Mboye
SAKATA la gesi limetua rasmi bungeni baada ya
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe kuitaka Serikali iweke
hadharani mikataba ya utengenezaji wa bomba la kusafirishia gesi hiyo
kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam ili kuondoa usiri uliogubika mradi
huo.
Mbowe alitoa wito huo jana alipokuwa akimuuliza Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda maswali bungeni katika kipindi cha Maswali na Majibu kwa
Waziri Mkuu.
“Mheshimiwa Waziri ni dhahiri kuwa vurugu
za Lindi na Mtwara zimesababishwa na mawasiliano hafifu kati ya Serikali
na wananchi, ikiwamo kauli za viongozi wa Serikali na CCM je, ni kwa
nini Serikali isiwachukulie hatua za uwajibikaji watumishi wa Serikali
na vyombo vya ulinzi na usalama ambao wanaonekana dhahiri kuhusika,”
alihoji Mbowe.
Kiongozi huyo wa upinzani alimtaka Waziri Mkuu
kueleza ni kwa nini Serikali isiweke wazi mikataba yote ya gesi ili
kuondoa hofu iliyojengeka kwa wananchi kwamba kumekuwa na hali ya
ufisadi.
Akijibu swali hilo, Pinda aliwataka wabunge
kutumia utaratibu mzuri wa kupata mikataba hiyo akisema haiwezekani
ikawekwa hadharani.
Mbali na jibu hilo, Pinda alivitupia lawama vyama vya siasa akisema vimechangia kwa kiasi kikubwa mgogoro wa gesi mkoani Mtwara.
Licha ya juzi kueleza kuwa kulikuwa na
mgogoro wa viongozi ndani ya mkoa huo pamoja na CCM, jana alikwepa swali
la kutaka wahusika wawajibike na badala yake akasema suala hilo liko
juu yake.
Alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali lingine
la Mbowe ambaye alimtaka Pinda kutoa kauli juu ya nani aliyesababisha
mgogoro wa Mtwara uliosababisha maafa.
Hata hivyo, alitangaza neema kwa waathirika
kwamba Serikali inaangalia namna ya kuwapunguzia gharama wale wote
waliopatwa na matatizo hayo ikiwamo kuwalipa fidia.
“Vyama vya siasa
vimechangia kwa kiasi kikubwa katika kupotosha jambo hilo, ushindani wa
chaguzi zinazokuja umejitokeza pia,” alijibu Pinda.
Kiongozi huyo alisema wanaofanya uchochezi huo
wanafanya bila ya kujua kwamba unaweza kuwakumba watu wote wakiwamo hao
wanaofanya hivyo.
“Tutalaumiana wengi lakini ni vyema kuweka mambo
hadharani na kwamba ni hatari kufanya mambo kama hayo kwani amani ya
nchi ni lulu ambayo ikipotea inaweza kuwa tabu kuipata.”
Alipinga hoja ya Mbowe kuwa Serikali inatekeleza majukumu yake baada ya shinikizo na maandamano ya wanasiasa.
Alilieleza Bunge kuwa wananchi wa Mtwara wanaweza
kupoteza fursa nyingi kutokana na wawekezaji kuanza kuondoka wakikwepa
vurugu na kukimbilia Msumbiji ambako kuna dalili za gesi pia.
Kamati ya Makinda yayeyuka
Jana, Spika wa
Bunge Anne Makinda aliliambia Bunge kuwa Kamati aliyotarajia kuiunda
haitakuwapo kutokana na ukweli waliokuwa wakiutaka kutoka Mtwara
kuelezwa na Waziri Mkuu.
Akiahirisha Bunge mchana wa Januari 29, mwaka huu, Makinda
alitangaza kuwa angeunda kamati ya Bunge kwenda Mtwara kuangalia mgogoro
huo.
“Kutokana na ukweli uliotolewa na Waziri Mkuu leo bungeni,
naomba nimshukuru sana kwa dhati kwa kulishughulikia tatizo la Mtwara,
lakini nieleze kuwa nilikusudia kuunda tume kwa ajili ya kwenda kutazama
suala hilo, lakini tayari tumepata ukweli hivyo naona haina haja ya
kuunda tume hiyo,” alitangaza Makinda.
Moto bungeni
Hoja
binafsi ya Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia inayokosoa mfumo wa elimu
Tanzania kwa shule za msingi na sekondari kuwa ni dhaifu na hauleti
matumaini kwa wanafunzi, ilizua mjadala mzito bungeni jana baada ya
Serikali kukataa pendekezo lake la kuunda kamati maalumu ya kutafuta
chanzo cha tatizo hilo.
“Kutokana na hayo, ninaliomba Bunge lako
tukufu kuunda Kamati Teule ya Bunge kuchunguza kina cha udhaifu huo wa
kimfumo katika sekta ya elimu hapa nchini na kupendekeza hatua za
kuchukua ili taifa liondokane na aibu ya udhaifu huo,” alisema Mbatia.
Baada ya hoja hiyo, Waziri wa Elimu na Mafunzo
ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alipangua hoja moja baada ya nyingine na
kuliomba Bunge lisikubali kuundwa kwa kamati teule, bali liiagize
Serikali kushughulikia suala hilo.
Baada ya Dk Kawambwa kutoa hoja hiyo, Mbatia
alisimama na kuikataa akisema kile alichokiainisha juu ya udhaifu
hakifanani na kutaka kuundwa kamati kupitia kila hatua yenye udhaifu.
Baada ya Mbatia kusema hayo, ulizuka ubishi
baada ya Spika Makinda kutaka kujadiliwa kwa mabadiliko ambayo Serikali
inataka au hoja ya Mbatia iendelee.
Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Singida
Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alisema kuna kila sababu ya kuunda
kamati lakini iwe teule ya Bunge.
“Tunatakiwa tujadili kwanza hoja
iliyoko mezani na si kujadili mabadiliko ya hoja Mheshimiwa Spika, hoja
aliyotoa Mbatia isibadilishwe kwa kuwa ni kinyume na kanuni za Bunge
lako tukufu,” alisema Lissu.
Baadaye walisimama wabunge zaidi ya watatu
wakitaka kuchangia lakini Spika Makinda alitoa nafasi kwa Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi ambaye
alisema: “Tukiunda tume itachukua muda... Hoja iliyotolewa na Mbatia ni
ya msingi, sasa kamati za Spika zishirikiane na Wizara ya Elimu kufanya
kazi hiyo.”
Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekiah Wenje
alisema haiwezekani Bunge likakubali Serikali ijichunguze yenyewe kwa
kuwa ni kitu ambacho hakikubaliki na ni kinyume cha kanuni za Bunge.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka
(CCM) alisema kuna matatizo katika sera, mitalaa na muhtasari na kusema
sasa ni kazi ya Bunge kupata tume stahiki.
No comments:
Post a Comment