Dar es Salaam ili kupata ufumbuzi wa suala hilo.
“Ni
kweli suala hili limenifikia na kwa kuwa kesho (leo) kuna kikao, basi
litawekwa katika ajenda ili lipate kuondoa malumbano hayo.
“Lazima
tuangalie sheria zinasemaje juu ya machangudoa, sasa tutajadiliana ili
kupata msimamo wa kudhibiti biashara hiyo, kwani kuna matukio mengi ya
namna hiyo yapo yanafanyika lakini kwa upande wetu polisi lazima tuwe na
sheria ya kudhibiti vitendo hivyo.
“Kikao cha kesho (leo)
kitaangalia sana sheria kuliko maoni ya watu, tutaangalia upande wa
mahakama kama sheria zipo za kuwatia hatiani wahusika wa biashara hiyo,
nakuhakikishia tofauti hizi za ma RPC wawili zitakwisha na wote tutapata
msimamo wa pamoja.
“Si kwamba kikao cha kesho (leo) kimeitishwa
kwa sababu ya mzozo huo wa ma RPC hao, hapana, kilipangwa tangu siku
nyingi lakini tushukuru mzozo huu umeibuka wakati tunatarajia kukutana,”
alisema Kamanda Kova.
Kamanda Kiondo alipozungumza na MTANZANIA
kwa simu, alisema alitoa kauli hiyo baada ya kupigiwa simu na waandishi
wa habari wakitaka atoe ushauri juu ya operesheni inayofanywa na Kamanda
Kenyela.
“Nilichokifanya ni kutoa ushauri na uzoefu wangu
nilioupata wakati nikiwa masomoni nchini Afrika Kusini, ambako Serikali
ya nchi hiyo ilipambana kisheria na machangudoa lakini ikashindwa kwani
hata soko liliongezeka.
“Hata huku kwangu eneo la Sokota kuna
machangudoa na kila ninapojaribu kuwakamata, ndipo soko linapoongezeka.
Hivyo hivyo na gongo, ukiikamata inapanda bei.
“Kwa hiyo,
nilichokifanya mimi ni kutoa ushauri ili itolewe elimu kwa wanawake na
wanaume ili wajue madhara wanayoweza kupata pindi wanapojihusisha na
biashara hiyo.
“Sasa basi ninachosema hapa ni kwamba, nguvu ya
Kenyela haitaleta mafanikio bali itaongeza soko, kwani ukiwakamata
wahusika maana yake unawafanya waliobaki waongeze bei na pia ieleweke
kwamba, wanaokamatwa ni machangudoa wa Kinondoni tu wala siyo Dar es
Salaam nzima.
“Kwa hiyo, sina maana ya kutaka kumchafua Kamanda
Kenyela, niliyasema kwa nia nzuri kabisa, sina tatizo naye, naomba
anielewe hivyo,” alisema Kamanda Kiondo.
No comments:
Post a Comment