Rasimu ya Katiba imesheheni mambo mengi muhimu, yanayohitajika kwa
wakati tulionao. Ikiwa yatakosekana kupatikana mwakani, anaweza akatokea
rais mkorofi, asiyeambilika wala kushaurika akasema hana mpango wa
kuunda katiba mpya hadi miaka 50 mingine ipite na kuiona iliopo inafaa
na kukidhi haja.PICHA|MAKTABA
Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi
Sauti za viongozi wa kisiasa, kiserikali na
madhehebu ya dini kuwaasa na kuwasihi Ukawa warejee bungeni zimesikika,
kazi sasa ni kwa wajumbe wa kundi hilo kuitikia wito huo au kuziba
masikio.
Matamshi ya viongozi hao kwa nyakati tofauti,
yameeleza wazi na kuwataka wabunge hao kutengua misimamo yao na kurejea
bungeni ili kuchuana, kushindana kwa hoja na kukosoana wakiwa ndani ya
Bunge, si nje ya chombo hicho cha kikatiba na kisheria au kufanya
mikutano ya hadhara nchi nzima.
Viongozi hao kwa nyakati tofauti, wameeleza kuwa
itakuwa busara ikiwa upande wa wabunge waliobaki ndani ya Bunge na wale
waliotoka nje, wakakaa pamoja kwa kuzitumia kamati ya mashauriano,
iliyopo.
Miongoni mwa viongozi waliotoa wito wa kuwataka
Ukawa warejee bungeni ni Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais Dk Mohamed
Gharib Bilal, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar
Balozi Seif Ali Idd na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk
Hussein Mwinyi.
Wengine ni Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis
Mutungi, Askofu wa Kanisa la Katoliki Jimbo Iringa Tarcius Ngalalekumwa
na Mufti Mkuu wa Bakwata Sheikh Shaaban Bin Simba.
Hata hivyo Ukawa wameeleza kuwa wamelisusa Bunge
la Katiba, baada ya kujitokeza matusi, kejeli na maneno ya ubaguzi
kutoka kwa wajumbe wa CCM, ambao wanadaiwa kuwa waliacha kujadili hoja
za msingi na kuanza malumbano kinyume na dhamira ya kuundwa Bunge
maalumu la Katiba.
Pia wanaeleza na kutoa masharti kuwa Rasimu ya
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ijadiliwe kama ilivyo, isipunguzwe
kipengele wala kifungu chochote na kwamba ushauri au maoni ya Tume
yabaki vilevile kama yalivyo bila ya kutiwa mikono au kuchakachuliwa.
Madai haya ya Ukawa kwa upande mmoja yanaleta
mkanganyiko na kutia hofu. Kazi ya Bunge maalumu la Katiba ni kuipitia
rasimu, kuijadili, kuongeza au kupunguza yaliyomo kwa masilahi ya taifa
pale inapobidi, si kuwa muhuri wa kuidhinisha matakwa ya tume yatokanayo
na makamishna wao kwa kulitumia Bunge, kabla ya kuitishwa kura ya
maoni.
Pia Ukawa wanamtupia lawama Rais Kikwete na
kumtaja kuwa ndiye chimbuko la kuvurugika kwa mchakato huo, baada ya
kutoa maoni yake kama Mkuu wa Nchi.
Dai hili kwa maoni yangu naona kama limekosa nguvu
ya hoja kutokana na Rais kuwa na haki ya kutoa maoni kama ambavyo
makamishna wa Tume na Mwenyekiti wao walivyotoa.
Rais pia ana haki ya kutoa maoni yake kwa niaba ya
chombo anachokiongoza ambacho ni serikali na kwa niaba ya taifa akiwa
Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.
Anapotakiwa anyamaze, afumbe mdomo au aache mambo
yaende kama yanavyotakiwa na wengine, hapo atakuwa anapoteza sifa ya
kuitwa Rais wa Nchi na kiongozi wa Serikali.
Kama alivyosimama Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
Jaji Jopseph Warioba, Makamu Mwenyekiti wake Jaji Augustino Ramadhan na
makamishna wa tume hiyo na kushiriki makongamano, semina na warsha
nyingine kutetea msimamo wao, rais pia ana haki na wajibu wa kusimamia
lile analoliamini kwa niaba ya Serikali.
Madai kwamba Rais amevuruga mchakato wa katiba
hayana mashiko na yamekosa uzani wa kusimamia ukweli katika lengo la
kumlisha maneno au kumwambia amevuruga zoezi zima la kupatikana Katiba
Mpya kama inavyodaiwa na baadhi ya wanasiasa, wanataaluma na makala za
waandishi wa habari.
Sote tumeshuhudia jinsi Rais Kikwete
alivyoichambua Rasimu ya Katiba kitakwimu, hoja alizoziainisha, hofu
yake kuhusu vipengele alivyovitaja pia wasiwasi wake kama Mkuu wa Nchi
kuhusu suala la mabadiliko ya muundo wa Muungano na mabadiliko yake kama
inavyotarajiwa iwe kulingana na maoni ya Tume ya Katiba.
Kadhalika wakati mjadala ukianza na wabunge
kujadili sura ya kwanza hadi ya sita, pande zote mbili zilikuwa
zikitupiana vijembe, mipasho na wakati mwingine kutupiana maneno mazito
kinyume na uungwana wa demokrasia.
Madai ya kupatikana Katiba Mpya yamekuwa yakidaiwa
na kambi ya upinzani na baadhi ya wadau tangu mwaka 1992 kwa kuelezwa
kuwa Katiba ya mwaka 1977 haikidhi haja, imepitwa na wakati, ina
upungufu wa msingi na si ya kidemokrasia.
Malalamiko hayo yakazingatiwa na utawala wa awamu
ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete. Yamefanyika kwa weledi na utashi,
mambo yamewiva, yameonyesha njia na mwelekeo wa kutosha badala yake,
Wajumbe wa Ukawa wanatoka na kususia vikao.
Katika rasimu hiyo ya Katiba ukiangalia kwa kina
na undani, utajua na kubaini pande zote zinatakiwa kuacha kejeli na
mipasho, zijadili hoja, wanachokikataa au kukiafiki waonyeshe kama ni
kweli hawakitaki kwa sababu zipi na kuafiki kwa minajili gani badala ya
kuweka mbele itikadi na sera za vyama.
Kwa mfano, kabla ya kutoka kwao nje kumekuwa na
matamshi kuwa Wajumbe wa CCM madai waliokuwa wakiyatoa Zanzibar kabla ya
kufika Dodoma wamefyata na kushangaa hulishwa kitu gani wanapovuka
bahari kuja Dar es Salaam hadi Dodoma.
Wengine wakasoma Hansard kuhusu michango ya wajumbe ili kuwasuta na kuelezwa huo ndiyo unafiki na uzandiki.
Upande wa upinzani nao ukatupiwa maneno ya usaliti
wa Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar, wakaitwa vibaraka na mawakala wa
utawala ulioangushwa mwaka 1964 huku wengine wakiambiwa Zanzibar si kwao
na hata rangi zao hazifanani na Afrika,
Wakati akitoka bungeni Profesa Ibrahim Lipumba
aliliita Bunge hilo ni la Interahamwe. Tafsiri yake ni mbya sana, haifai
kuelezwa au kutamkwa na kiongozi anayeaminika katika jamii mwenye
kaliba yake kama msomi na mweledi kitaaluma.
Haya yote hayakustahili kutamkwa ndani ya Bunge la
Katiba. Madhali viongozi wa juu wakiwamo wanasiasa na viongozi wa
madhehebu ya dini kuwataka Ukawa warejee bungeni, nafikiri ni wakati wao
mwafaka Ukawa kukaa na kutafakari ushauri uliotolewa ili warejee
bungeni.
Rasimu ya Katiba imesheheni mambo mengi muhimu, yanayohitajika
kwa wakati tulionao. Ikiwa yatakosekana kupatikana mwakani, anaweza
akatokea rais mkorofi, asiyeambilika wala kushaurika akasema hana mpango
wa kuunda katiba mpya hadi miaka 50 mingine ipite na kuiona iliopo
inafaa na kukidhi haja.
Ikiwa hilo litatokea,kundi la Ukawa halitaachwa
kubebeshwa lawama na viongozi wake wataingia katika kurasa za lawama ya
kihistoria kwa kutopima wakati na kusoma kuvuma kwa pepo ili kushika
turufu na piku mkononi mwao.
No comments:
Post a Comment