BEI ya unga wa sembe mkoani Dar es Salaam
inatarajia kupungua kutoka Sh1,500 hadi 900 kwa kilo kuanzia wiki hii
baada ya tani 3056 za mahindi kuanza kukobolewa.
Serikali ilitoa vibali kwa wenye vinu vya
usagishaji kuchukua mahindi kwenye maghala ya kitaifa kwa ajili ya
kupunguza makali ya bei za vyakula kupanda.
Mkoa wa Dar es Salaam ulipata mgao wa tani 6,400
kutoka wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika na hadi sasa tani 3056 za
mahindi zimetolewa kwa wafanyabiashara hao walioingia mkataba na
Serikali kuuza unga bei ya rejareja Sh900.
Akizungumza na gazeti hili
jana, Ofisa Kilimo Mwandamizi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Denis
Nyakisinda alisema tani hizo zimegawanywa katika wilaya tatu za mkoa huo
ambapo Kinondoni imepata tani 3,600 wakati Temeke na Ilala zimepata
tani 1,400 kila moja.
Alisema Wilaya ya Kinondoni imepewa tani nyingi
kwa sababu kuna mashine nyingi na kwamba Tandale na Manzese ndiyo
inayolisha Dar es Salaam.
“Kila aliyepewa mahindi amepewa mkataba wenye
maelekezo kwamba auze unga kwa bei ya Sh900 kwa kilo na tutafuatilia ili
kuona bei ya unga inashuka,” alisema Nyakisinda na kuongeza kuwa:
“Kuna baadhi ya maeneo kama ya Mbagala ambako kuna
wafanyabiashara walishachukua mahindi hivyo tunategemea bei ya unga
itapungua baada ya mahindi kuingia sokoni na kukobolewa,” alisema.
Alisema hadi sasa kuna wafanyabiashara 48 ambao
wamepewa vibali kwa ajili ya kwenda kununua mahindi hayo katika maeneo
ya Songea, Makambako na Mbozi na kwamba wafanyabishara hao ni wale wa
kati, wadogo na baadhi ya makampuni makubwa.
Alisema mchakato wa kuwapata wafanyabiashara hao
ulifanyika kwenye wilaya kwa kupitia kwa watendaji wa mitaa ambako
mashine zipo na kwamba baada ya hapo mkoa ulipokea majina na kuyatuma
Wakala wa Chakula (NFRA) kwa ajili ya kupewa vibali.
Kwa mujibu wa ofisa huyo, Songea zimetengwa tani
4200 ambapo wafanyabiashara watakaokwenda kuchukua huko watauziwa kwa
bei ya Sh460 kwa kilo wakati Mbozi zimetengwa tani 1800 na
wafanyabiashara watauziwa Sh490 kwa kilo na Makambako ziko tani 400
ambazo wafanyabiashara watauziwa Sh500 kwa kilo.
Alisema mfanyabiashara atakayekiuka mkataba
atachukuliwa hatua za kisheria kwani wamejipanga kufuatilia kwa kila
mfanyabiashara aliyepewa kibali na kwamba kila wanaposhusha mzigo lazima
wapige simu kwa maofisa kilimo wa maeneo husika.
No comments:
Post a Comment