Simanzi yatawala, Waziri azomewa
SIMANZI na vilio vilitawala mazishi ya Padri
Evarist Mushi yaliyofanyika Kitope Zanzibar jana huku Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud akipata wakati mgumu
baada ya kuzomewa na waombolezaji kutokana na kukerwa na hotuba yake.
Padri Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi,
Jumapili iliyopita wakati akijiandaa kwenda kuongoza misa katika Kanisa
la Mt. Joseph Minara Miwili mjini hapa.
Ibada ya mazishi iliyoongozwa
na Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali
Pengo ilianza saa nne asubuhi katika Kanisa la Mt. Joseph Minara Miwili
na kuhudhuriwa pia na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.
Baada ya misa hiyo iliyomalizika saa 6.30
mchana, msafara wa mazishi ulielekea Kitope yalipo makaburi ya viongozi
wa Kanisa Katoliki. Baada ya kufika makaburini, ibada ya mazishi ilianza
saa 7.30 mchana na mwili wa Padri uliwekwa kaburini saa moja baadaye.
Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni
pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif
Hamad, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi, Mwenyekiti wa NCCR
Mageuzi, James Mbatia na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa.
Kuzomewa
Waziri
Aboud alizomewa kutokana na kauli yake aliyotoa katika salamu za
Serikali kuwa kifo cha Padri Mushi ni kazi ya Mungu, ambayo haina
makosa.
“Serikali imepokea msiba huu kwa huzuni na
masikitiko makubwa. Maumivu ya familia ya marehemu ni maumivu ya
Serikali. Padri Mushi ametuachia pengo kubwa lakini kazi ya Mungu haina
makosa,” alisema Waziri Aboud kauli ambayo ilipokewa kwa waomboleza
kuguna wengine wakizomea hali iliyowafanya baadhi ya viongozi
kuwatuliza.
Mmoja wa waombolezaji alisikika akisema: “Kazi ya Mungu ndiyo imewatuma hao wahalifu kuua kwa risasi?”
Mwakilishi wa familia, Francis Mushi alijibu
kauli ya waziri huyo alipopewa nafasi ya kutoa salamu kwa kusema:
“Tumeupokea msiba huu kwa masikitiko makubwa hasa kwa kuwa Padri
hakuugua… Alikuwa kiungo kikubwa katika familia yetu.” Maneno ambayo
yaliibua simanzi na vilio kutoka kwa waombolezaji wengi.
Hata Askofu wa Jimbo Katoliki Zanzibar,
Augustino Shao aliyekuwa amekaa karibu na Rais Dk Shein alipopewa nafasi
naye alisema waziwazi: “Naomba kusema kuwa, kauli hii ya mapenzi ya
Mungu haipo… Hili ni suala la uovu na tusikubali kushindwa na uovu.”
Kauli hiyo ilionekana kuungwa mkono na waumini.
Ibada hiyo ilihitimishwa kwa sala iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Tanga, Antony Banzi.
Wanasiasa waomboleza
Akizungumza
baada ya kumalizika kwa msiba huo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod
Slaa alisema wananchi wamechoshwa na kauli za Serikali za kuwatuliza
huku watu wakiendelea kuuawa.
“Watanzania tusiendekeze kauli za Serikali za
kila siku, eti Bwana ametoa Bwana ametwaa! Kifo cha Padri Mushi
hakikutokana na ugonjwa wala Serikali, lakini haiwezekani kila siku
Serikali iendelee na ahadi za maneno matupu.
“Haiwezekani Katibu wa
Mufti, Fadhili Soraga ajeruhiwe kwa tindikali, Padri ajeruhiwe kwa
risasi, kule Geita mchungaji ameuawa na mwaka jana mwandishi wa habari
aliuawa na Jeshi la Polisi, tusidanganyane… tuseme ukweli,” alisema
Slaa.
Akizungumzia kauli ya Rais Jakaya Kikwete ya
kulitaka Jeshi la Polisi kushirikiana na vyombo vya nje katika
upelelezi, alisema: “Suluhisho siyo kuleta ‘Scotland Yard’ hapa, tatizo
letu tunashughulika na matawi wakati mzizi ukiwa bado haujakatwa.
Tung’oe mzizi wa tatizo.”
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia
alivilaumu vyombo vya usalama kwa kushindwa kudhibiti mauaji hayo na
kumtaka Rais Jakaya Kikwete kuwajibika kwa mauaji yanayoendelea nchini.
“Rais anapoingia madarakani anaapa kuwa mtiifu
kwa Katiba na raia wake, lakini haya matukio ya umwagaji damu yamekuwa
kawaida sasa. Damu ya mtu ni ya thamani huwezi kuinunua hata uwe
tajiri.”
“Vyombo vya usalama vinavyolipwa kwa kodi za wananchi vimeshindwa kazi. Kila siku wanasema hayatatokea, lakini yanatokea.”
Tamko la Rais Kikwete
Katika tamko lake
lililosomwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (Tec), Askofu
Anthony Makunde katika ibada ya asubuhi, Rais Kikwete ameliagiza Jeshi
la Polisi nchini kuwakamata mara moja wote waliohusika na mauaji hayo
ili kukata mzizi wa fitina.
“Nawahakikishia kuwa tuko pamoja katika msiba
huu ambao ni wetu sote. Nimeliagiza Jeshi la Polisi kukusanya nguvu zote
na kufanya uchunguzi wa kina na wa haraka. Nimewaagiza Polisi
kushirikiana na vyombo vya nje, ukweli wote ujulikane ili kukata mzizi
wa fitina,” ilisema taarifa ya Rais Kikwete.
Askofu Nzigirwa aomba upendo
Askofu
Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius
Nzigirwa amewataka waumini wa kanisa hilo kutokuwa hasira badala yake
wawaombee watu waliompiga risasi Padri Mushi ili watubu na kumrejea
Mungu kutokana na dhambi waliyoitenda.
Askofu Nzigirwa alisema hayo wakati akisoma
Ibada ya Misa kwa ajili ya kuomboleza kifo cha Padri Mushi na kuliombea
Taifa amani katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph, Jijini Dar es
Salaam jana.
Alisema waliotekeleza mauaji hayo ni maadui wa
Ukristo na walitenda hayo kwa kutumia nguvu za ibilisi... “Mungu
alitupa amri kuu ya kupendana,” alisema Askofu Nzigirwa: “Tusipendane
sisi wenyewe kwa wenyewe Wakristo tu, bali tuwapende na maadui zetu.”
Aliwasifu
waumini wa Kanisa Katoliki visiwani Zanzibar kwa kutotaka kulipiza
kisasi na kuwa na hekima katika tukio la kuuawa kwa Padri Mushi.
Alisema kuwa iwapo Wakatoliki wataona taifa la
Tanzania linakwenda mrama kutokana na matukio hayo ya uadui dhidi ya
Ukristo, wazidi kumuomba Mungu ili mapenzi yake yafanyike.
Askofu huyo alimtambulisha kwenye ibada hiyo,
Padri Ambrosi Mkenda ambaye alipigwa risasi mbili, kidevuni na mgongoni,
Desemba mwaka jana, akisema anaendelea vizuri kiafya.
Nyongeza na Leon Bahati
No comments:
Post a Comment