Rais wa Chama cha Madaktari nchini (MAT), Dk Namala Mkopi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jana imeshindwa
kuanza kuisikiliza kesi inayomkabili Rais wa Chama cha Madaktari nchini
(MAT), Dk Namala Mkopi, baada ya Wakili wa Serikali, Teophil Mutakyawa
kuomba muda wa kulipitia jalada.
Mutakyawa alidai jana ilikuwa ni siku ya
kusikiliza kesi hiyo lakini jalada lake lilikuwa halionekani, hivyo
aliomba apewe muda wa kulipitia. Hakimu Liwa alikubaliana na maelezo
hayo, na kuiahirisha kesi hiyo hadi Februari 21, mwaka huu.
Dk Mkopi anakabiliwa na mashtaka ya kupuuza amri
halali ya Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, iliyomtaka atangaze kusitishwa
kwa mgomo wa madaktari, kupitia vyombo vya habari.
Kesi hiyo kwa sasa inasikilizwa na Hakimu, Hellen
Liwa baada ya Hakimu aliyekuwa akiisikiliza awali, Chamshana
kuhamishiwa Bagamoyo.
Katika kesi hiyo, Dk Mkopi alipandishwa kizimbani
mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, Julai 10, 2012, na kusomewa mashtaka
mawili, ambapo Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Tumaini Kweka alidai
katika kosa la kwanza, mshtakiwa huyo alidharau amri ya Mahakama Kuu
Kitengo cha Kazi iliyomtaka kutangaza kupitia kwenye vyombo vya habari
kusitishwa kwa mgomo wa madaktari nchini kote.
Katika shtaka la pili, Wakili Kweka alidai
mshtakiwa huyo akiwa Rais wa Chama cha Madaktari aliwashawishi madaktari
kuendelea na mgomo wao kinyume cha amri ya Mahakama. Wakati akimsomea
maelezo ya awali, Desemba 27, 2012, Wakili Kweka alidai kuwa Juni, 2012,
madakatari wanaofanya kazi katika hospitali za umma waliingia katika
mgomo, na kwamba mgomo huo uliandaliwa na MAT.
Alidai katika mgomo huo madaktari hao waligoma
kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa na shughuli nyingine za kila siku,
ambazo ni sehemu ya mkataba wao na Serikali. “Kwa kuwa mgomo huo
ulikuwa ni batili, Serikali ilifungua maombi (namba 73 ya mwaka 2012),
Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, kwa Chama cha Madaktari,” alidai Wakili
Kweka na kuongeza:
“Katika maombi hayo, pamoja na mambo mengine
iliomba mahakama itoe zuio la muda kwa MAT na wanachama wake
kutokuitisha wala kushiriki katika mgomo, kusubiri uamuzi wa mgogoro
uliowasilishwa Mahakama Kuu na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA).
No comments:
Post a Comment