dhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh
(katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu
ripoti ya ukaguzi ya mwaka wa fedha ulioishia 30 Juni, 2012
zilizowasilishwa bungeni jana mjini Dodoma. Kushoto ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe na kulia ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Rajab
Mbarouk Mohammed.
Dodoma. Ripoti ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ilitolewa jana ikiweka bayana
madudu mbalimbali ya ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma, udhaifu katika
usimamizi wa mikataba na Serikali kushindwa kutoa fedha zilizoidhinishwa
na Bunge kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Moja ya matatizo yaliyojitokeza ni Wizara ya
Nishati na Madini kushindwa kukusanya nyongeza ya mrabaha wa madini
baada ya kuongezwa kutoka asilimia tatu hadi nne.
Akizungumza na
waandishi wa habari mara baada ya kuwasilisha ripoti hiyo ya mwaka wa
fedha unaoishia Juni 30, 2012, CAG Ludovick Utouh alisema pamoja na
kuwapo mafanikio ya kimahesabu ukilinganisha na miaka iliyopita, bado
kuna mambo ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi.
Alilishauri Bunge kuangalia upya suala la
kuivunja Kamati ya Hesabu ya Mashirika ya Umma (POAC) na kuunganisha
shughuli zake na Kamati ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC) na mkakati wa
ofisi kufanya ukaguzi wa misamaha ya kodi ambayo imeongezeka kuangalia
uhalali wake.
Hata hivyo, Utouh alikataa katakata kuzungumzia deni la taifa ambalo pia limeongezeka akisema “amefanya hivyo makusudi”.
Bajeti na miradi ya maendeleo
Kwa mujibu wa
CAG, imebainika kuwa kuna tatizo kubwa la Serikali kushindwa kutoa kwa
halmashauri mbalimbali fedha za maendeleo kama zilivyopitishwa na Bunge.
Alisema
Bunge lilipitisha vifungu vya fedha za maendeleo vyenye jumla ya
Sh595,064,422,505 katika halmashauri 113, lakini fedha zilizopokewa ni
Sh345,568,067,477 sawa na asilimia 42 tu, hivyo kufanya upungufu wa
Sh249,496,355,027.
Licha ya fedha hizo kutokutolewa zote, kiwango
kilichotolewa hakikutumika chote kutokana na kucheleweshwa. “Hadi
mwishoni mwa mwaka, kulikuwa na baki ya fedha za miradi ya maendeleo
kiasi cha Sh188,405,740,589 ambayo ni sawa na asilimia 55 ya fedha
zilizotolewa na Serikali,” alisema Otouh na kuongeza: “Tunashauri bajeti
iendane na shughuli zilizopangwa, kwa sasa utaratibu wa bajeti haujawa
mzuri.”
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hata fedha za Mfuko
wa Maendeleo ya Jimbo zinazotolewa kwa wabunge hazikutumika zote.
Sh2,561,882,820 zilizotengwa kwa ajili ya sampuli ya majimbo 69
zilibaki.
“Sababu ya kutokutumika ni ama halmashauri
hazina utaratibu maalumu wa kutumia fedha hizo au Serikali kutoa fedha
hizo mwishoni mwa mwaka,” alisema.
Udhaifu katika usimamizi wa mikataba ya madini
Katika
ripoti hiyo, CAG alisema Wizara ya Nishati na Madini ilishindwa
kukusanya Dola za Marekani 12,634,354 (sawa na Sh19,709,593,191)
zilizotokana na ongezeko la mirabaha ya madini, baada ya mabadiliko ya
Sheria ya Madini.
Katika iliyokuwa Wizara ya Miundombinu,
ukaguzi huo umebaini kuwa madeni yake ya mwaka 2010/11 yanayofikia Sh253
bilioni yamelipwa kwa kutumia fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya
ujenzi wa barabara mwaka uliofuata wa 2011/12.
Katika kipindi hicho, CAG alisema dhamana za
Serikali za jumla ya Sh578.4 bilioni zilikuwa zimeisha muda wake na
hivyo kuifanya Serikali ikiwa mdhamini kuwajibika kulipa deni hilo.
Vilevile, CAG ameona kuna kodi inayopotea
kutoka sekta isiyo rasmi, hivyo kuishauri Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) kuwatumia vizuri makatibu kata kuwatambua walipakodi kama vile
wamiliki wa kumbi za harusi na mikutano.
Alishauri kuwa TRA ianze kukusanya kodi kwenye huduma za
kuhamisha fedha kwa njia ya simu za kiganjani maarufu kama M-Pesa, Tigo
Pesa, Airtel Money na nyinginezo.
Alisema kampuni hizo zinatakiwa
kulipa kodi ya zuio ya malipo ya kamisheni inayolipwa kwa wanaofanya
biashara hiyo na kodi hiyo ipunguzwe kutoka katika kodi ya mwisho
itakayotakiwa kulipwa na kampuni za simu.
Misamaha ya kodi
Ripoti hiyo ya CAG
ilishauri mikataba ya madini ijadiliwe na Kamati ya Bunge inayohusika na
kutoa mapendekezo kabla haijasainiwa na hati za misamaha ya kodi
ziwekwe bayana kuwa ni msamaha wa muda gani, inaanza na kumalizika lini.
Alishauri
pia vipengele vyote vya misamaha ya kodi vipitiwe na Mwanasheria Mkuu
wa Serikali kwa ajili ya kushauri kabla ya kusainiwa na upande husika.
Katika mwaka 2013/14, CAG ameamua kuanza
kuikagua misamaha yote ya kodi kwa madhumuni ya kuangalia manufaa yake
kwa uchumi wa taifa, kwa kuwa misamaha hiyo pia ni fedha za Serikali.
Hesabu za TRA zimeonyesha makusanyo ya kiasi cha Sh6,703,229,704,887
ikilinganishwa na makadirio ya Sh6,456,832,630,000 na kusababisha
makusanyo ya ziada ya Sh 246,397,074,887 sawa na asilimia nne ya
makadirio.
Taarifa ya CAG inaonyesha mwelekeo wa misamaha
ya kodi unaonyesha ongezeko kwa kiasi cha Sh789,883,259,827 sawa na
asilimia 78 kutoka kiasi cha Sh1,016,320,300,000 kilichoripotiwa mwaka
2010/2011 hadi Sh1,806,203,559,827 kwa mwaka 2011/2012.
Kuvunjwa kwa POAC
Utouh alisema kitendo cha
kuvunjwa kwa POAC na kuunganisha majukumu yake na PAC ni bahati mbaya
kwa kuwa sababu za kuanzishwa kwake bado zipo hai kama ilivyokuwa wakati
inaanzishwa na kwamba uamuzi huo hautakidhi matarajio ya wadau.
“Kamati ya PAC itazidiwa na ukubwa wa
majukumu, hivyo ofisi bado inashauri kuona uwezekano wa kurudisha kamati
hii hata kama itakuwa na haja ya kubadilisha jina lake,” alisema.
Spika Anne Makinda aliamua kuvunja kamati zote za Bunge kwa kuunda mpya na kuvunja nyingine.
POAC
iliyokuwa chini ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
iliunganishwa na ile ya PAC, ambayo pia inaongozwa na mbunge huyo.
“Kamati
ya PAC itazidiwa na ukubwa wa majukumu, hivyo ofisi bado inashauri
kuona uwezekano wa kurudisha kamati hii hata kama itakuwa na haja ya
kubadilisha jina lake,”
No comments:
Post a Comment