Kufa kumeumbiwa kiumbe chochote kilicho hai.
Kama kilizaliwa basi siku moja kitakufa. Lini kitakufa hakuna ajuaye
labda yule aliyepanga mauaji ya kiumbe hicho na wakati mwingine hata
yeye muuaji anafikia hatua asifanikiwe katika azma yake hiyo. Kwa sisi
wenye imani za dini tunaamini kwamba Mungu alitupa ruhusa ya kutoa uhai
wa mimea na wanyama ili kujifanyia chakula. Wapo wanaoondoa baadhi ya
wanyama kwamba nao hawaruhusiwi kwa imani zao.
Pia wapo wale wanaoondoa wanyama wote na kubaki na
ruhusa ya kutoa uhai wa mimea tu. Katika wote hao sijasikia wanaosema
kwamba imani yao imewapa ruhusa ya kutoa roho za watu wengine. Hivyo
kila mwenye kuamini kwa imani yake anaamini kwamba mwenye haki na roho
ya binadamu ni yeye aliyemuumba yaani Mungu anayemwamini. Pamoja na
ukweli huo ambao bahati nzuri wengi wetu tunauamini bado wapo watu ambao
wao wanafikiria wamepata ruhusa ya kutoa roho za watu wengine.
Tuwaache wale wenye kupewa kazi ya kunyonga au
wanajeshi wanaokwenda vitani ambao hao mjadala wao ni tofauti na hawa
ninaowazungumzia. Mimi nazungumzia wale ambao kazi walizopewa ni
kuzifikisha roho za watu salama kule ziendako hapa duniani yaani
madereva wa mabasi ambayo yanasafirisha abiria. Watu hawa naona
wamesahau kwamba wana jukumu hilo. Ajali zinazotokana na magari ya
abiria zimekuwa nyingi mno na kwa asilimia kubwa utaambiwa chanzo ni
uzembe wa dereva. Hatuwezi kuendelea kuufumbia macho uzembe huu! Ni
lazima tufanye kitu kwa madereva hawa waliojiajiri kutoa roho za watu.
Dereva aliyekamilika yaani ni mtu mzima, hajalewa,
hana ugonjwa wa akili, kwa jumla anajitambua sawasawa na bila shaka
anajua kwamba roho ya binadamu ikitoka haina mbadala. Pia anajua kwamba
alichokibeba ndani ya gari hilo kina thamani kuliko vitu vyote ambavyo
Mungu ameviumba.
Haiwezekani kabisa kwa dereva kama huyo kuamini
kwamba fedha anazozisaka ni muhimu kuliko hao binadamu. Kwanza hata kama
anapenda fedha kuliko watu atapata wapi watu wa kumpatia hiyo fedha
kama yeye kazi yake ni kuwapunguza kila siku? Kwa sababu hiyo mimi
naamini kwamba hawa madereva wanaoendesha magari ya abiria ambao kila
kukicha tunawasikia kwa uzembe huu na ule uliosababisha maafa ya
kupoteza uhai wa watu, au kuwapatia vilema vya kudumu ni watu wenye
hitilafu fulani katika ubinadamu wao kama siyo akili zao.
Maana wewe unajua umebeba roho za watu ambazo
hazina mbadala lakini kichwani kwako unachofikiria ni fedha iliyoko
katika kituo kinachofuata kiasi kwamba hujali namna unavyoyapita magari
yaliyo mbele yako. Akili yako inakuwa imevurugukiwa kiasi kwamba hatari
ya kugongana uso kwa uso na gari iliyopo upande huo unaopita huifikirii
bali unachokiona ni fedha zilizopo kituo hicho unachokikimbilia.
Nasema huu ni uwazimu kwa sababu pamoja kwamba
tunasema binadamu anatakiwa kuthubutu ili apate anachohitaji lakini
kuthubutu huko huwa kunafanyika kwa mahesabu; yaani asilimia gani
umeweka ya kufanikiwa katika mkakati wako? Ukifanikiwa utapata nini?
Ukikosa utapoteza nini? Sasa katika hali ya
kawaida kabisa inaonesha kwamba uwezekano wa kufanikiwa kuyapita magari
yaliyo mbele yako bila kupata ajali ni mdogo. Kwa uwezekano huo mdogo
bado ni kwamba ukishindwa utapoteza maisha ya watu. Kweli unacheza
kamari ya uwezekano mdogo wa kufanikiwa na kupata vinauli dhidi ya
uwezekano mkubwa wa kushindwa na kupoteza maisha ya watu? Kama huko siko
kukosa hekima ni nini?
Mimi nafikiri wakati umefika sasa wa kupandisha
viwango vya watu wanaotaka leseni za udereva wa kubeba abiria. Kama vile
ilivyo kwa kazi nyingine nyeti kama usalama wa taifa basi na udereva
nao ungechukuliwa hivyo hivyo.
Watu wachunguzwe hata katika maisha yao ya
kawaida, namna wanavyoyapokea mambo mbalimbali yanayohusu jamii, namna
wanavyofanya uamuzi pale inapobidi wafanye uamuzi kati ya fedha au vitu
na watu na mengine. Vigezo hivyo wapewe wamiliki wa vyombo ili
kuhakikisha kwamba wanaajiri watu wanaojitambua katika kazi hizo.
Bila kufanya hivyo tutaendelea kuwa na madereva
hawa wasiojali, wasiojitambua, wasiokuwa na ubinadamu na ambao wameamua
kujiajiri kwenye kazi ya kunyonga watu.
Baada ya hapo sheria pia zirekebishwe kuhakikisha
kwamba anayefanya uzembe barabarani na kupoteza maisha ya watu basi
asikabidhiwe tena roho nyingine maana yake asiruhusiwe tena kuwa dereva
wa magari ya abiria.
Huyo mmiliki wa gari naye asijinasue kwenye mkono wa sheria
mpaka hapo atakapothibitisha kwamba yeye alitimiza sehemu yake kwa
kuajiri dereva mwenye viwango. Pia anampatia dereva wake huyo mwenye
viwango muda wa kupumzika kwa kuhakikisha kwamba haruhusu dereva huo
mwenye viwango kuendesha gari toka saa kumi asubuhi mpaka saa sita usiku
bila mapumziko.
Kama dereva hana viwango au kama mwajiri hajafanya
mpango wa dereva kupumzika kwa kumuwekea dereva mwingine kwa gari
linalohudumia zaidi ya muda wa kawaida wa kufanya kazi basi sheria
imgeukie mwajiri, naye asiruhusiwe kuhudumia umma katika biashara ya
kubeba abiria.
No comments:
Post a Comment