KADA CHADEMA APIGWA, KUNG’OLEWA MENO

KADA wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika tawi jipya la Misongeni, mjini hapa, Emmanuel Constantine, amenusurika kifo baada ya kushambuliwa na watu wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa CCM.

Katika tukio hilo lililotokea juzi saa 12 jioni, Emmanuel ambaye amefungua jalada polisi Agosti 28, mwaka huu, aling’olewa meno mawili ya juu na kuumizwa sehemu mbalimbali za mwili.

Gazeti hili lilifika katika wodi namba moja ya Hospitali ya Rufaa mjini hapa ambapo kada huyo amelazwa na kuelezwa na mashuhuda kuwa watu hao wakiwa na fimbo na makopo ya rangi, waliing'oa bendera ya CHADEMA kwenye jiwe lililozinduliwa juzi na kisha kulipaka rangi nyingine jiwe hilo.

“Ilipofika saa 12 jioni wakatokea hao jamaa wa CCM wakiwa na fimbo na makopo ya rangi, wakaing'oa bendera na kuitupa kisha wakaanza kupaka rangi walizokuwa nazo, Emmanuel akawasogelea na kuwauliza kwanini wanafanya hivyo, ndipo wakamgeukia na kuanza kupiga,” alisema shahidi aliyejitambulisha kwa jina la Innocent.

Mwenyekiti wa CHADEMA mkoani hapa, Zuberi Kiloko, aliyefika eneo hilo baada ya kada huyo kujeruhiwa, alisema kuwa alimkuta Emmanuel akiwa hajitambui na kulazimika kukodi gari ili kumkimbiza hosipitali.

“Ingawa kulijitokeza usumbufu wa kupata PF3, tunashukuru kuwa hatimae tuliipata na mgonjwa ametibiwa kwa kuwekwa nyaya mdomoni na kushonwa nyuzi sita kwenye taya...ameruhusiwa kurudi nyumbani,” alifafanua.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile alikana kuwa na taarifa hiyo, huku akisema matukio kama hayo ni mengi sana hivyo hawezi kufahamu labda ni walevi waligombana vilabuni.

No comments:

Post a Comment