Msemaji wa Mkuu wa Polisi nchini, Advera Senso
George Njogopa
BOTI ya abiria iliyokuwa
ikitokea Pangani mkoani Tanga kwenda Zanzibar ikiwa na watu 32 juzi
usiku ilizama katika eneo la Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Zanzibar ambapo
watu 10 wanahofiwa kuwa wamepoteza maisha.
Taaarifa zilizofikia gazeti hili jana jioni
zilisema kati ya abiria 27 na wafanyakazi watano waliokuwa kwenye boti
hiyo, ni watu 20 tu waliokuwa wameokolewa wakati wengine 10 wakiwa
hawajulikani walipo.
Msemaji wa Mkuu wa Polisi nchini, Advera Senso
alisema jahazi liitwalo Sunrise liliondoka Tanga juzi saa 2:00 usiku
kuelekea Zanzibar, lakini lilipigwa na dhoruba katika eneo la Nungwi.
“Mpaka sasa watu 22 wameokolewa akiwamo
nahodha Abdallah Selemani, kumi wanatafutwa ijapokuwa wanahofiwa kuwa
wameishakufa. Kati ya hao ni watoto watatu na watu wazima ni
saba,”alisema Senso katika ujumbe alioutuma kupitia simu yake ya
mkononi.
Aliendelea: “Boti kutoka Tanga ipo kwenye eneo
la tukio kusaidia uokozi na wakazi wa Kaskazini Unguja wamepokea watu
waliookolewa na kuwapa huduma. Taarifa zaidi tunaendelea kufuatilia
Tanga na Zanzibar”.
Hata hivyo idadi ya watu waliookolewa kwa
mujibu wa Senso ilitofautiana na ile iliyokuwa imetolewa awali na
Kamanda wa Wanamaji na Bandarini Zanzibar, SP Martin Lisu aliyesema
juhudi za kuwaokoa abiria hao zilikuwa zikiendelea na kwamba waliokuwa
wamepatikana wakiwa hai ni watu 21.
Lisu alisema abiria hao
walionusurika kifo walipelekwa hospitalini kwa ajili ya kuchunguzwa afya
zao na wengine walipatiwa huduma za kwanza kutokana na mshtuko
walioupata.
“Kusema kweli tulifanikuwa kuwaokoa abiria 21
na wengine siwezi kusema kama wamezama ila nachoweza kusema ni kwamba
bado hatujawapata,” alisema Kamanda Lisu na kuongeza:
“Taarifa
nilizonazo ni kwamba, hii boti ilikuwa ikitokea Pangani, ilipofika eneo
la Nungwi ikakubwa na dhoruba kali na kisha kuanza kupoteza mwelekeo”.
Eneo la Nungwi
Eneo
la Nugwi lina historia ya kusababisha ajali za mara kwa mara na mara ya
mwisho ndiko ilitokea ajali ya meli ya MV Spice Islander iliyosababisha
vifo vya zaidi ya watu 400 mwaka 2011.
Ajali hiyo ilielezwa kusababishwa na uzembe wa
baadhi ya watendaji ikiwemo kukosekana kwa ukaguzi kabla ya meli hiyo
kuondoka.Taarifa zilizema kuwa meli hiyo ilizidisha idadi ya abiria na
mizigo hivyo ilipofika eneo la Nungwi ilizidiwa na kuanza kuzama.
Katika kujaribu kusaka ukweli wa mambo, Rais
wa Zanzibar, Dk Ally Mohamed Shein aliunda tume maalumu kuchunguza
mazingira yaliyosababisha ajili hiyo.
Ripoti ya tume hiyo ilifichua
uzembe uliojitokeza kwenye mamlaka husika na kupendekeza hatua kadhaa
ili kuimarisha hali ya usafiri kwenye maji.
Ajali nyingine kubwa ni ya meli ya MV Skagit
iliyotokea mwaka jana ikiwa inakaribia katika bandari ya Zanzibar,
ambayo hatua za awali za uokoaji zilishindikana na kusababisha vifo vya
mamia ya watu.
No comments:
Post a Comment